Habari za Punde

Waziri Mbarouk awataka wamiliki hoteli za kitalii kuajiri wazalendo

Na Mwashamba Juma
MAGEUZI katika uwajibikaji yanahitajika hasa katika sekta ya utalii Zanzibar ili kuwainua wazawa na changamoto ya ajira.

Waziri wa Habari, Utamaduni Utalii na Michezo, Mhe. Said Ali Mbarouk, alisema hayo wakati akizungumza na wahitumu wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii (ZIToD) katika mahfali ya tano ya chuo hicho.

Alisema wakati umefika kwa taasisi za utalii nchini kutoa kipaombele cha ajira kwa wazawa badala ya nafasi kubwa kupewa wageni.

Alisema Wazanzibari wana uwezo na kumudu nafasi hizo endapo watapatiwa taaluma na uzoefu katika fani zao.

Aliwataka wahitimu kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu kwa ambao watabahatika kuajiriwa ili kuonesha uwezo kwa waajiri wao pamoja na kukabiliana na soko la ajira lenye ushindani mkubwa.

“Ajira sio lazima serikalini, bali hata kujiajiri mwenyewe kwa kuunda vikundi kutokana na taaluma za fani zenu, tumieni ujuzi wenu kwa kuwa wabunifu ili mujiajiri na kuajiri wengine,” alisema.

Alitumia nafasi hiyo kupongeza juhudi za serikali kwa kukiweka chuo hicho kama sehemu ya Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) na kuongeza kuwa bidiii zinahitajika kukuza fani ya utalii katika chuo hicho ili kukabiliana na ushindani katika soko la ajira kwani fani ya utalii inasomwa hadi ngazi ya shahada ya uzamivu (PhD).

Alisema katika kuendana sambamba na mahitaji ya soko la ajira kwenye sekta hiyo chuo kimeongeza majengo na fani mbalimbali, hasa katika masuala ya uongozi wa  mahoteli na watembeza watalii.

Akitoa mwelekeo wa maendeleo ya chuo, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Khamis Mussa, alisema sekta ya utalii ni moja ya sekta kiongozi katika uchumi wa Zanzibar na kuongeza kuwa chuo kinajitahidi kutoa elimu yenye ubora ili kukabiliana na ushindani katika soko la ajira duniani.

Alisema katika kuongeza nguvu kwenye sekta ya utalii baraza lina mpango wa kuanzisha chuo kama hicho katika visiwa vya Pemba ambacho kitatoa wanafunzi wenye ubora ambao wataweza kushindana katika soko la ajira.

Aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazokikabili chuo hicho ikiwemo kuongeza kompyuta.

Kuhusu changamoto ya mmong’onyoko wa ardhi katika maeneo karibu na fukwe za bahari pamoja na tatizo la usafiri kwa wanafunzi chuoni hapo, alisema chuo kinazifanyia kazi na kuadihi ndani ya kipindi kifupu matatizo hayo yataondoka.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa chuo hicho, Zulekha Kombo, alisema chuo kinajitahidi kutafuta wafadhili kwa lengo la kujiboresha.

Nao wa wanafuzi hao waliahidi kuzitumia taaluma zao kwa kutoa huduma zenye uobora katika maeneo yao ya kazi.

Jumla ya wanafunzi 650 wa fani mbalimbali walitunukiwa vyeti.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.