Habari za Punde

AG:Muungano ni halali licha ya hati kutoridhiwa BLM

Na Husna Mohammed
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema licha ya kwamba hati ya Muungano haikuridhiwa na Baraza la Mapinduzi, lakini muungano huo ni halali.

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman,aliliambia baraza la wawakilishi jana wakati akijibu hoja za wajumbe wa baraza hilo waliochangia hotuba ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Alisema kutoridhiwa kwa hati hiyo ya muungano hakubatilishi muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni halali na kwa kuwa hati hiyo haikuridhiwa basi bado haijabatilisha muungano kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Akizungumzia kuhusu umiliki wa kisiwa cha Fungu Mbaraka, Mwanasheria huyo alisema kisiwa hicho ni milki ya Zanzibar.

Alisema kisiwa hicho kinamilikiwa na Zanzibar na hadi sasa hakuna  mtu au taasisi yoyote iliyodai kumiliki kisiwa hicho.

"Tumeangalia katika utaratibu wa sheria hakuna madai ya umiliki wa kisiwa hicho kwa mtu au taasisi yoyote nataka kuithibitishia serikali na watu wake," alisema.


Alisema kisiwa hicho kinamiliwa na Zanzibar tokea mwaka miaka 1918 ambapo kilirithiwa kutoka kwa Ujerumani.

Alisema madai ya kusema kisiwa hicho si mali ya Zanzibar hayana msingi wowote hasa kutokana na kuweko kwa mikataba na sheria inaonesha ni haki ya Zanzibar.

"Serikali inatoa agizo rasmi kwa wizara husika kuandaa mipango madhubuti ya kukiendesha kisiwa hicho kwa sababu hadi sasa hakuna madai yoyote kuhusiana na kisiwa hicho,” alisema.

Kuhusu Tume ya pamoja ya Fedha, alisema kuanzisha kwa akaunti ya fedha za pamoja ni muhumu kwani ibara ya 133 inaeleza wazi kuwa akaunti hiyo ndio inayoweka fedha za muungano.


"Kuweko kwa akaunti hiyo kwa kiasi kikubwa kutaondosha hata mzozo wa muungano na  itatumiwa na wote na kuweka mipaka kati ya mamlaka ya Serikali ya Muungano na ile ya Tanzania Bara,” alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.