Habari za Punde

Bomu lajeruhi 17 Arusha

Na Joseph Ngilisho,ARUSHA
WAKATI wakaazi wa jiji la Arusha wakiwa bado na kumbukumbu ya kupoteza wapendwa wao katika miripuko ya mabomu ya kurushwa kwa mkono katika kanisa la Katoliki Olasiti na katika kampeni za uchaguzi, uwanja wa Soweto mwaka jana, watu 17 wamejeruhiwa vibaya na bomu la kutegwa wakati wakiangalia mpira katika baa ya Arusha Night Park iliyopo Mianzini jijini Arusha.

Kati ya majeruhi hao, 12 wamelazwa katika hospitali ya Mkoa Maunt Meru na mmoja hospitali ya Selian, huku watano wakiruhusiwa, baada ya kupatiwa matibabu.

Aidha, wagonjwa 11 walioko hospitali ya mkoa Mount Meru, mmoja  hali yake ni mbaya, kutokana na kusagika mfupa katika mguu wake wa kulia, hata hivyo uongozi wa hospitali hiyo unafanya mawasiliano na Wizara ya Afya ili kujua kama kuna uwezekano wa kuhamishiwa katika hospitali ya rufaa KCMC mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza kwenye wodi ya majeruhi hospitalini Mount Meru, Obeid Mbasha, alisema yeye alikwenda kwenye baa hiyo kuangalia mpira , ila ilipofika majira ya saa 1:30 na saa 2:00  usiku alisikia mripuko mkubwa na kujikuta yupo chini huku wengine wakilia na kukimbia ovyo.

Kwa upande wake mmoja wa majeruhi waliopatwa na mkasa huo, ambaye hakutaja jina lake alisema alikuwa akiangalia mpira, ghafla alisikia kishindo kikubwa, kilichoambatana na moshi hali ambao iliwashtua na kujikuta wakiwa wameumia.


Mmoja wa wahudumu wa baa hiyo, Aneth Mushi, alisema yeye alikuwa amekwenda jikoni kuchukua chakula ili awapelekee wateja wake waliomwagiza, wakati akibeba sahani, ghafla alisikia kishindo na kelele za watu, hivyo alipoona hivyo alimwaga chakula na kukimbia.

Mganga Mkuu wa mkoa wa Arusha, Dk.Frida Mokiti, akizungumza baada ya kutembelea majeruhi, alisema hospitali ya mkoa walipokea majeruhi 17 ambao kati yao mmoja alikwenda Selian na watano waliruhusiwa baada ya kutibiwa.

"Lakini hapa Mount Meru wamebaki  watu kumi na moja  ambao kati yao wanaume nane na wanawake watatu ila majeraha yao makubwa yapo miguuni na kwenye  mapaja," alisema.

Alisema hata hivyo mgonjwa mmoja ambaye hakumtaja jina lake, alisema hali yake siyo nzuri, kwani ameumia sana na kusagika mfupa mdogo, hivyo wanafanya mawasiliano na watu wa Wizara ya Afya wapate maelekezo ya kufanya au kama kumuhamishia hospitali watajua.

Mganga wa zamu katika hospitali ya Selian mkoani Arusha, Dk.Peter Mabula, alisema  amepokea majeruhi mmoja na hali yake inaendelea vizuri.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Liberatus Sabas aliyekuwa eneo la tukio muda mwingi na kikosi cha ukaguzi wa mabomu, alisema hawezi kuzungumza chochote.

Kwa upande wa mkuu wa mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo alisema kuwa mripuko huo ni wa bomu linaloonekana kutengenezwa kienyeji na kwamba wanaendelea kushirikiana na wataalamu wa mabomu kutoka jeshi la wananchi JWTZ.

Alisema tukio hilo limetokea majira  ya saa 2:00 usiku, wakati watu wakiwa wanaangalia mpira na ndipo wakasikia kishindo kikubwa na kinachosadikiwa kuwa ni bomu la kutengenezwa kwa mujibu wa taarifa za awali.

Wahudumu watano waliojeruhiwa katika baa hiyo wametambulika kuwa ni Suzani Jacob (31)mkazi wa Mianzini, Joyce Williamu (29) mkazi wa Moshono, Loice John(29) mkazi wa Sanawari, Evance Charles (24) na Peter James(25) mkazi wa Ilboru.

Akizungumza bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Matius  Chikawe, alisema uchunguzi wa awali unaonesha bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

Alisema watu walioshuhudia walimuona mtu mmoja akiweka bomu hilo na kuliripua na baadae akaenda kwenye baa ya jirani ya Washington na kutega bomu jengine lakini halikuwahi kuripuka.


Alisema wataalamu wa bomu wamepelekwa jijini humo kufanya uchunguzi na kuwabaini wanaohusika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.