Habari za Punde

Bajeti ya Wizara ya Afya yakwama

Na Himid Choko, BLW
Bajeti ya Wizara ya Afya  ambayo ilikuwa inajadiliwa  katika Mkutano wa bajeti unaondelea imerejeshwa tena katika Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii ,  kwa ajili ya marekebisho zaidi.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho  amesema, Baraza  la Wawakilishi limefikia uwamuzi huo baada ya Wajumbe wengi  kubaini  mapungufu makubwa ya mgawanyo wa fedha katika bajeti ya Wizara hiyo mwaka huu.
Spika Kificho ametowa ufafanuzi huo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Chukwani.
Amesema Wajumbe hao sio tu wamebaini kiasi kidogo cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya wizara hiyo mwaka huu,  bali pia  maeneo ambayo sio   kipaumbele cha Wizara yametengewa fedha nyingi ukilinganisha na   maeneo ya kutoa huduma ambayo   yametengewa kasma ndogo mno kiasi ambacho  kitanguza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa jamii   kwa kiwango kikubwa.

Kwa hatua hiyo Mheshimiwa Spika ameagiza bajeti hiyo irudi katika  Kamati husika ili ikae  tena na Wizara ya Afya pamoja na Watendaji wa Wizara ya Fedha  kwa lengo la  kurekebisha mapungufu hayo  kabla ya kuendelea kujadiliwa tena ndani ya Baraza Jumanne ijayo.
Tukio hili linaonyesha jinsi Wajumbe wa Baraza  la Wawakilishi walivyo makini katika kuhakikisha  bajeti ya Serikali inakuwa kwa maslahi ya wananchi na si vinginevyo.
Hivi karibuni, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipatiwa mafunzo  kuhusu uchambuzi wa Bajeti kupitia mradi wa Kuimarisha Vyombo vya Kutunga sheria (LSP) na umakini huo wa Wajumbe katika kuijadili Bajeti ya Wizara ya afya unathibitisha namna mafunzo hayo yalivyosaidia katika kuwajengea Wajumbe uwezo katika eneo hilo la kujadili na kupitisha bajeti.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.