Habari za Punde

Balozi Seif Azungunzxa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Huawei.

Na Othman Khamis Ame OMPR.
Kampuni ya Kimataifa ya mawasiliano ya Teknolojia kutoka Nchini Jamuhuri ya Watu wa China ya Huawei Technology ambayo tayari imeshafungua tawi lake Mjini Dar es salaam imeonyesha nia ya kutaka kusaidia Zanzibar kimaendeleo katika mfumo wa kisasa wa  Teknolojia.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Nchini Tanzania Bwana Bruce Zhang alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Sei Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Bruce alisema Kampuni ya Huawei Technologies ambayo imepanga kutumia kiasi cha Dolla Bilioni Tano { U$ 5,000,000,000 } ndani ya kipindi cha miaka mitano katika kutekeleza miradi  ya mafunzo ya Teknolojia, fursa za masomo ya nje na Afya ikilenga zaidi kwa wananchi wakipato cha kawaida.

Alisema mafunzo ya Teknolojia ya kisasa tayari yameshaanza kutolewa na Taasisi hiyo kwa kuwapatia watendaji wa makampuni yanayotoa huduma za simu sambamba  na wanafunzi maskulini ili kuwajengea uwezo wa kazi kupitia mfumo wa kisasa wa mawasiliano.

Alieleza kwamba miradi kadhaa ya kielimu imeanzishwa na taasisi hiyo kuwapatia mafunzo wanafunzi wa  vyuo na skuli mbali mbali nchini Tanzania zikiwemo fursa za nje ya nchi pamoja na kutafuta wanafunzi  wenye vipaji maalum watakaowezeshwa kujengewa uwezo zaidi wa kielimu.

“ Tumekuwa na utaratibu wa kila mwaka ndani ya Kampuni yetu kutenga bajeti maalum kwa ajili ya mafunzo kwa wafanyakazi wa taasisi za mitandao, wanafunzi, utoaji wa vifaa kama Kompyuta pamoja na misaada katika sekta ya afya “. Alifafanua Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Huawei Technologies.


Aidha Bwana Bruce Zhang alifahamisha kwamba Kampuni yake kwa kushirikiana na taasisi za Teknolojia ya mawasiliano zimekuwa zikiendesha shindano la kutafuta mabingwa wa mitandao ya Kompyuta  { ITC – Star } ili kuzalisha wataalamu zaidi katika fani hiyo muhimu hivi sasa.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi  aliueleza ujumbe huo wa Kampuni ya Huawei Technologies kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa iko katika kipindi cha mpito ikijiandaa na mfumo wa matumizi ya Teknolojia ya kisasa ya mawasiliano { E Government  } katika utendaji wa Wizara zake zote.

Balozi Seif aliutaka uongozi wa Kampuni hiyo kujitayarisha na maombi ya miradi itakayoweza kuwekeza  na taasisi hiyo hapa Zanzibar ili kwenda sambamba na Serikali katika mfumo wa matumizi hayo ya teknolojia ya kisasa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi wa Huawei Technologies kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila msaada ili kuona malengo la Kampuni hiyo yanafaidisha pande zote mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.