Habari za Punde

Wahamiaji Haramu Watadhibitiwa -Maalim Seif

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema wahamiaji haramu watadhibitiwa kuingia Zanzibar iwapo kutakuwa na ufuatiliaji wa kila siku kwa wageni wanaoingia pamoja na kuzingatiwa matumizi ya teknolojia ya kisasa. 
Maalim Seif ameyasema hayo huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, wakati alipokuwa na mazungumzo na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu, ambaye alikwenda kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema suala la ufuatiliaji wageni hasa wale wanaoingia ni muhimu kwa Zanzibar, kwa sababu baadhi ya wageni hujifanya wao ni Watanzania waliotokea Tanzania Bara na kuingia Zanzibar, wakati wao si Watanzania.
Amesema tayari wahamiaji haramu wengi wamekamatwa na wengine wamekimbia baada ya kusikia wanafuatiliwa baada ya kuishi Zanzibar kwa muda mrefu wakijifanya ni Watanzani, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara makubwa kwa nchi na raia wake, ikiwemo kuongeza uhalifu.
“Lazima Idara ya Uhamiaji iwe na utaratibu mzuri wa kufuatilia wageni wote wanaoingia Zanzibar kila siku, msisubiri kufanya operesheni maalum kutafuta wahamiaji haramu”, alihimiza Maalim Seif.
Aidha, aliipongeza Idara ya Uhamiaji Zanzibar kwa kuweza kupiga hatua kubwa katika kuondoa urasimu wa upatikanaji hati za kusafiria uliokuwepo siku za nyuma ambapo sasa muombaji hutumia muda usiozidi wiki mbili kuweza kuipata, jambo ambalo halinadubi kuendelezwa.
Amesema ipo haja kwa Idara hiyo kufungua vituo vidogo katiba baadhi ya maeneo ambayo kumekuwa na uingiaji mkubwa wa wageni, ikiwemo katika mkoa wa Kaskazini Pemba, ili kuepusha uingiaji holela wa wageni wanaojihusisha na vitendo viovu, ikiwemo biashara ya dawa za kulevya.
Maalim Seif amemhimiza Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar kuweka mkazo mkubwa zaidi katika kuwapatia mafunzo watendaji wa Idara hiyo, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ulio mkubwa zaidi.
Nae Kamishna Sururu amesema Idara hiyo imejipanga vizuri katika kuhakikisha inafanya kazi zake kwa ufanisi na kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na kupanua shughuli zake katika maeneo mengi zaidi hapa Zanzibar.
Amesema miongoni mwa mikakati yao, hivi sasa wamo katika hatua za kuandaa utaratibu wa kuwarahisishia wasafiri kukamilisha taratibu za kuingia na kutoka nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa ambao utakuwa tayari hivi karibuni.  
Ameahidi kuwa Idara hiyo itafanya kazi kwa mashirikiano makubwa miongoni mwa watendaji wake na wananchi na matarajio yao ni kuwa wataweeza kuleta mafanikio na mabadiliko makubwa katika kipindi kifupi kijacho.
 

1 comment:

  1. Isiwe wahami aji haramu wannje tuna piga kelele wandani tuna waacha, tuzibiti humiaji wandani unatisha unguja, baada yamiaka 20 itakuwa hakuna eneo lawazi na wanao jenga holela ni hawa wahamiaji haramu wa ndani maali umesema na sisi tuna kuunga mkono

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.