Habari za Punde

Hatutaki usingizi huu Bunge la Katiba

Na Salim Said Salim
 
RAIS Jakaya Kikwete ametangaza majina 201 ya wajumbe kutoka makundi mbalimbali nchini walioomba kuteuliwa ili waungane na wabunge wa Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Kabla ya kutangaza majina hayo kwa niaba ya Rais Kikwete, Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Florence Turuka, alisema kazi ya kuwapata wajumbe wa Bunge hilo ilikuwa ngumu kwani walioomba walikuwa 3,754 na waliotoswa ni 3,553.
Hadi sasa Rais Kikwete ameshanawa mikono kama Pilato, na sasa analala usingizi mnono, akiwatazama wajumbe aliowatupia mzigo ili wajadili mustakabali wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni wa nchi hii. Hivyo wakiboronga; hukumu iko kwao, si Rais Kikwete.
Kwa msingi huo huo, mosi; hatutarajii tuone tena kuna watu wanasinzia na kulala usingizi katika Bunge hili Maalumu kama tulivyowaona wabunge fulani wakubwa kwa nyadhifa zao, wakipiga usingizi hadi wakafikia kukoroma.
Pili; lakini muhimu. Hatutaki kuona tena, usingizi huu wa ‘Sasa nitawauliza; wanaoafiki waseme ndiyo’. Utasikia wengi wenye chama chao wakikurupuka usingizini na kujibu; ‘Ndiyoooo’. Wasioafiki waseme siyo’….Hatutaki! tunataka kama hakuna maafikiano, ‘zipigwe kura za siri’.
Pamoja na wabunge wa Bunge la Muungano na Wawakilishi wa Zanzibar, lakini macho na masikio ya Watanzania nikiwemo mimi, kwa sehemu kubwa sana tunawaangalia na kuwategemea wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali, walioteuliwa ili wawe mawakili wetu watusemee.
Walioteuliwa ni kutoka taasisi zisizokuwa za kiserikali, taasisi za kidini, kundi la vyama vya siasa, taasisi za elimu, watu wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wafugaji, vyama vya wavuvi, vyama vya wakulima na watu wenye malengo yanayofanana.
Kama miongoni mwa Watanzania milioni 50, wajumbe hao 201 wameteuliwa; ni matarajio yangu watathamini uteuzi huo, na hivyo katika mjadala huo wa rasimu ya pili ya Katiba, watajikita kuangalia mustakabali na uzalendo wa taifa hili; ili waandike historia muhimu maishani mwao.
Naamini wajumbe hao watatamani kuandika historia za maisha yao ili waje wakumbukwe na vizazi vya miaka 50 ijayo, ambapo vizazi hivyo vitasoma, vitasikia, na kushuhudia Katiba nzuri, wakiwapongeza kuwa walifanya kazi nzuri na kusujudu makaburi yao badala ya kuwalaumu.
Lakini kama wajumbe hao watajadili usingizi wa itikadi zao, dini zao, masilahi ya uongozi wa watu fulani binafsi, ukanda, ukabila bila kujali utaifa; vizazi vijavyo vitawalaumu kwa kutengeneza Katiba mbaya na watathubutu kutandika bakora makaburi yao.
Tunawaonya wajumbe waliochaguliwa, wasiwe watu watakaokwenda na mawazo waliyofundishwa kwa kitu kidogo au takrima, ili Katiba hiyo isipatikane kwa lengo la mwanya wa kusema, wajumbe wameshindwa kuleta Katiba mpya, hivyo tuirudie ya awali.
Kutopatikana kwa Katiba mpya, kutasababisha msuguano mkubwa miongoni mwa jamii nchini Tanzania, kwa sababu iliyopo imeonyesha upungufu mkubwa ambao kwa namna moja au nyingine, imekuwa ikiwanyima haki wananchi na hasa wapiga kura.
Ni rai yangu wajumbe wafahamu kwamba, waingie ‘mjengoni’ wakijua kuwa kama watafanya ‘madudu’ yasiyotarajiwa kutupatia Katiba mpya, waelewe wananchi bado tuna dume na jike la karata (kura ya maoni), ambapo tutapiga kura ya kuikataa.
Aidha, ni onyo letu kwa vyombo vya dola, visithubutu kufanya uumini na ushiriki wao wa kukiegemea chama tawala kiasi cha kusababisha vurugu ambazo tumekuwa tukizishuhudia katika mabunge yaliyopita.
 
Chanzo - Tanzania Daima

2 comments:

  1. mm nionavyo wabunge na wawakilishi wa znz wana.tatizo la kutojiamini lkn sio wote na waangaalia maslahi yao na pili znz tuna unafiki na kubadilika kama kinyonga lkn kama tulowatuma wakaendea tulowatuma basi mabadiliko hayazuiliki

    ReplyDelete
  2. Usingizi ndo uwepo tuuu,maana jengo limejaa vipooza hewa(bardiiiiiii ndani.) na madam wale watu ngangari uwajuwao hawakupewa nafasi ya uteuzi kuwa wawemo basi basi waliobakia wote ni mikoromo tuuu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.