HOTUBA YA WAZIRI WA
KATIBA
NA
SHERIA MHESHIMIWA
ASHA-ROSE MTENGETI MIGIRO
(MB) AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO
NA MAKADIRIO YA MAPATO
NA MATUMIZI YA FEDHA KWA
MWAKA 2014/2015
A.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako tukufu na
Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, naomba kutoa hoja kwamba
Bunge lako tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Mpango na Makadirio
ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/2015.
2.
Mheshimiwa Spika, ninasimama mbele ya Bunge lako tukufu kwa mara ya kwanza toka niteuliwe na
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Kwa hiyo kabla ya kuwasilisha Mpango na
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa
mwaka 2014/2015, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa
kunipa heshima hii kubwa. Ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais na Watanzania
wenzangu wote kwamba nitafanya kazi kwa bidii, uadilifu na kujituma kwa uwezo
wangu wote.
3.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa uniruhusu nitoe pole zangu za dhati kwako kufuatia vifo vya wabunge
mahiri, Mheshimiwa Dkt. William Augustao Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kalenga
na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania; na Mheshimiwa
Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Chalinze. Mungu
azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
4.
Mheshimiwa Spika, ninayo furaha kuwapongeza wabunge
wenzangu ambao ni wapya, Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, kwa kuchaguliwa kuwa
Mbunge wa jimbo la Chambani; Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa kwa kuchaguliwa
kuwa Mbunge wa jimbo la Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete kwa
kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Chalinze. Ninawatakia kheri na mafanikio
katika majukumu yao mapya.
5.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee natoa pongezi na shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa
Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mbunge wa jimbo la Mpanda Mashariki, na Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kwa hotuba yake ambayo imetoa mwelekeo
wa ujumla wa shughuli za Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
6.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii pia kutoa shukurani zetu za dhati kwa Waheshimiwa
Wajumbe wote wa Kamati ya Bunge ya Katiba,
Sheria na Utawala chini ya uongozi mahiri wa Mwenyekiti wake Mheshimiwa William
Mganga Ngeleja, Mbunge wa jimbo la Sengerema. Maoni, ushauri na maelekezo yao yameiwezesha
Wizara yangu kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio. Tutaendelea kuzingatia
ushauri wa Kamati hii wakati
tukitekeleza malengo yetu kwa mwaka huu wa fedha na katika siku zijazo kwa
ujumla.
7.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu wake Mheshimiwa Jaji
Augustino Ramadhani kwa kuiongoza vema Tume hiyo. Ninawapongeza pia wajumbe wote kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Rasimu ya Katiba waliyoiwasilisha imetuwekea msingi mzuri wa kujadili uandishi
wa Katiba mpya, jambo ambalo lina mchango wa pekee katika kujenga mustakabali
wa taifa letu. Ni matumaini yangu kwamba tutapata Katiba bora itakayotuongoza
kwa miaka mingi ijayo, itakayoimarisha
umoja wetu na itakayoleta utangamano wa kitaifa na ustawi wa nchi yetu.
B.
MUUNDO NA MAJUKUMU YA WIZARA
8.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya
Katiba na Sheria
inajumuisha Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya
Kurekebisha Sheria, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakala wa
Usajili, Ufilisi, na
Udhamini (RITA), Taasisi ya
Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, na Chuo
cha Uongozi wa Mahakama. Kwa pamoja taasisi
hizi ndizo zinazotekeleza majukumu ya
Wizara kama yalivyoainishwa kwenye Tangazo
la Serikali Namba 20 la mwaka 2010.
9.
Mheshimiwa Spika,
Wizara
ya Katiba na Sheria kwa kuzingatia dira yake ya upatikanaji haki kwa watu wote na kwa wakati, inasimamia
na kutekeleza majukumu yafuatayo: masuala ya kikatiba na kisheria; shughuli za uendeshaji wa mashauri na utoaji
haki; utekelezaji wa haki za binadamu na utawala bora; shughuli za utafiti, urekebu
na uandishi wa sheria; kuishauri na kuiwakilisha Serikali katika masuala ya kisheria
ndani na nje ya nchi; shughuli za usajili, ufilisi na udhamini; kuratibu taasisi za mafunzo zilizo chini yake na
kusimamia maslahi na maendeleo ya watumishi.
C.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI
WA MPANGO
NA BAJETI KWA MWAKA 2013/2014
10.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014
Wizara yangu ilitekeleza malengo
iliyojiwekea ambayo ni yafuatayo: kuratibu
mchakato wa mabadiliko ya Katiba; kusikiliza na
kuendesha mashauri nchini; kusimamia masuala ya haki za binadamu na utawala bora; kutoa huduma za kisheria; kuhakiki na kushiriki
majadiliano ya mikataba mbalimbali; uandishi wa sheria na hati za Serikali; kufanya tafiti na tafsiri ya sheria; kuendesha shughuli za usajili, ufilisi na udhamini; na kuratibu mafunzo ya uanasheria kwa vitendo na uongozi wa Mahakama. Pia, Wizara iliboresha miundombinu ya utoaji haki; ilitoa elimu na habari kuhusu upatikanaji haki kwa jamii; iliratibu shughuli za maboresho ya Sekta ya Sheria na kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma. Utekelezaji wa majukumu hayo umefanyika kwa mafanikio na viwango mbalimbali
vya utekelezaji.
Kuratibu
Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba
11. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na mfumo
imara wa sheria unaozingatia mahitaji ya wakati tulionao, Wizara ya Katiba na
Sheria ilisimamia na kuratibu mchakato wa kihistoria wa kuandika Katiba.
Tofauti na michakato miwili iliyopita (mwaka 1965 na mwaka 1977), safari hii
mchakato wa kuandika Katiba ulihusisha watu wengi zaidi. Wananchi wameshiriki
moja kwa moja kwa kutoa maoni yao
mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba au kwa maandishi. Hali kadhalika
watashiriki kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba inayopendekezwa kupitia kura
ya maoni. Aidha, wananchi walipata fursa ya kupendekeza majina ambayo
Mheshimiwa Rais aliyazingatia katika kufanya uteuzi wa wajumbe wa Tume.
12. Mheshimiwa Spika, Tume hii ilifanya kazi ya kukusanya maoni kutoka
kwa wananchi moja kwa moja na kupitia mabaraza ya Katiba ya wilaya na ya
kitaasisi. Baada ya zoezi hili Tume iliandaa Ripoti iliyojumuisha Rasimu ya
Katiba. Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ,
na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
mnamo tarehe 30 Desemba, 2013.
13. Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea Ripoti ya Tume, Mheshimiwa Rais
aliitisha Bunge Maalum ambalo lilianza kazi rasmi kwa kupokea Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji
Joseph Sinde Warioba tarehe 18 Machi, 2014. Tume ilihitimisha kazi zake na kuvunjwa rasmi kwa
Tangazo la Serikali Namba 81 la tarehe 21 Machi, 2014.
