Na
A K Khiari
Wazungu
wana msemo mmoja, silence is golden, ukimaanisha kwamba kunyamaza kimya wakati
mwengine huwa kama ni dhahabu.
Watu
wanaweza kusema, wakanena, wakan’gaka, wakatamka lakini wengine huweza kukaa
kimya bila ya kusema chochote. Si kwamba hawana la kusema bali wameangalia hali
iliyopo na mazingira yalivyo na kwa kutumia hekima wakaona bora wanyamaze
wasiseme. Si kwamba hawawezi kusema, laa hasha basi tu walijiamulia tu
kujinyamazia.
Mwanafalsafa wa kigiriki, Plato, nae
pia aliwahi kunukuliwa akisema: ‘Wenye hekima husema kwa sababu wana sababu ya
kusema, majahili (husema) ili wapate tu na wao kusema’ Yaani almuradi na mimi
nimeonekana kusema.
Kunyamaza
kimya bila ya kusema wakati wengine wakisema ni moja katika mambo yanayohitajia
hekima.
Hekima ni kitu adhimu sana katika maisha ya binadamu na ndiyo maana
Allaah Subhaanahu Wata’ala Amesema ndani ya Qur’aan kwamba ‘Humpa hekima
amtakae na humuondoshea hekima amtakae na aliyepewa hekima basi amepewa kheri kubwa’ ( Al Baqarah 269).
Nabii
Suleiman ‘Alayhis Salaam alipopewa nafasi ya kuchagua jambo lolote kutoka kwa Muumba
alichagua hekima, hakuchagua mali wala utajiri au utawala alimuomba Allaah
Subhaanahu Wata’ala amjaalie awe na hekima.
Mtume wetu Muhammad, rehma na amani
zimwendee, alituruhusu tuwe na husda (kitu ambacho ni haramu kimsingi) katika
mambo mawili tu: kwa mtu aliyejaaliwa na Mwenyezi Mungu mali kisha akawa
anatumia utajiri wake kwa haki ( huyu tuwe na husda naye kwa kutaka kuwa kama
yeye) na yule mtu aliepewa hekima na
akawa anaitumia hekima aliyojaaliwa
na kuifundisha kwa watu ( huyu pia tunaweza kuwa na husda naye). Bukhaari na
Muslim
Kilichonisukuma
kuandia waraka huu mfupi ni kwa jinsi ninavyoshuhudia yanayojiri na yanayotokea
katika Bunge la Katiba linalofikia tamati huko Dodoma ambapo vitu viwili
nilivyogusia hapo juu vilipokosekana.
Madhara ya kusema tu bila ya kuwa na
hekima yanaweza kuwa makubwa na tumeona mifano michache ya kauli za
waliobahatika kusema katika bunge la katiba ambao ima waliamua kwa maksudi
kuiweka hekima pembeni au masikini hawakufahamu kwamba kabla ya kusema
unahitajia kuwa na hekima.
Yaa
laiti kwamba walioteuliwa wangelikuwa wamepata kheri ya hekima basi tungeliona
kheri hii ikitumika Dodoma,.Yaa laiti walioteuliwa wangeliamua kunyamaza basi
tungeliweza kuwajua ni wapi waliojaaliwa hekima na wepi waliokosa kheri hii na
kuangukia katika kundi ambalo waarabu wana msemo husema atakaposema mtu jahili
basi usimjibu kwani jibu lake ni kunyamaza kimya.
Baya
zaidi ni kuona mpaka viongozi wa dini ambao tuliwatarajia kuwa mstari wa mbele
kuonesha kuwa na hekima nao wametumbukia katika dimbwi la kukosa busara kwa
jinsi ya kauli za na matamshi yao. Viongozi hawa wa dini kama wangelitumia
fursa ya kuzungumza na kudarisisha Bunge kuhusu hekima basi wangelikuwa
wamefanya kazi kubwa sana kwani ndiyo kitu muhimu klilichokosekana kule.
Ni
jambo la kusikitisha sana kuona fursa ya kutumia hekima imekosekana bungeni na
hali hii inaakisi hali halisi ya wananchi wa nchi hii walivyokosa upeo wa kuwa
na hekima. Tukichukulia sampuli chache ya yanayotokea Bungeni basi inatupa
picha halisi kwamba Wananchi wetu sasa hawana hekima! Na hili ni janga kubwa
kwa taifa!.
Nadhani
umefika wakati tuandae mtaala maalum ambapo somo hili la hekima na busara lianzwe
kusomesha maskulini, misikitini, madarasani na hata makanisani ili kuweza kukiokoa
kizazi chetu na kijacho na janga kubwa la kukosa hekima kwani madhara yake pia yatakuwa makubwa pia kama yanavyoonekana kwenye bunge la katiba!.
No comments:
Post a Comment