Habari za Punde

Makamu wa Rais Dkt.Bilal Aiwakilisha Tanzania kwenye Maadhimisho ya Miaka 52 ya Uhuru wa Burundi.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA SIKU YA UHURU WA BURUNDI
Julai 01, 2014 Bujumbura
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, leo Jumanne Julai Mosi, 2014 ameiwakilisha Tanzania katika sherehe za kilele cha miaka 52 ya Uhuru wa Burundi, sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Prince Louis Rwagasore.
Katika sherehe hizo pamoja na Makamu wa Rais wa Tanzania, pia kulikuwa na Makamu wa Rais wa Somalia, Waziri Mkuu wa Chad na viongozi mbalimbali waliowakilisha nchi kutoka Afrika. Sherehe hizo zilianza kwa Rais Pierre Nkurunzinza kuweka silaha katika eneo  maalum la Uhuru na kufuatiwa na maadhimisho yaliyoshirikisha wananchi mbalimbali katika uwanja wa Rwagasore.
Akizungumza baada ya kutoa tuzo mbalimbali za heshima, Rais Nkurunzinza aliwashukuru wageni wote waliofika katika sherehe hizo na akabainisha kuwa Tanzania ni rafiki wa Burundi hivyo anafurahishwa sana kuona ikiwa imewakilishwa na uongozi wa ngazi za juu katika sherehe hizo.
Burundi ambayo inategemea sana bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania na hasa uwepo wa Ziwa Tanganyika ambalo linaiunganisha na Tanzania, inaadhimisha miaka 52 ya uhuru huku ikiwa imepiga hatua mbalimbali kiuchumi sambamba na kisiasa kufuatia kuwa na miongo kadhaa ya mauaji ya wenyewe kwa wenyewe. Kwa sasa Burundi licha ya kukua kimaendeleo pia inaongezeka idadi ambapo inakadiriwa kuwa na watu milioni 6. Uhusiano baina ya Tanzania na Burundi unabaki kuwa wa damu ambapo pia redio za nchi hii hutangaza vipindi kadhaa kwa kutimia Kiswahili sambamba na nyimbo za muziki za wasanii wa Tanzania hupata nafasi kubwa katika redio za Burundi.
Katika sherehe hizo Mheshimiwa Makamu wa Rais pia alifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Julai Mosi, 2014 Bujumbura: Burundi
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano mwa Tanzania Mhe. Dkt Mohammed Gharib Bilal, Rais wa Burundi Mhe. P. Nkurunziza wakipokea maandamano ya maadhimisho ya Miaka 52 wa Uhuru wa Nchi hiyo yaliyofanyika leo Julai 1-2014 katika uwanja wa Prince Louis Rwegasore jijini Bujumbura Burundi. 
 
 Rais wa Burundi Mhe. P. Nkurunziza akikagua gwaride rasmi kwa ajili ya maadhimisho ya Miaka 52 wa Uhuru wa Nchi hiyo yaliyofanyika leo Julai 1-2014 katika uwanja wa Prince Louis Rwegasore jijini Bujumbura Burundi.  
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe.Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Rais wa Burundi Mhe. P. Nkurunziza walipokutana kwenye Uwanja wa Prince Louis Rwegasore jijini Bujumbura Burundi wakati wa maadhimisho ya Miaka 52 wa Uhuru wa Nchi hiyo yaliyofanyika leo Julai 1-2014.  

Ujumbe wa Tanzania uliofuatana na Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal kwenye maadhimisho ya Miaka 52 wa Uhuru wa Nchi hiyo yaliyofanyika leo Julai 1-2014 katika uwanja wa Prince Louis Rwegasore jijini Bujumbura Burundi. No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.