14.
Mheshimiwa Spika,
Bunge Maalum lilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais tarehe 21 Machi 2014. Hadi
sasa Bunge Maalum limefanya kazi ya kuandaa Kanuni za kusimamia uendeshaji wa
shughuli zake za kila siku. Aidha, Bunge Maalum limejadili Sura ya Kwanza na
Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba kama hatua za awali za uchambuzi wa Rasimu
hiyo.
Kuimarisha
Haki za Binadamu na Utawala Bora
15.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha mwaka 2013/2014 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa
elimu kwa umma katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora. Elimu iliyotolewa
ilihusu sheria za ardhi na umiliki wa mali , ambapo wananchi 8,529 kutoka katika
kata 69 na Shehia 7 walifikiwa. Pamoja na kutoa elimu, Tume ilipokea malalamiko
923 ya aina mbalimbali katika kipindi hicho yakiwemo yale yanayohusu migogoro
ya ardhi. Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 324 yalishughulikiwa na kutolewa
uamuzi.
16.
Mheshimiwa Spika, Tume iliandaa
Mwongozo wa Utawala Bora wenye lengo la kukuza uelewa katika eneo hili. Jumla
ya nakala 25,000 za Mwongozo huo zilisambazwa kwa watendaji wa ngazi za vijiji
na kata ili waweze kuzingatia misingi ya utawala bora na haki za binadamu
wakati wanapotekeleza majukumu yao .
17.
Mheshimiwa Spika, hadhi ya Tanzania kuhusu
haki za binadamu imeendelea kuwa nzuri ndani na nje ya nchi yetu. Ni wajibu wa
Wizara yangu kukuza na kuendeleza mafanikio yaliyokwishapatikana. Wizara
imekamilisha Rasimu ya Taarifa ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu
hapa nchini ambayo itawasilishwa kwenye Kamisheni ya Afrika ya Haki za
Binadamu na Watu. Taarifa hiyo inaeleza namna ambavyo Serikali yetu inatekeleza
mikataba mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika kukuza na kulinda
haki hizo.
18.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha 2013/2014, Wizara iliandaa Mpango Kazi wa
Kitaifa wa Haki za Binadamu (2013–2017) uliozinduliwa na Makamu wa Rais
Mheshimiwa, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, tarehe 10 Desemba, 2013. Wizara yangu
ina wajibu wa kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi huu katika taasisi kadhaa za umma na za kijamii.
Kupitia Mpango huu wadau mbalimbali watapata fursa ya kujadili na kutekeleza
masuala ya haki za binadamu. Pia ni fursa kwa Wizara kuimarisha usimamizi na
ufuatiliaji wa masuala mbalimbali yanayohusu haki za binadamu na utawala bora.
19.
Mheshimiwa Spika, uzinduzi huo ulikwenda sambamba na
uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Haki za Watoto (2013-2017).
Mpango huo uliandaliwa kutokana na tafiti mbili zilizofanywa juu ya upatikanaji
haki kwa watoto wanaokutana na mkono wa sheria na hali ya watoto wanaokinzana
na sheria. Matokeo ya tafiti hizo yaliwezesha kubaini vipaumbele vya kimkakati
ndani ya mkakati wenyewe na hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa katika
kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango huo.
20.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaratibu shughuli za Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mauaji ya
Kimbari iliyoundwa chini ya Itifaki ya nchi za Maziwa Makuu ya kuzuia mauaji ya
kimbari. Kamati hii ina jukumu la kujenga uelewa na kuishauri Serikali juu ya
viashiria vinavyoweza kuathiri amani na kusababisha vitendo vya ukatili kwa
binadamu. Katika kipindi cha mwaka 2013/2014, pamoja na kutoa elimu kwa umma
juu ya masuala ya amani kupitia redio na luninga, Wizara imewajengea uwezo
viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali katika kulinda amani katika mikoa ya Arusha,
Mbeya, Mwanza, Mjini Magharibi, Morogoro na Tanga. Katika mikoa hii, viongozi
wa dini waliunda Kamati za amani zenye wajumbe kutoka dini na madhehebu mbalimbali.
Kamati hizi zina jukumu la kuhakikisha amani inadumishwa katika mikoa hiyo.
21.
Mheshimiwa Spika, katika uendeshaji wa shughuli zake, azma ya Serikali ni kuongeza uwazi
katika ngazi zote za utendaji. Ili kufikia lengo hilo Serikali ilijiunga na
Mpango wa Kimataifa wa uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (Open Government
Partnership) mwaka 2011. Tamko la Tanzania katika kutelekeza matakwa ya ubia
huu ni kuweka mazingira ya upatikanaji wa taarifa kuhusu shughuli zinazofanywa
na Serikali. Wizara yangu iliandaa Rasimu ya Waraka wa Baraza la Mawaziri wa
mapendekezo ya kutunga sheria ya haki ya kupata taarifa kutoka katika taasisi za umma kwa lengo la kuongeza
uwazi na uwajibikaji wa Serikali.
22.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali nzuri ya utawala bora
na kuzingatiwa kwa haki za binadamu katika nchi yetu, hivi karibuni kumekuwa na
tuhuma nzito kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu. Tuhuma hizo zilitokana na
utekelezaji wa “Operesheni Tokomeza” ambayo ililenga kuwasaka na kuwafikisha
kwenye vyombo vya Sheria watu wote waliokuwa wanajihusisha na vitendo vya ujangili
katika hifadhi za taifa na mapori tengefu. Kwa kuzingatia uzito wa tuhuma hizo
Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya Uchunguzi chini ya Sheria inayohusu uundwaji wa
Tume za Uchunguzi (Commissions of Inquiry Act, Cap. 32). Kuundwa kwa Tume hiyo kulitangazwa
katika Gazeti la Serikali na. 131 la tarehe 2 Mei, 2014. Tume hiyo yenye makamishna
watatu (3) imepewa hadidu za rejea ambazo ni:
(i)
Kuchunguza namna Operesheni Tokomeza ilivyofanyika;
(ii)
Kuchunguza kama maofisa walioendesha Operesheni hiyo
walifuata sheria, taratibu na hadidu za rejea walizopewa;
(iii)
Kuchunguza endapo maofisa walioendesha Operesheni hiyo walivunja
sheria, taratibu na hadidu za rejea zilizotolewa;
(iv)
Kuchunguza kama kuna watu waliovunja sheria wakati wa
Operesheni hiyo na kuona kama hatua walizochukuliwa wenyewe au mali zao
zilikuwa sahihi;
(v)
Kushauri hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa mtu yeyote aliyevunja
sheria, taratibu na kwenda kinyume na hadidu za rejea zilizokuwepo katika
kutekeleza Operesheni hiyo;
(vi)
Kushauri mambo yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kuandaa
Operesheni nyingine kama hiyo ili mambo yaliyojitokeza katika Operesheni hii
yasijirudie.
