Na Mwandishi wetu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif
Ali Iddi, amesema mkanganyiko uliojitokeza kuhusu fedha za majimbo hauhusiani
na ofisi yake, kwani bado fedha hizo hazijaingizwa kwenye akaunti ya ofisi ya
Makamu wa Pili.
Kauli ya Balozi Seif inakuja baada ya baadhi ya
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka Zanzibar, kusema kwamba ofisi
hiyo imezuia fedha hizo kwa sababu zisizoeleweka huku taarifa hizo zikisambazwa
kwenye mitandao ya kijamii.
Alisema ni kweli kumekuwa na malalamiko ya aina
hiyo yaliotolewa na baadhi ya Wabunge, lakini suala hilo haliihusu ofisi yake
kwa vile fedha hizo baada ya kutolewa, haziingii moja kwa moja ofisini kwake.
Alisema ili fedha hizo ziweze kutolewa lazima
kwanza zipite Wizara ya Fedha Tanzania, Ofisi ya Makamu wa Rais na baadae Wizara ya
Fedha Zanzibar
kabla ya kupelekwa ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Alisema baada ya fedha hizo kufikishwa ofisini
kwake, hupelekwa halmashauri za mikoa ambazo ndio wenye mamlaka ya kugawa fedha
hizo majimboni.
Alisema madai kwamba ofisi yake imkalia fedha hizo
hayana ukweli kwa sababu bado hazijatoka Wizara ya Fedha Zanzibar .
Alisema ni kweli fedha hizo zimeshafika Zanzibar,
lakini kilichotokea ni kutokamilika kwa taratibu za fedha, baada ya kutokea
matatizo.
Wabunge hao walidai wanapatwa na wasiwasi wa fedha
hizo na kwamba huenda zimeliwa na ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Bunge hutoa shilingi milioni 25 kila mwaka kama fedha za maendeleo ya jimbo huku Baraza la
Wawakilishi likitoa shilingi milioni 15 kwa kila Mwakilishi.
No comments:
Post a Comment