Na Kija Elias, Arusha
Viongozi wa bodi ya chama cha wakulima nchini (TFA)
wamefukuzwa madarakani na mkutano mkuu maalum, kutokana na matumizi mabaya ya fedha
za ofisi na kukisababishia hasara chama hicho zaidi ya shilingi bilioni tano.
Mkutano huo mkuu maalum uliohudhuriwa na wanachama
zaidi ya 500 kutoka matawi 12 yaliyopo nchini ulichukua maamuzi hayo magumu
baada ya kuchoshwa na ubadhirifu ambao umekuwa ukifanywa na watendaji hao.
Hasara iliyopata chama hicho ni pamoja na Mwenyekiti
wa Bodi wa
TFA, Elias Mshiu, kujiidhinishia nyumba kubwa ya
kisasa iliyopo barabara ya Haile Selasie, kiwanja namba 57 kilichopo katikati
ya jiji la Arusha na baadae kuomba kupewa nyumba hiyo kama
zawadi pamoja na mafao ya shilingi milioni 65 baada ya kustaafu kwake.
Mwenyekiti wa kamati iliyoundwa na wanachama
kuchunguza TFA, Maynard Swai, alibainisha hayo katika taarifa yake aliyoisoma
katika mkutano mkuu maalumu wa chama hicho uliofanyika makao makuuu ya TFA, Arusha.
Wajumbe kwa kauli moja waliazimia kuwaita Mwenyekiti
na Wakurugenzi wa bodi na utawala wa TFA uliodumu kwa zaidi ya miaka hamsini
madarakani.
Swai alisema TFA, imeipata hasara za mfululizo mwaka
hadi mwaka kutokana na Mwenyekiti kuwa na nyadhifa mbili kwa wakati mmoja kuvaa
koti la Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti TFA kwa kipindi kirefu na hivyo kuwa
na mamlaka ya kusaini mikataba na ajenda za vikao pekee bila ya kuwepo Katibu Mtendaji
wala Wakaguzi wa mahesabu wa ndani na nje.
Alisema matumizi mabaya ya madaraka yamesababisha
hasara kubwa kwani viongozi wa bodi na utawala umekuwa na matumizi makubwa
kuliko mapato huku wakichukua mikopo mikubwa kwa riba kubwa na kushindwa
kulipa.
Kamati hiyo pia ilimtuhumu Mwenyekiti kujiidhinishia
malipo makubwa ya mshahara wake,posho na masurufu mengine licha ya kwamba kila
mwezi alikuwa akilipwa mshahara wa dola 1000 za Marekani sawa na shilingi milioni
1.6.
Mshiu pia anatuhumiwa kumiliki kampuni binafsi ya
ulinzi Apex Security Service Ltd na kampuni inayojighulisha na usafi wa mazingira,
Aresco na kujipa zabuni ya ulinzi na usafi katika makao makuu ya TFA bila
kufuata taratibu za kisheria ya manunuzi na ugavi.
Kamati hiyo ya uchunguzi ilibaini kushindwa kwa
Mwenyekiti wa bodi na mtandao wake kuinusuru kampuni ya TFA na kuisababishia
hasara ya mabilioni ya fedha na hakuna hatua endelevu alizozichukua ili kuinusuru
TFA.
Mshiu alisema alianza kazi TFA akiwa na umri wa miaka
18 na baadae kusomeshwa hadi chuo kikuu huku akiwa ameikuta TFA na mtaji wa shilingi
milioni 200 na sasa ameondolewa madarakani kibabe huku akiwa ameacha mtaji wa
zaidi ya shilingi bilioni 22 na matawi
kumi na mbili nchini nzima.
No comments:
Post a Comment