Kusikiliza na
kuendesha mashauri nchini
23.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
Dira ya upatikanaji haki kwa watu wote na kwa wakati, Wizara
yangu imeongeza kasi ya kuendesha na kusikiliza mashauri yaliyosajiliwa
Mahakamani. Kasi hiyo imetokana na mikakati
mbalimbali na malengo mahsusi ambayo Mahakama ya Tanzania imejiwekea ya kusikiliza
mashauri kwa ngazi zote za Mahakama. Utaratibu huu unaweka wastani wa idadi ya mashauri yatakayosikilizwa na kila ngazi ya Mahakama
kwa kila mwaka. Katika Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu lengo ni kumaliza mashauri
mapya ndani ya miezi 24, Mahakama ya Hakimu Mkazi katika muda usiozidi miezi 18
na Mahakama ya Mwanzo kumaliza mashauri mapya
ndani ya miezi 12.
24.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu umesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri kwa kiasi kikubwa
ambapo hadi kufikia Desemba, 2012
Mahakama ya Tanzania ilikuwa na jumla ya mashauri 114,278 yaliyohusu masuala ya
madai, jinai na ardhi. Katika mwaka 2013 Mahakama ilisajili mashauri mapya ya
aina hiyo 168,068 na kufanya idadi ya mashauri yaliyokuwepo kufikia 282,346.
Hadi mwezi Desemba 2013 jumla ya mashauri 182,237 yalisikilizwa na kutolewa
uamuzi, sawa na asilimia 65 ya mashauri yote yaliyosajiliwa mahakamani. Mashauri yaliyobaki Mahakamani ni 100,109. (Kiambatisho
“A”).
25.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu umeanza kwa mafanikio ambapo hivi sasa mashauri mengi
yanayosajiliwa Mahakamani yamekuwa yakimalizika katika kipindi kisichozidi
miaka miwili. Wizara yangu itaendelea kubuni njia mbalimbali zitakazosaidia
kuondokana na tatizo la mlundikano wa mashauri na ambalo linaathiri utoaji
haki.
26. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaratibu na kusimamia
utekelezaji wa mpango wa kutenganisha kazi ya upelelezi wa jinai na uendeshaji
wa mashtaka. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni pamoja na kupungua
kwa tuhuma za wananchi za kubambikiziwa kesi katika Mahakama ambazo Mawakili wa
Serikali wanaendesha mashauri ya jinai na kupungua kwa idadi ya wafungwa na
mahabusu magerezani. Kabla ya kuanza kwa mpango huu, mwaka 2007 kulikuwa na
wafungwa 22,622 na mahabusu 20,210. Tangu wakati huo idadi ya wafungwa na
mahabusu imekuwa ikipungua kadri Wizara inavyoendelea kueneza utekelezaji wa
mpango huu katika mikoa na wilaya mbalimbali. Katika mwaka wa fedha wa
2013/2014 idadi ya wafungwa ilipungua kutoka 16,869 mwezi Juni 2013 hadi wafungwa
15,659 mwezi Machi 2014 na idadi ya mahabusu ilipungua kutoka 17,046 mwezi Juni
2013 na kufikia mahabusu 16,647 mwezi Machi 2014.
27.
Mheshimiwa Spika, Kurugenzi ya
Mashtaka pamoja na Mahakama ya
Tanzania zimeanza kutekeleza utaratibu maalum wa kukamilisha usikilizaji wa
mashauri 28 ya dawa za kulevya yaliyosajiliwa Mahakama Kuu. Mashauri haya yamepangwa
kusikilizwa katika kikao maalumu cha Mahakama Kuu kitakachofanyika kuanzia
mwezi Juni 2014. Mashauri 110 yapo Mahakama za wilaya na mikoa kwa hatua za
awali za kuyaandaa ili yahamishiwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa.
Mashauri haya ni yale yenye thamani inayoanzia shilingi milioni kumi na
kuendelea.
28. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na utekelezaji wa mkakati maalumu wa kusikiliza
mashauri 9 ya
jinai ya wizi wa shilingi bilioni 29.8 zilizokuwa katika
akaunti ya madeni ya nje (external payments arrears account - EPA) iliyokuwa
Benki Kuu. Hivi sasa Kurugenzi ya Mashtaka inaendesha jumla ya
mashauri 14
yanayotokana na makosa ya utakatishaji wa fedha kiasi cha shilingi
bilioni 56
zilizopatikana kwa njia ya uhalifu, na mashauri mengine
70
ya kukutwa na nyara za Serikali, zenye thamani ya shilingi
bilioni 45 kinyume cha sheria.
29.
Mheshimiwa Spika, kufikia mwezi Aprili 2014 kulikuwa na jumla ya majalada 404 ya uchunguzi
wa makosa mbalimbali ya rushwa yaliyowasilishwa katika Kurugenzi ya Mashtaka kutoka
TAKUKURU. Kati ya hayo, majalada 202
yaliandaliwa hati za mashtaka, 103 yalirudishwa TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi zaidi, na majalada 98
yanaendelea kufanyiwa uchambuzi.
30.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara ikishirikiana na taasisi mbalimbali
iliongeza jitihada zake za kukabiliana na vitendo viovu wanavyofanyiwa watu wenye
ulemavu wa ngozi. Jitihada hizi zimechangia kiasi kikubwa kupungua kwa idadi ya
matukio ya aina hii katika kipindi cha Julai 2013 hadi Mei 2014, ambapo hakuna
tukio lolote lililoripotiwa Polisi. Hali hii ni tofauti na mwaka wa fedha 2012/2013
ambapo matukio matatu yaliripotiwa Polisi. Hivi sasa Wizara yangu inaendelea na
mashauri 9 ya aina hiyo yanayotokana na matukio ya miaka ya nyuma.
31.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mashauri ya ukiukwaji wa Haki
za Binadamu, Wizara yangu iliendesha
mashauri 6 kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliyopo
Arusha. Mashauri haya yanajumuisha mashauri 4 mapya ambayo bado yanaendelea na mashauri
2 ambayo yametupiliwa mbali na Mahakama hiyo kutokana na waombaji kutotimiza
matakwa ya sheria.
32.
Mheshimiwa Spika, jumla ya mashauri ya madai ambayo Serikali ilishitaki au kushitakiwa, na
yale yanayohusu Katiba yaliyokuwa Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na katika
mabaraza ya usuluhishi (mediation and arbitration) katika kipindi cha Julai 2013 hadi Aprili 2014
ni 750. Kati ya hayo mashauri yaliyosikilizwa
na kutolewa uamuzi ni 89. Serikali ilishinda mashauri 77 yenye thamani ya Shilingi 2,216,502,356,629
na kuokoa kiasi hicho cha fedha. Serikali ilishindwa mashauri 12 yenye thamani ya Shilingi
25,986,416,661.
