Hakuna huduma za maji, wananchi wajisaidia fukweni
Na Mwandishi wetu
Na Mwandishi wetu
Uharibifu mkubwa wa
mazingira umezikumba fukwe zote ambazo zinafanywa biashara ya upikaji na
uanikija dagaa hasa maeneo ya kaskazini Unguja na eneo la Maruhubi mkoa wa
mjini magharibi.
Uchunguzi uliofanywa
na gazeti hili umebaini kuwa maeneo ya Fungu refu Mto wa Pwani, Bwekunduni,
Muwanda na eneo la Maruhubi kwa kiasi kikubwa kumekuwa na uharibifu wa
mazingira unaotokana na kumwaga maji ya moto ya kuchemshia dagaa na hata mabaki
ya dagaa waliooza.
Sambamba na hilo l pia imebainika
kukatwa kwa mikoko mingi ili kutoa nafasi ya uanikaji wa dagaa katika maeneo
hayo.
Aidha mashamba
kadhaa ya maeneo ya Bwekunduni na Mto wa pwani yamevamiwa na maji chumvi baada
ya kukatwa mikoko hiyo.
Mbali na hayo,gazeti
hili pia limebaini kuwa hakuna huduma za vyoo katika maeneo ya bishara hizo
jambo ambalo linasababisha watu wanaojishughulisha na biashara hiyo, kujisaidia
pembeni mwa fukwe au sehemu za mikoko.
Pia katika eneo hilo kumekosekana maji safi na salama na kusababisha wanaoishi
maeneo hayo kutumia maji ya kuokota.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti, wakulima wa Mto wa pwani,eneo la Fungurefu kwa masharti ya kutotajwa majina yao waliliambia gazeti hili kuwa eneo kubwa
la mashamba limevamiwa na maji chumvi na hivyo kusitisha shughuli za kilimo.
“Kwa kweli nilikuwa
nalima, mpunga viazi vitamu lakini kwa sasa nusu ya shamba langu limevamiwa na
maji ya chumvi”, alisema.
Aidha alisema
wakulima wanaolima karibu na eneo hilo
wamekuwa hawapati mavuno mazuri kutokana na kuingiliana na maji chumvi.
Akizungumza na
gazeti hili, Katibu wa Kamati ya Mazingira ya Mkoa wa Kaskazini Unguja (MECA),
Hadia Ali Makame, alikiri kuwepo kwa uchafuzi wa mazingira na kwamba taratibu
zote za kuiarifa Idara husika zimefanywa lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.
Aidha alisema k
baada ya kuona hali mbaya katika eneo hilo
walilazimika kupanda mikoko ili kurejesha uhalisia wake lakini wamevunjika moyo
kutokana na miti yote kuhujumiwa.
Nae Msimamizi wa
eneo hilo, Kaite Mwadini Haji, alisema hakuna uharibifu wa mazingira katika eneo
hilo lakini alibainisha kukosekana kwa huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na
vyoo na maji safi na salama.
“Tunajaribu
kudhibiti mazingira sana lakini nikiri kuwa watu wanajisaidia katika mikoko na
maji safi hayapo mpaka tununue barabarani,” alisema.
Aidha mmoja wa
waanikaji wa madagaa, Asha Nuru, alisema serikali lazima iwawekee mazingira
mazuri kwani wamekuwa wakipata shida ya vyoo na maji.
Pia Fatma Ali na
Mtumwa Ali, ambao wameajiriwa kwa ajili ya kazi ya kupika dagaa katika eneo la
Maruhubi walikiri kuwa maji ya kuchemshia dagaa wanalazimika kumwaga maeneo
yoyote tu kwa kuwa hakuna udhibiti wa mazingira sambamba na kwenda haja kubwa
na ndogo.
Mkuu wa Wilaya ya
Kaskazini ‘A’ Unguja, Riziki Juma Simai, alikiri kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa
mazingira katika eneo la Mto wa pwani fungu refu.
“Tayari tumekutana na wavuvi, matajiri,
wapikaji na waanikaji wa madagaa wa maeneo yote na kukubaliana kupunguza eneo
hilo utaratibu ambao kwa sasa uko mbioni na utakamilika hivi karibuni,”
alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Idara ya Mazingira, Sheha Mjaja, alikiri uharibifu huo na kwamba walifanya
ziara ya makusudi katika maeneo yote ya uanikaji wa madagaa.
No comments:
Post a Comment