Habari za Punde

Vurugu chaguzi za udiwani · Mbeya Mbunge wa CCM ajeruhiwa · Bagamoyo gari lakamatwa likisafirisha silaha

Na Mwandishi wetu, MBEYA
MBUNGE wa Mbeya Vijijini, Lackson Mwanjali (CCM) amejeruhiwa baada ya kushambuliwa na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Habari zinasema, Mbunge huyo alishambuliwa pamoja na wenzake jana asubuhi katika uchaguzi wa udiwani kata ya Santilya.

Mbunge huyo na wenzake walishambuliwa baada ya kuzuka vurugu kati ya wafuasi wa CCM na Chadema waliokuwa wamejazana katika vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo, vurugu hizo zilizimwa na polisi waliokuwa wakifanya doria kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa salama.

Watu saba wanaoaminika kuwa wafuasi wa CHADEMA wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio la kumshambulia Mbunge huyo.


Na huko Bagamoyo gari nilalosadikiwa kuwa la CCM  limekamatwa na wafuasi wa Chadema likidaiwa kuwa na silaha za jadi yakiwemo mapanga na kuwashambulia watu waliokuwemo pamoja na kuliharibu vibaya gari hilo.
Chama cha Mapinduzi mkoani wa Pwani kimelaani vurugu hizo zilizotokea kata ya Magomeni kikidai zilifanywa na  wafuasi wa  CHADEMA na CUF.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisi za CCM wilaya hiyo, Katibu wa CCM mkoa wa Pwani, Sauda Mpambalioto, alisema wafuasi hao mbali ya kuharibu na kuwapiga wafuasi wa chama chao pia waliiba fedha na simu.
Alisema gari lililoharibiwa lina namba za usajili T 112 BBF ambapo pia wafuasi hao wa vyama vya upinzani walitumia silaha za jadi kuwajeruhi wafuasi wa CCM na viongozi wao.
"Tunashangaa ni kwanini wanafanya fujo kwani kila kitu kiko wazi kama waliona sisi tumekiuka taratibu wangefuata sheria kuliko kufanya vurugu ambazo zimesababisha gari letu kuvunjwa vioo na kuharibika vibaya,”alisema.

Kwa upande wake moja ya viongozi wa CUF ambaye alijitambulisha kwa jina la Hassan Kingwelu, alisema silaha hizo zilikuwa ndani ya gari la CCM kwa lengo la kuvuruga uchaguzi.

Msimamizi wa uchaguzi wa kata ya Magomeni, Mahafudh Jembe, alisema hadi wakati huo alikuwa bado hajapokea taarifa yoyote kuhusu vurugu hizo.
Alisema uchaguzi ulifanyika baada ya diwani wa kata hiyo, Jafar Yusuf, kufariki dunia.


Chaguzi za udiwani zilifanya jana katika kata 27 za Tanzania Bara baada ya madiwani wake kufariki dunia au kufukuzwa na vyama vyao.

2 comments:

  1. kiukweli sumu zinazopandikizwa ndani ya mioyo ya baadh ya vijana itakuja kutugharimu.

    ReplyDelete
  2. Mungu ikumbuke Tanzania kwni kila kukicha balaa tupu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.