33.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali za kupambana na vitendo vya uhalifu, bado
kumekuwepo na matukio ambayo baadhi ya watu wamejipatia mali kinyume cha sheria.
Kwa kutambua hilo, Wizara yangu imekuwa ikitenga fedha kwenye mipango yake ya
mwaka kwa ajili ya kujenga uwezo wa Kitengo cha utaifishaji na urejeshaji wa
mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu (Assets
Recovery and Forfeiture Section). Kati ya Julai 2013 na Machi 2014, Mahakama
iliamuru kurejeshwa Serikalini jumla ya
mali na fedha zinazofikia thamani ya zaidi ya shilingi milioni 233 baada ya
watuhumiwa kutiwa hatiani.
Kuimarisha utoaji wa
huduma za kisheria
34.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeboresha mazingira ya upatikanaji haki kwa wananchi ikitambua kuwa
uwakilishi mbele ya vyombo vya sheria ni haki ya msingi. Katika kipindi cha
Julai 2013 hadi Machi 2014 Wizara iliandaa Rasimu ya Waraka wa Kutunga Sheria
ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ili kuwapa fursa wananchi kupata msaada wa
kisheria. Rasimu ya Waraka huo imewasilishwa Serikalini. Sheria hii itakapotungwa
itawawezesha wananchi wengi wasio na uwezo kupata ushauri na kuwakilishwa
katika vyombo vya sheria.
35. Mheshimiwa Spika, wakati
utaratibu wa kutunga sheria hii ukiwa unaendelea, Wizara imeanzisha chombo cha mpito kijulikanacho kama Sekretarieti
ya Msaada wa Kisheria, ili kuratibu utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 jumla ya wananchi 12,809 walipata
huduma ya msaada wa kisheria kupitia Sekretarieti hii.
Kuhakiki
na kushiriki majadiliano ya mikataba mbalimbali
36.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mikataba, Wizara
yangu imetoa ushauri wa kisheria kwa Serikali unaozingatia ubora na weledi, na
pia imeendelea kushiriki katika majadiliano mbalimbali ya mikataba ya kibiashara,
mikutano ya kitaifa, kikanda na
kimataifa kwa manufaa ya nchi. Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014,
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilitekeleza jukumu hili kwa kushiriki
katika mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika, Nchi za Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Ulaya na Umoja wa
Mataifa.
37. Mheshimiwa Spika, ili kulinda maslahi ya nchi katika mikataba kati ya
Serikali na wadau mbalimbali, Serikali imefanya mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi
(Public Procurement Act, 2011). Pamoja na
mambo mengine, Sheria hii inazitaka wizara, taasisi na idara za Serikali kupata
ushauri wa kisheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya
kufunga mkataba wowote wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 50.
Mabadiliko haya yamechangia kuongezeka kwa mikataba inayowasilishwa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuhakikiwa, kutoka mikataba 120 mwaka 2013
hadi mikataba 375 kufikia Machi 2014. Hali hii imeiepusha Serikali na mikataba
isiyo na maslahi kwa taifa.
Uandishi
wa sheria na hati za Serikali
38.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliandaa jumla ya miswada 11 iliyojadiliwa
na kupitishwa na Bunge lako tukufu kuwa sheria. Miswada hiyo ilihusu: Sheria ya Fedha na Sheria ya Matumizi ya Fedha inayopitishwa
wakati wa Bunge la Bajeti; Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji; Sheria ya Vyama vya
Ushirika; Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya
Maoni. Miswada mingine ni Sheria ya Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini, Sheria
ya Takwimu, Sheria ya Marekebisho ya Ushuru na Bidhaa na Sheria ya Marekebisho
ya Sheria Mbalimbali (Na. 1) na (Na. 2). Aidha, Sheria
Ndogo 136 zilitayarishwa na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali tayari kuanza
kutumika.
Kufanya utafiti na
tafsiri ya sheria
39.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Tume ya Kurekebisha Sheria ilifanya mapitio na utafiti wa mifumo ya sheria
mbalimbali. Utafiti wa kwanza ulihusu mfumo wa sheria wa utatuzi wa migogoro ya
ardhi. Utafiti huu umekamilika na Ripoti yake imekabidhiwa kwa Waziri wa Katiba
na Sheria. Ni azma ya Wizara yangu kuipitia Ripoti hii kwa kushirikiana na
Wizara nyingine zinazoshughulika na utatuzi wa migogoro ya ardhi. Utafiti wa
pili ulihusu mfumo wa sheria inayosimamia huduma ya hifadhi ya jamii kwa wazee.
Mwisho, Tume ilifanya utafiti kuhusu sheria zinazolinda watumiaji wa bidhaa na
huduma ili kubaini upungufu uliopo.
40.
Mheshimiwa Spika, ufanisi katika
utekelezaji wa sheria unategemea sana uelewa wa wananchi kuhusu sheria hizo.
Kwa kutambua hilo
Wizara imetafsiri Sheria 7 kutoka Kiingereza kwenda lugha
ya Kiswahili.
Wizara
itaendelea kutafsiri Sheria nyingi zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya jamii na
uwezo uliopo. Wizara inapenda kutoa mwito kwa
wadau mbalimbali ndani na nje ya Serikali kuchangia katika kuhamasisha wananchi
kuwa na mwamko wa kupenda kusoma na kuzifahamu sheria za
nchi. (Kiambatisho
“B”).
41.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wizara yangu kwa
kushirikiana na nchi wanachama imeendelea kufanya mapitio ya Sheria
zinazosimamia haki za ubunifu na haki miliki (Intellectual property laws). Lengo ni kuhakikisha kuwa sheria za
nchi wanachama zinawiana na sheria za Jumuiya hiyo kama ambavyo nchi hizo zimekubaliana katika kutekeleza
Itifaki ya Soko la Pamoja.
Kuimarisha shughuli za
Usajili, Ufilisi na Udhamini
42.
Mheshimiwa Spika, usajili wa matukio muhimu ya binadamu (vizazi, vifo, ndoa, talaka na watoto
wa kuasili) unalenga kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na za uraia. Aidha, usajili
huu unaiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya mipango mbalimbali ya
maendeleo. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2013 hadi Machi 2014 Wizara imeboresha
mfumo wa usajili wa vizazi kwa kusogeza huduma hii hadi ngazi za chini kama vile kata na vituo
vya tiba. Maboresho haya yamefanyika kupitia Mpango wa usajili wa vizazi kwa watoto
wenye umri wa chini ya miaka mitano uliozinduliwa rasmi mkoani Mbeya mwezi
Julai 2013.
