Habari za Punde

Jaji Mshibe:Wazanzibari mkiichezea bahati mtajuta


Baadhi ya Washiriki wa Kongamano, la Kuchangia Mjadala wa Katiba uliofanyika katika Ukumbi wa Chjuo Kikuu cha Zanzibar SUZA na kuwashirikisha Wananchi mbalimbali na Wanasiasa na Viongozi wa Dini Zanzibar kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba a 



WAKATI mkutano maalum wa bunge la katiba ukitarajiwa kuanza Februari 18, wajumbe kutoka Zanzibar wametakiwa kuweka mbele maslahi ya nchi badala ya vyama.

Aidha wameonywa kwamba kama fursa hiyo wataichezea  watajuta maishani mwao pamoja na kusababisha mashaka makubwa makubwa kwa vizazi vyao.

Wakichangia mjadala wa katiba uliofanyika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kampasi ya Vuga, washiriki, walitahadharisha kwamba kama Zanzibar itazembea na kuweka mbele maslahi ya vyama, matatizo yaliyopo sasa yatakuwa makubwa zaidi siku za usoni na wakati huo hakutakuwa na mtu wa kuyasema kwa sababu fursa ilitolewa ikachezewa.

Akifungua mjadala huo, Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, Mshibe Ali Bakar, aliwatoa hofu wajumbe akisema wasihofu kuzungumza kwa sababu tu miongoni mwa wajumbe wamo viongozi wa serikali na vyama vya siasa.

Alisema katika bunge hilo watu wote sawa bila kujali kiongozi au raia wa kawaida na kwamba wote wana haki ya kuzunguza na kutoa michango inayojenga bila woga.

Hata hivyo, alitahadharisha kwamba kama Wazanzibari hawaweka kando misimamo ya vyama vyao, athari itakayoletwa na matokeo ya katiba mpya ni kubwa zaidi.

Mwakilishi wa wanawake, Asha Bakar Makame, alihimiza umoja na mshikamano miongoni mwa wajumbe bila kujali itikadi.
Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, alionesha hofu na sheria ya mabadiliko ya katiba, akisisitiza umuhimu wa kuwepo usawa kati ya Zanzibar na Tanganyika.

Mwakilishi wa Magomeni, Salmin Awadh yeye alitilia wasi wasi uwezo wa Zanzibar kuchangia serikali ya Muungano iwapo kutakuwa na mfumo wa serikali tatu, akisema Zanzibar haitakuwa na uwezo wa kuchangia na kwamba hali hiyo inaweza kuvunja muungano.

Hata hivyo, mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole, alisema mapato ya serikali ya Muungano  yameanishwa ndani ya rasimu jinsi yanatavyopatika, akisisitiza kwamba taasisi za fedha nchini (BoT, TRA na ZRB) zimethibitisha kwamba fedha hizo zitapatikana.

Aidha alisema Muungano umejengwa katika misingi mitatu muhimu ambayo ni usawa, mshikamano na kusaidiana akisema nchi moja ikipata shida ni wajibu wa mshirika wake kusaidia.
“Watanganyika wakipata shida, rasimu imewawajibisha wenzao wa Zanzibar kuwasaidia kwa hali na mali na hivyo hivyo iwapo Wazanzibari watapata shida,” alisema.


Mjadala huo uliowashirikisha wasomi, wafanyabiashara, wanasiasa,  wananchi, baadhi ya wajumbe wa bunge maalum la katiba na Wawakilishi uliandaliwa na Taasisi ya Utafiti na Sera (ZIRPP) kwa msaada wa Foundation for Civil Society.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.