Habari za Punde

Uturuki kuendelea kukuza uhusiano wa kiuchumi na kiutamaduni na Zanzibar

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Wizara ya mambo ya nje wa Uturuki, pamoja na baadhi ya viongozi wa SMZ waliofuatana nao
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiagana na Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mhe. Ahmet Davutoglu, baada ya kumaliza mazungumzo yao ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Wizara ya mambo ya nje wa Uturuki, pamoja na baadhi ya viongozi wa SMZ waliofuatana nao
 
Picha na Salmin Said OMKR
 
Na Hassan Hamad OMKR
 
Uturuki imesema itaendelea kukuza uhusiano wa kiuchumi na utamaduni kati yake na Zanzibar, ili kuimarisha uhusiano huo uliodumu kwa kipindi kirefu sasa.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mhe. Ahmet Davutoglu ameeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ofisini kwake Migombani.
Amesema Uturuki na Zanzibar zimekuwa zikijivunia uhusiano wa muda mrefu katika Nyanja mbali mbali zikiwemo za kiuchumi na utamaduni, na kutaka uhusiano huo uendelezwe kwa maslahi ya pande zote mbili.
Mhe. Ahmet amesema Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuonesha ustaarabu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na kwamba Uturuki itaendelea kushirikiana nayo kuona kuwa ustaarabu na utamaduni wa Zanzibar unaendelezwa.

Aidha amefahamisha kuwa Uturuki ikiwa nchi ya saba duniani kwa maendeleo ya kilimo na utalii, inayo nafasi kubwa ya kutoa mchango wake kwa Zanzibar katika maeneo hayo, kwa lengo la kuchangia maendeleo ya Zanzibar.
Ameeleza kuwa katika kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya Uturuki na Tanzania unaimarishwa, Uturuki inakusudia kufungua kituo maalum jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).
Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amewakaribisha wawekezaji wa Uturuki kuja kuwekeza Zanzibar hasa katika sekta za utalii na viwanda vidogo vidogo.
Amesema Zanzibar ikiwa nchi ya visiwa haina nafasi ya kuwekeza viwanda vikubwa, lakini ina fursa nzuri kwa viwanda vidogo vidogo vikiwemo vya usindikaji wa matunda, ikizingatiwa kuwepo kwa matunda mengi kila ifikapo msimu wa matunda hayo.
Maalim Seif ametaja maeneo mengine ya uwekezaji ni pamoja na uwekezaji wa hoteli za hadhi ya juu pamoja na vituo maalum vinavyoweza kuhudumia mikutano wa kimataifa.
Amesema katika kuhakikisha kuwa mambo hayo yanafanikiwa, serikali imekuwa ikiweka mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundo mbinu ya barabara, viwanja vya ndege na umeme.
Kuhusu elimu Maalim Seif amesema Zanzibar bado inakabiliwa na uhaba wa wataalamu hasa katika taaluma za sayansi, na kuiomba nchi hiyo kutenga nafasi maalum za masomo kwa ajili ya Zanzibar, wakati inapotoa nafasi hizo kwa Tanzania.
Amesema hatua hiyo itasaidia kutoa fursa kwa vijana wa Zanzibar kupata nafasi za masomo nchini Uturuki na kupunguza tatizo la upungufu wa wataalamu wa fani za Sayansi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.