43.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango huu
umeongeza idadi ya watoto wa umri chini ya miaka mitano waliopatiwa vyeti vya
kuzaliwa kutoka watoto 37,090 kabla ya mpango huu kuanza, hadi 169,477 Machi
2014. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 31.4 la watoto wote wa umri wa chini
ya miaka mitano mkoani humo. Mbali na usajili huu mkoani Mbeya, Wizara imefanya
usajili wa kawaida katika sehemu nyingine za Tanzania bara wa jumla ya vizazi
493,887, ndoa 14,031, talaka 53, vifo 34,460, na watoto wa kuasili 30. Hali
kadhalika jumla ya hati 182 za wadhamini wa vyama
vya siasa, makanisa, misikiti na mali za vikundi vya kijamii zilisajiliwa. (Kiambatisho
“C”)
Kuimarisha Taasisi za
Mafunzo ya Sheria
44.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2013/2014 Wizara imeimarisha taasisi ya mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo
na Chuo cha Uongozi wa Mahakama. Hadi kufikia Machi 2014, jumla ya wanafunzi
293 walihitimu mafunzo ya uanasheria kwa vitendo na kustahili kusajiliwa kuwa mawakili,
ikilinganishwa na mwaka 2012/2013 ambapo wahitimu walikuwa 272. Jumla ya
wanafunzi 896 walihitimu mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama, kati ya
hao wahitimu 267 walitunukiwa Stashahada ya Sheria na 629 Cheti cha Sheria.
Vile vile, Wizara imeanzisha Tawi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama katika jiji
la Mwanza na kudahili wanafunzi 95 kwa mara ya kwanza mwaka 2013/2014. Jitihada
hizi zitaongeza idadi ya watalaam wenye sifa za kuajiriwa katika fani
mbalimbali za sheria.
Kuboresha miundombinu
ya utoaji haki
45.
Mheshimiwa Spika, ubora wa huduma unaotolewa na taasisi za sheria unategemea ubora wa
mazingira na miundombinu ya utoaji haki. Kwa kuzingatia umuhimu huo, katika
kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014, Wizara imefanya yafuatayo:-
·
Imekarabati masijala
kwenye Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Kanda za Dar es Salaam na Mtwara;
·
Imepata washauri elekezi
kwa ajili ya kukarabati Mahakama za
Mwanzo 10, na kujenga Mahakama za Mwanzo 25. Utaratibu wa kupata wakandarasi umetangazwa kwenye magazeti ya tarehe 11 na 12
Mei 2014;
·
Imejenga uzio wa Mahakama
Kuu Kanda ya Bukoba; kutenga vyumba vya ofisi za majaji na makatibu muhtasi; na
kuziba sehemu ya wazi ya paa;
·
Imeboresha masijala 71 za
Mahakama za Mwanzo kwa kuziwekea mfumo wa kielektroniki wa kutunza kumbukumbu
za majalada;
·
Imekamilisha ukarabati wa
Mahakama za Mwanzo za Mgandu na Mwamagembe katika mkoa wa Singida;
·
Inakamilisha ujenzi wa
bweni la wanafunzi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama;
·
Imefungua ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mkoa
wa Geita; na inakamilisha taratibu za kuanza ukarabati wa Ofisi katika
mikoa ya Simiyu na Katavi;
·
Imekamilisha ujenzi wa
jengo la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini;
·
Imekamilisha upembuzi
yakinifu wa mradi wa mfumo mpana wa
mawasiliano (Wide Area Network) utakaounganisha Makao Makuu ya Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kurugenzi ya Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali mkoa ya Dar es Salaam.
46.
Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu kuhusu mradi wa e-justice
utakaorahisisha uendeshaji wa mashauri ya jinai umekamilika. Mradi huu utaunganisha Mahakama, Magereza na
Ofisi za mikoa za Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa njia ya mtandao. Ripoti ya
zoezi hili imewasilishwa Ofisi ya Rais -Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha kwa
hatua za maamuzi.
47. Mheshimiwa Spika, Wizara imetumia fursa za
maendeleo zinazotokana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika
kuboresha huduma zinazotolewa. Mahakama ya Tanzania imejiimarisha katika matumizi
ya TEHAMA kwa kuanzisha mfumo endelevu wa upatikanaji wa takwimu mbalimbali za
Mahakama. Mfumo huo umeanza kufanya kazi katika Mahakama ya Rufani, Mahakama
Kuu katika Divisheni za Biashara, Kazi na Ardhi, na Mahakama Kuu Kanda ya Dar
es Salaam. Itakapofika Desemba 2014 Mahakama Kuu zote nchini, mahakama za mikoa
na mahakama zote za wilaya zitatumia TEHAMA katika ukusanyaji na utunzaji wa takwimu.
48. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini umeanzisha utaratibu wa kupokea taarifa za usajili wa
vizazi kupitia simu za mkononi mara tu mtoto anaposajiliwa kwenye kata au kituo
cha tiba. Hivi sasa utaratibu huu unafanyika mkoani Mbeya kupitia mpango wa
kusajili watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano (U5BRI). Sambamba na hilo mwananchi yeyote nchini anaweza
akapata taarifa za huduma za RITA kupitia simu za mkononi kwa kutuma neno RITA
kwenda namba 15584 na Tovuti ya Wakala (www.rita.go.tz).
Elimu kwa Umma
49. Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua kuwa wananchi wana nafasi muhimu
katika kuimarisha utawala wa sheria, misingi ya haki za binadamu na utawala
bora. Kwa kuzingatia hilo ,
Wizara imetoa elimu kwa umma kwa njia mbalimbali zikiwemo redio na luninga.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara ilirusha vipindi 35 vya
redio na vipindi 9 vya luninga vilivyotoa elimu kuhusu mapambano na rushwa;
haki za watoto na misingi ya haki za binadamu na utawala bora. Vile vile,
Wizara iliandaa mikutano ya wadau katika mikoa ya Rukwa na Tanga kwa lengo la
kuwajengea uelewa wa sheria. Pia Wizara ilishiriki maonesho ambapo jumla ya
vitabu 25,000 na vipeperushi 2,800 kuhusu haki za binadamu na misingi ya
utawala bora vilisambazwa. Katika mikutano hiyo, vitabu 500 na vipeperushi 1000
kuhusu historia ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na majukumu ya Wizara
vilisambazwa.
Uratibu na Utekelezaji wa Maboresho ya Sekta ya Sheria
50.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imetekeleza na kuratibu programu na miradi mbalimbali ya
kuboresha Sekta ya Sheria. Utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya
Sheria unalenga kuimarisha mifumo ya utoaji haki na kukuza uwezo wa taasisi za sheria
katika kutoa huduma bora. Hadi sasa Programu hii imewezesha, pamoja na mambo
mengine, kutenganishwa kwa shughuli za upelelezi na mashtaka, kufanya mapitio ya
sheria mbalimbali na kuanzishwa kwa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa
Vitendo.
