Na Mwandishi wetu
MAREKANI imeipatia Tanzania vitabu
vingine milioni 2.5 vya masomo ya sayansi kwa skuli za sekondari katika
mwendelezo wa nchi hiyo kuisaidia Tanzania kukabiliana na uhaba wa vitabu na
walimu wa masomo hayo, Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzania Mark, Chilress alisema.
Balozi Childress amezieleza habari hizo
njema kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete,
wakati walipokutana kwa mara ya kwanza tokea balozi huyo alipowasili nchini na
kuwasilisha hati zake za utambulisho.
Wakati Rais Kikwete akimweleza hali ya
utendaji wa sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii nchini na hasa jitihada za
Serikali kukabiliana na changamoto za elimu, Balozi Childress alimweleza Rais
Kikwete kuwa uchapishaji wa vitabu hivyo umeanza kufuatia uidhinishwaji wa
fedha za kuifanya kazi hiyo mwezi uliopita.
“Mheshimiwa Rais ninayo furaha
kukujulisha kuwa kazi hiyo imeidhinishwa ifanywe tokea mwezi Mei na kuwa vitabu
vitawasili nchini mwanzoni mwa mwaka ujao,” alisema.
Vitabu hivyo vya sayansi vinakadiriwa
kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni tisa na vitasafirishwa na kuwasili
nchini Januari mwakani kabla ya kufunguliwa kwa skuli kwa mwaka mpya wa masomo.
Kama ambavyo imekuwa kwa misaada ya
vitabu kutoka Marekani, miswada ya vitabu hivyo vipya imeandaliwa na kuandikwa
na wataalam wa taasisi ya Tanzania Institute of Education na kuhakikiwa na
wataalamu wa masomo hayo ya sayansi, fizikia, kemia na biolojia kabla ya
kupelekwa Marekani kwa uchapishaji.
Tanzania ilianza kupata vitabu vya
sayansi kwa mara ya kwanza tokea Rais Kikwete alipomwomba Rais wa 43 wa
Marekani, George Bush kuisaidia Tanzania
kukabiliana na changamoto kubwa za ufundishaji masomo ya sayansi mwaka 2008.
Vitabu hivyo ambavyo idadi yake ilikuwa
milioni tatu viliwasili nchini mwaka 2010 na kugawiwa katika skuli mbali mbali
za sekondari.
Rais Barack Obama aliendeleza sera ya
kutoa msaada wa vitabu vya sayansi kwa Tanzania na inakadiriwa kuwa vitabu
vya sasa vitamaliza mahitaji yote ya vitabu vya masomo ya sayansi kwa wanafunzi
wa sekondari nchini kwa angalau miaka miwili ijayo.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na
kufanya mazungumzo na Rais wa kampuni ya ujenzi wa reli ya Tanzania Railway
Construction Corporation ya China, Zhang Zongyan pamoja na Mwenyekiti wa kampuni
ya China Civil Engineering Construction Corporation, Lui Zhimng.
No comments:
Post a Comment