Na Kauthar Abdalla
BODI ya Mikopo
ya Elimu ya Juu
Zanzibar, imesema uhaba wa fedha umesababisha wanafunzi wanaosoma vyuo
vya ndani kuchelewa kupata mikopo na badala yake kipaumbele kimetolewa kwa
wanafunzi walioko nje ya nchi.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi ofisini kwake
Majestik, Mkurugenzi bodi
hiyo, Iddi Khamis
Haji, alisema si kweli kwamba
bodi ya mikopo imekataa kuwapa fedha wanafunzi wa vyuo vya ndani, isipokuwa
kikwazo ni upatikanaji mdogo wa fedha kutoka wizara ya fedha.
Hata hivyo, alisema wapo baadhi ya wanafunzi wanaosoma vyuo vya ndani
wameshalipiwa baadhi ya fedha.
Alisema bodi ilibaini kwamba kama ingechelewesha fedha kwa wanafunzi
walioko ugenini, wangepata shida na kushindwa kumudu mahitaji yao, ikiwemo
gharama za malazi.
Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014, bodi ilitengewa
shilingi bilioni 9.1 lakini hadi kufikia Januari 2014, fedha zilizoingizwa
zilikuwa shilingi bilioni 2.1 pekee.
Hata hivyo, alisema bodi itawalipia wanafunzi hao mara fedha
zitakapopatikana na kwamba hatarajii chuo chochote kuwafukuza wanafunzi.
Aidha aliwataka wanafunzi na wazazi kuwa wastahamilivu katika kipindi
hichi ambacho bodi inasubiri fedha kutoka hazina.
Akizungumzia deni la bodi kwa wahitimu, alisema ni wahitimu 300 pekee
kati ya 2800 ndio walioanza kulipa mikopo yao.
No comments:
Post a Comment