51.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2013 hadi
Machi 2014, shughuli nyingine muhimu za kuboresha sekta ya sheria
zilizotekelezwa ni pamoja na:- kufanya tathmini ya hali ilivyo sasa na
kuishauri Serikali namna ya kuendeleza maboresho katika sekta ya sheria; kuimarisha
utendaji wa Sekretarieti ya Huduma ya Msaada wa Kisheria; kuratibu uanzishwaji
wa maeneo ya kuhifadhi watoto waliokinzana na sheria ili kulinda haki zao, na kuimarisha
madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya Polisi na Magereza.
52.
Mheshimiwa Spika, maboresho ya sekta ya sheria ni pamoja na mapambano na rushwa. Wizara yangu
ni moja ya taasisi zinazotekeleza mradi wa Uimarishaji wa Mapambano na Rushwa
Tanzania (Strengthening Tanzania
Anti-Corruption Action - STACA) unaolenga kuziba mianya ya rushwa katika
taasisi zake. Mradi huu ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2011/2012 na
unatarajia kukamilika mwaka 2014/2015. Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014
jumla ya pikipiki 214 zilinunuliwa kwa ajili ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo
kwa nia ya kuondoa kero ya usafiri na kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri.
Pia jumla ya masijala 68 za Mahakama za Mwanzo ziliboreshwa kwa kuwekewa mfumo
wa kielektroniki wa kutunza kumbukumbu za majalada. Mfumo huo umerahisisha
upatikanaji wa taarifa za kimahakama na hivyo kuondoa mianya ya rushwa.
53.
Mheshimiwa Spika, kupitia mradi huu kitengo cha utaifishaji na urejeshaji wa mali
zilizopatikana kwa njia ya uhalifu (Assets Recovery and Forfeiture Section)
kimeimarishwa kwa kupatiwa vitendea kazi ambavyo vimesambazwa katika ofisi za
Mikoa na Wilaya za Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Vifaa hivyo ni kompyuta 35, mashine
za uchapishaji, vitabu vya rejea na samani za ofisi. Hali kadhalika mawakili 64 wa Serikali wamepatiwa mafunzo kuhusu stadi za kuendesha
mashauri ya rushwa na namna ya kushughulikia mali zinazopatikana kwa njia ya
rushwa. Kwa kuwa Kurugenzi ya Mashtaka ni kiungo muhimu katika uendeshaji wa
kesi na upelelezi, Kurugenzi iliandaa mikutano ya kikazi na kiutendaji na wadau
mbalimbali chini ya Jukwaa la Haki Jinai. Vikao hivyo vilikuwa kati ya Mawakili
wa Serikali Wafawidhi, Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa na Vikosi Tanzania Bara,
TAKUKURU, Mkemia Mkuu wa Serikali, Idara ya Uhamiaji, Idara ya Wanyamapori na
Tume ya Uratibu wa Dawa za Kulevya. Lengo la mikutano hiyo lilikuwa ni
kuboresha uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka. Ubia huu unasaidia
kukusanya nguvu pamoja ili kuleta
ufanisi zaidi katika utendaji.
54.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yangu ilichukua hatua za
kuziimarisha Kamati za Maadili za Mahakama za mikoa na wilaya. Tume ya Utumishi
wa Mahakama ilifanya ukaguzi wa Kamati za Maadili za Mahakama kwenye ngazi ya mkoa
na wilaya katika mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma. Katika ukaguzi huo, Tume ya
Utumishi wa Mahakama ilibaini changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu
wa fedha. Wizara imeanza kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuzipatia fedha
Kamati za Maadili za Mahakama ngazi za mikoa na wilaya. Katika mwaka wa 2013/14
jumla ya shilingi 36,000,000 zilitolewa kwa mikoa 18 na shilingi 136,500,000
kwa wilaya 91.
Kwa upande wa mawakili,
Kamati ya Maadili ya Mawakili wa Kujitegemea (Advocates’ Committee) ilishughulikia
malalamiko 18 katika kipindi cha Julai 2013 hadi Aprili 2014. Kati ya hayo,
malalamiko 6 yamekwishatolewa uamuzi.
55.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imewajengea uwezo watumishi waliopo na kuajiri watumishi
wapya ili kuleta tija na ufanisi katika kutekeleza majukumu yake. Katika
kipindi cha Julai 2013 hadi Machi, 2014 Wizara iliajiri watumishi wapya 541; ilipandisha
vyeo watumishi 487; na kuwezesha watumishi 1,081 wa kada mbalimbali kupata mafunzo ya muda
mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi.
Utekelezaji
wa masuala
mtambuka
56.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Katiba na Sheria inazingatia masuala mtambuka katika utekelezaji
wa majukumu yake. Haya ni kama vile kuingiza masuala ya jinsia katika sera,
mipango na uendeshaji; kuzingatia mahitaji ya watu wanaoishi na virusi vya
UKIMWI; na masuala yanayohusu maadili. Kwa upande wa kuzingatia jinsia katika ajira
jumla ya watumishi 541 waliajiriwa. Kati yao wanawake ni 241 (44.5%) na wanaume
ni 300 (55.5%). Vile vile, jumla ya watumishi 487 walipandishwa vyeo ambapo
wanawake walikuwa 217 (44.56%) na wanaume walikuwa 270 (55.44%). Aidha, jumla ya watumishi waliopata mafunzo
ni 1,081 kati yao wanawake ni 588 (54%)
na wanaume 493(46%) (Kiambatisho ”G”). Aidha,
Wizara imeendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwawezesha watumishi wake wa
kike na wa kiume kuweka uwiano muafaka wa kutekeleza kazi zao na vilevile kumudu
majukumu ya uzazi na ulezi.
57.
Mheshimiwa Spika, kuhusu masuala ya UKIMWI, watumishi wa Wizara walipata mafunzo ya jinsi ya
kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kupitia Kamati za UKIMWI zilizopo
katika Wizara na taasisi zake. Wizara inawahudumia watumishi wanaoishi na virusi
vya UKIMWI kwa matibabu na lishe.
58.
Mheshimiwa Spika, kuhusu masuala ya maadili, mafunzo yametolewa kwa watumishi 100 wa kada
mbalimbali kutoka Kurugenzi ya Mashtaka kwa nia ya kutoa uelewa wa masuala ya
rushwa, kujenga maadili na uhusiano wenye
staha kazini.
MAPATO NA MATUMIZI YA
FEDHA KWA MWAKA 2013/14
Ukusanyaji wa Maduhuli
ya Serikali
59.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yangu ilipanga kukusanya jumla ya
Shilingi 5,250,454,700 kama maduhuli ya Serikali kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.
Hadi kufikia mwezi Machi 2014 Wizara ilikusanya jumla ya Shilingi
6,007,714,285, sawa na asilimia 114 ya
lengo. Tofauti hii inatokana na ongezeko la makusanyo ya ada za wanafunzi wa
Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na maduhuli ya Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (RITA).
Mapato na Matumizi ya Fedha 2013/2014
60.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 260,656,733,000
kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo Shilingi
205,397,547,000 ni matumizi ya kawaida na Shilingi 55,259,186,000 ni fedha za miradi
ya maendeleo. Kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Shilingi 42,537,099,000 ni kwa
ajili ya mishahara na Shilingi 162,860,448,000 ni kwa ajili ya matumizi
mengineyo. Kati ya fedha za matumizi ya maendeleo Shilingi 44,000,000,000 ni
fedha za ndani na Shilingi 11,259,186,000 ni fedha za nje.
61.
Mheshimiwa Spika, kufikia Machi 2014, Wizara imepokea kiasi cha Shilingi 120,363,046,912
sawa na asilimia 46 ya fedha zilizoidhinishwa. Kati ya fedha hizo Shilingi 110,763,667,097
ni fedha za matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 54. Kati ya fedha hizi za
matumizi ya kawaida, shilingi 36,312,510,030 ni mishahara ya watumishi; na Shilingi
74,451,157,067 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo. Fedha za maendeleo
zilizopokelewa ni Shilingi 9,599,379,815, sawa na asilimia 17 ya fedha zote za
Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 5,157,500,000 ni fedha za ndani na
Shilingi 4,441,879,815 ni fedha za nje. Ufafanuzi wa taarifa hizi unapatikana
katika (Kiambatisho ”D”).
D.
CHANGAMOTO ZILIZOPO
62.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio ambayo Wizara yangu imeyapata, zipo changamoto mbalimbali
zilizojitokeza wakati wa kutekeleza majukumu yake. Changamoto hizi ni pamoja na:
·
Bajeti ndogo inayotengwa ikilinganishwa
na mahitaji halisi ya Wizara na taasisi zake;
·
Mapokezi ya fedha kidogo
zilizoidhinishwa hayatabiriki na hivyo kuifanya Wizara na taasisi zake
kushindwa kutekeleza Mipango Kazi yao kwa namna endelevu;
·
Wizara kutotengewa fedha
za maendeleo za ndani kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makaazi. Hali hii
inazilazimu baadhi ya taasisi za Wizara kutumia pesa nyingi kwa ajili ya
kulipia kodi ya pango, na hivyo kuathiri
utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki na mazingira ya kazi;
·
Wanafunzi wa Taasisi ya
Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo kutopatiwa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu
ya Juu kunachangia kuwepo kwa malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wanafunzi
na kuathiri utulivu masomoni;
·
Uhaba wa vitendea kazi na
rasilimali watu;
·
Ongezeko la matukio ya
makosa ya jinai pamoja na mbinu mpya za kutenda uhalifu;
·
Kuwepo kwa mazingira
yanayoweza kuhatarisha usalama wa majaji, mahakimu na mawakili wa Serikali na
hivyo kuathiri utendaji kazi wao; na
·
Kuongezeka kwa mmonyoko
wa maadili miongoni mwa baadhi ya
watendaji wanaoshughulika na utoaji haki katika sekta ya sheria.
E.
MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2014/2015
63.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara yangu imepanga kuimarisha
utekelezaji wa malengo mkakati iliyojiwekea ili kutoa haki kwa watu wote na kwa
wakati. Ili kufikia azma hiyo, Wizara itasimamia na kufuatilia utekelezaji wa
majukumu yake katika maeneo ya kipaumbele yafuatayo:
i.
Utekelezaji wa Katiba ya nchi na Sheria
a)
Kufuatilia mchakato wa
kutunga Katiba;
b)
Kufanya maandalizi ya mapitio na marekebisho ya
sheria zitakazoguswa na mabadiliko ya Katiba;
c)
Kutoa elimu ya Katiba kwa
wananchi kuhusu taratibu za kimahakama zinazopaswa kuzingatiwa katika kudai
haki;
d)
Kushughulikia maswala ya
urekebu wa Sheria;
e)
Kushughulikia uandishi wa
Miswada ya Sheria, Sera na Hati za Serikali;
f)
Kuhakiki rasimu za mikataba ya Serikali na kushiriki
katika majadiliano yanayohusu mikataba hiyo.
ii.
Kusimamia na kufuatilia utoaji haki
a)
Kusimamia shughuli za
uendeshaji na usikilizaji wa mashauri;
b)
Kuziimarisha Kamati za
Maadili za Mahakama katika ngazi ya mikoa
na wilaya kwa kuzipa mafunzo na kuzifanyia ukaguzi. Kazi hii itaanzia
katika mikoa ya Dodoma, Katavi, Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Singida,
Tabora;
c)
Kuimarisha utekelezaji wa
mpango wa kutenganisha shughuli za upelelezi na mashtaka.
iii.
Kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na utawala wa sheria
a)
Kuhakikisha haki za
binadamu zinalindwa na kuendelezwa;
b)
Kuwasilisha Bungeni miswada
mbalimbali inayohusu upatikanaji wa msaada wa kisheria; kulinda mashahidi na
waathirika wa vitendo vya jinai (witness and victims of crime protection law);
kulinda watu wanaotoa taarifa kwa siri (whistle blowers) kuhusu vitendo vya
uhalifu au vya ukiukwaji wa maadili; marekebisho ya sheria ya usajili wa vizazi
na vifo; sheria ya ufilisi;
c)
Kueneza mfumo wa usajili
wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano katika mikoa ya Simiyu na
Shinyanga;
d)
Kuimarisha usimamizi na
uendeshaji wa taasisi za mafunzo za Wizara.
iv.
Kuimarisha miundombinu ya utoaji haki
a)
Kujenga nyumba za majaji, majengo ya Mahakama na majengo ya Ofisi;
b)
Kuimarisha huduma za
masjala;
c)
Kufunga mfumo wa
kielektroniki wa e-justice kwa ajili
ya usikilizaji wa mashauri;
d)
Kuimarisha usimamizi na
uendeshaji wa Taasisi za mafunzo za Wizara.
v.
Kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
a)
Kupunguza mlundikano wa
mashauri katika Mahakama zote;
b)
Kuharakisha ufunguaji na
uendeshaji wa mashauri;
c)
Kufanya mapitio na
utafiti wa sheria zinazohusu uwekezaji
na biashara;
d)
Kuhakiki mikataba mapema
na kwa weledi.
vi.
Utekelezaji wa Masuala Mtambuka
a)
Kuimarisha Kamati za
Amani za Mikoa kupitia Kamati ya Kitaifa ya kuzuia mauaji ya kimbari katika
mikoa na wilaya. Vilevile, kutoa elimu na hamasa kwa Wabunge, Wanahabari na
wanafunzi wa vyuo vikuu ili kujenga utamaduni wa amani na utangamano kwa kila Mtanzania;
b)
Kuandaa na kuratibu awamu ya pili ya shughuli za maboresho ya Sekta ya Sheria;
c)
Kuimarisha usimamizi wa
maadili na uwajibikaji wa watumishi kazini.
64.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na changamoto zilizopo, Wizara yangu imejizatiti kufanikisha
malengo iliyojiwekea katika kutekeleza mpango na bajeti kwa kipindi cha mwaka
2014/2015.
F.
SHUKRANI
65.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wadau wetu wa maendeleo kwa
kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha Sekta yetu ya Sheria. Kwa
namna ya pekee napenda kushukuru nchi za Canada, Denmark, Sweden, Uswisi na
Uingereza kupitia Mashirika yao ya
Maendeleo ya CIDA, DANIDA, SIDA na DFID.
Vilevile, nayashukuru Mashirika na Taasisisi za Kimataifa zifuatazo: Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia
Watoto (UNICEF), Shirika la Umoja wa
Mataifa la Maendeleo (UNDP) na Benki
ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) katika kuchangia maendeleo ya Sekta ya
Sheria.
66.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za pekee kwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Sheria
kwa ushirikiano na ushauri wao uliowezesha kutekelezwa kwa majukumu ya Wizara
kwa mwaka 2013/2014 kama yalivyobainishwa katika hotuba hii. Ninapenda
kumshukuru Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki (Mb), Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu, Mheshimiwa Jaji Frederick
Mwita Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Fakih A.R Jundu, Jaji
Kiongozi, Ndugu Fanuel E. Mbonde, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu
Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, na Ndugu George Masaju,
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
67.
Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru Mheshimiwa Ignas Paul Kitusi, Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Dkt. Eliezer M. Feleshi, Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Winifrida
Korosso, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Bibi. Mary Massay,
Katibu Mtendaji Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mheshimiwa Jaji Dkt.
Gerald Ndika, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, Mheshimiwa
Jaji Ferdinand Wambali, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Ndugu Phillip
Saliboko, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa RITA, Bibi Enzel William Mtei, Katibu
Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakurugenzi wa Idara na Taasisi
zilizo chini ya Wizara yangu na Watumishi wote kwa ushirikiano na kazi kubwa
waliyoifanya katika kuandaa Mpango na Bajeti hii. Mwisho nitoe shukurani kwa
Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kufanikisha uchapishaji wa hotuba hii.
G.
MAJUMUISHO
68.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Sheria ina umuhimu wa
pekee katika kuchangia maendeleo ya nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii. Wizara
yangu ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa inakuza na kuimarisha amani,
utawala wa sheria na haki za raia. Kwa kuzingatia dhana hii, napenda
kutoa mwito kwa wananchi wote pamoja na Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kuwa
dhamira ya Serikali ya kulinda amani, utulivu na haki za binadamu inazingatiwa
na kupewa kipaumbele kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
H.
MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2014/2015
69.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yaliyopangwa katika mwaka wa fedha
2014/2015, Wizara yangu inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 231,372,948,000 kwa ajili ya Taasisi, Idara na
vitengo vyake. Kati ya fedha hizo, Shilingi 134,006,144,000 ni kwa ajili ya
Matumizi Mengineyo na Shilingi 48,804,234,000 ni Mishahara. Fedha za
Maendeleo ni Shilingi 48,562,570,000, kati ya hizo Shilingi 44,000,000,000
ni fedha za ndani na Shilingi 4,562,570,000 ni fedha za nje.
Fedha za Matumizi
70.
Mheshimiwa Spika, mchanganuo wa matumizi ya bajeti kwa Mafungu saba ya Wizara ni kama
ifuatavyo:-
Fungu 12: Tume ya Utumishi wa Mahakama
Matumizi ya Mishahara Sh. 208,764,000
Matumizi Mengineyo Sh. 2,871,716,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) - Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo (nje) Sh. 0.0
Jumla
Sh. 3,080,480,000
Fungu 16: Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Matumizi ya Mishahara Sh. 2,426,898,000
Matumizi Mengineyo Sh. 8,332,865,000
Matumizi ya Maendeleo
(Ndani) Sh.
0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje) Sh. 457,149,000
Jumla Sh. 11,216,912,000
Fungu 35: Kurugenzi ya Mashtaka
Matumizi ya Mishahara- Sh. 5,215,201,000
Matumizi
Mengineyo Sh. 16,460,826,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje) Sh. 468,299,000 Jumla Sh. 22,144,326,000
Fungu 40: Mfuko wa Mahakama
Matumizi ya Mishahara Sh. 35,040,061,000
Matumizi Mengineyo Sh. 89,660,284,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) Sh.
40,000,000,000
Matumizi ya Maendeleo
(nje) Sh. 1,687,748,000
Jumla Sh. 166,388,093,000
Fungu 41: Wizara ya Katiba na Sheria
Matumizi ya Mishahara Sh. 3,154,642,000
Matumizi Mengineyo Sh.
8,028,651,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) - Sh. 4,000,000,000
Matumizi ya Maendeleo
(nje) - Sh. 1,048,621,000
Jumla
- Sh. 16,231,914,000
Fungu 55:Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Matumizi ya Mishahara Sh. 2,041,593,000
Matumizi Mengineyo Sh. 4,795,802,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) - Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje) - Sh. 900,753,000
Jumla - Sh.
7,738,148,000
Fungu 59: Tume ya Kurekebisha Sheria
Matumizi ya Mishahara Sh. 717,075,000
Matumizi Mengineyo Sh. 3,856,000,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) - Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje) - Sh.
0.0
Jumla - Sh. 4,573,075,000
Makusanyo ya Maduhuli ya Serikali
71. Mheshimwa Spika, kwa mwaka 2014/2015 Wizara yangu inatarajia kukusanya
kiasi cha Shilingi 8,577,362,121 kama maduhuli ya Serikali, kama
ifuatavyo:-
Fungu 12: Tume ya
Utumishi wa Mahakama
|
Sh.
|
0.0
|
|||
Fungu 16: Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali
|
Sh.
|
4,502,000
|
|||
Fungu35: Kurugenzi ya Mashitaka
|
Sh.
|
17,103,000
|
|||
Fungu 40: Mfuko wa Mahakama
|
Sh.
|
4,115,843,000
|
|||
Fungu 41: Wizara ya Katiba na Sheria
|
Sh.
|
4,434,270,121
|
|||
Fungu 55: Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora
|
Sh.
|
5,644,000
|
|||
Fungu 59: Tume ya Kurekebisha Sheria
|
Sh.
|
0.0
|
|||
JUMLA
|
Sh.
|
8,577,362,121
|
|||
72.
Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment