Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya CCM,Ridhiwani Jakaya Kikwete (kushoto) akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Mindukene,Kata ya Talawanda ndani ya Jimbo la Chalinze leo Machi 18,2014.Katika Mikutano yake kwenye Vijiji vya Mindukene, Msigi na Kisanga ndani ya Jimbo hilo,Ridhiwani Kikwete ameahidi kuhakikisha vijiji vyote kwenye jimbo hilo vinakuwa na matrekta ili kuboresha kilimo.Picha na Othman Michuzi
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya CCM,Ridhiwani Jakaya Kikwete akisalimiana na jambo na wananchi wa Kijiji cha Kisanda,Kata ya Talawanda ndani ya Jimbo la Chalinze.Picha na Othman Michuzi
MGOMBEA wa Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye
Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete ameahidi
kuhakikisha vijiji vyote kwenye jimbo hilo vinakuwa na matrekta ili kuboresha
kilimo kiwe na tija.
Alitoa ahadi hiyo wakati wa mikutano ya kampeni kwenye vijiji
vya Mindukene, Msigi, Kisanga vyote vikiwa kwenye kata ya Talawanda.
Kikwete alisema kuwa wakulima wengi bado wanatumia jembe la
mkono ambalo haliwezi kuwaletea manufaa wala kuboresha kilimo ambacho ni
tegemeo lao.
“Nikianikiwa kupata ubunge nitahakikisha kila kijiji kinakuwa
na matrekta kwa ajili ya kuwa na wakulima ambao wataweza kulima kwa faida kwa
ajili ya chakula na ziada kuuza ili kujiongezea kipato,” alisema Kikwete.
Akizungumzia changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji
alisema kuwa atahakikisha anazikutanisha pande zote ili kujua chanzo cha
migogoro hiyo.
“Tatizo kubwa ni viongozi kushindwa kuzikutanisha pande
zinazohusika badala yake wanaongea na upande mmoja jambo ambalo haliwezi
kumaliza migogoro hiyo ambapo njia pekee ni kuwa na matumizi bora ya ardhi kwa
kutenga maeneo kwa wakulima na wafugaji,” alisema
Kikwete.
Aidha alisema kuwa migogoro hiyo inatokana na wafugaji
kuingia kinyemela pasipo kufuata taratibu bila ya kupitia kwenye mikutano mikuu
ya serikali za vijiji.
Katika hatua nyingine aliwataka wazazi kuepukana na tabia ya
kuuza kiholela maeneo yao hali ambayo itasababisha vijana kukosa ardhi kwa
ajili ya kilimo na makazi.
Aliongeza kuwa atahakikisha anaboresha masuala mbalimbali
ikiwemo sekta ya elimu, afya, miundombinu, kilimo, mikopo kwa vijana na akinamama, uzinduzi rasmi wa
kampeni unatarajiwa kufanyika kesho Aprili huko Chalinze na uchaguzi utafanyika
Aprili 6 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment