Habari za Punde

Sakata la wanafunzi kufundishwa bibilia


Wizara ya Elimu yachukua hatua

Uchunguzi wabaini ukweli wa madai hayo

Na Khamisuu Abdalla

SIKU mbili tu baada ya gazeti hili kuchapisha habari kuhusu wanafunzi kusomeshwa bibilia na kutakiwa kutokwenda skuli wakiwa wamefunga, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imefanya uchunguzi na kubaini kwamba tuhuma hizo ni za kweli.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Majestik, Mrajisi wa Elimu Zanzibar, Siajabu Suleiman Pandu, alisema baada ya uchunguzi kufuatia habari, waligundua malalamiko ya wazazi ya wanafunzi ni ya kweli.

Alisema alipohojiwa, mmiliki wa skuli hiyo inayoitwa Eden International,Pilsoon Youn (maarufu mama Kim), alikiri kwamba anatoa elimu ya bibilia kwa wanafunzi.

Alisema katika kuta za madarasa kumebandikwa vipande vya aya za bibilia  ambavyo vinathibitisha kwamba bibilia inasomeshwa.

Hata hivyo, alisema bibilia inafundishwa huku idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo ni Waislamu.


Mrajisi huyo alisema baada ya kuwahoji wanafunzi walielezea kusikitishwa kutosomeshwa dini yao (Uislamu) licha ya wingi wao madarasani na badala yake kufundishwa bibilia.

Aidha alisema hata mavazi ya wanafunzi hayaridhishi kwa sababu wanafunzi wa kike wa kiislamu hawaruhusiwi kuvaa hijab.

Alisema kulazimisha wanafunzi kusoma bibilia ni kinyume na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Muungano ya mwaka 1977, ambazo zimetoa uhuru kwa mtu kufuata dini aitakayo bila kulazimishwa.

“Hakuna kosa mtu kufundisha dini bali ni kosa kuwalazimisha watoto kusoma dini ambayo sio ya kwao,” alisema.

 “Wakati nilipokuwa nikipata maelezo kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa kiislamu wanaosoma katika skuli hiyo walisikitishwa sana kutosomeshwa dini yao licha ya kuwa wingi madarasa na badala yake kulazimishwa kusoma bibilia,” alisema Mrajis huyo.

Alisema sheria ya elimu kifungu 47 hadi 48 kinasema kuwa skuli au tasisi za kidni zinaweza kuanzishwa  chini ya sheria hiyo kifungu kidogo (2) pale skuli au tasisi za aina hii zinapoanzishwa masharti ya kifungu

Kifungu cha 13 (3) cha sheria ya elimu namba 6 ya mwaka 1982,kinasema  skuli au tasisi za kidini hazitojumuisha darasa au mafundisho mengine ya kidini yanayotolewa misikitini, makanisani au katika sehemu nyengine zozote za ibada mradi tu darasa au mafundisho hayo ni ya kidini kwa kila hali.”

Aidha kifungu cha 48 cha sheria hiyo kinasema: “Bila  kujali masharti ya kifungu cha 47 cha sheria hii (namba 6 ya 1982) mafundisho ya kidini yataweza kutolewa katika skuli yoyote ya serikali au binafsi au inayosaidiwa, mradi tu wakati wa utekelezaji wa masharti ya kifungu hiki, imani za kidini mbalimbali walizomo wanafunzi zitazingatiwa ili kuhakikisha mwanafunzi anapatiwa mafundisho ya dini ile inayomruhusu.”

Alisema  mmiliki wa skuli hiyo alikuja Zanzibar kama taasisi ya Africa Agape Assosiation, kwa ajili ya kuanzisha skuli na kusomesha watu masuala ya kidini na kumjua mungu.

Hata hivyo, alipofanya kikao na wazazi wa wanafunzi kabla ya kuandikishwa, aliwahakikishia kwamba skuli hiyo haitafundisha dini ya aina yoyote.

Mrajisi huyo alisema wizara tayari imeshajipanga kuhakikisha hatua nyengine za kisheria zinachukuliwa.

 “Sisi kama Wizara tayari tumeshajipanga na tunaendelea kujipanga kulifanyia kazi suala hili kwa kuliandikia ripoti ili hatua nyengine zichukuliwe kwani kama Mrajisi  sina mamlaka ya kuifungia skuli hii bali wenye mamlaka ni Baraza la Elimu,” alisema.

Akizungumzia kuhusu usajili wa skuli hiyo, alisema kwa mujibu wa taarifa aliyoipata Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) usajili wa skuli hiyo sio wa kudumu  na kwamba ilisajiliwa kwa namba RPS/329 mwaka 2010/2011.

Lengo la kutoa usajili wa muda ni kutoa nafasi ya kuchunguza malengo na dhamira yake kabla ya kupewa usajili wa kudumu.

Alisema katika kuondoa matatizo kama hayo, wameanzisha msako wa kutafuta skuli ambazo hazijasajiliwa ambapo tayariu skuli 40 zimekamatwa.

Akizungumzia madai ya skuli ya     Karibu ya Kijichi ya mwalimu kuwalazimishwa watoto kuweka maji mdomoni katika kipindi hichi cha Ramadhani, alisema tayari mwalimu aliefanya kitendo hicho ameshafukuzwa skuli.

Hivi karibuni mama Kim ambae ni raia wa Korea, aliwataka wazazi wa wanafunzi wa skuli ya Aden kuwahamisha watoto wao kama wanashindwa kutekeleza masharti.

Aidha alikiri skuli yake kufundisha bibilia na kuwalamisha wanafunzi waliofunga kutokwenda skuli.

Kauli ya mama Kim, ilikuja baada ya wazazi wa wanafunzi hao, kusema watoto wao wanafundishwa bibilia na kulazimishwa kwenda skuli na chakula wakati wamefunga au kutokwenda skuli kabisa.

2 comments:

  1. Wacha tulipe gharama za ujinga kidogo!

    Haya ni matokeo ya Taasisi za kiislamu kushindwa kuona mahitaji ya wakati kwa waumini wao kwamba sio misikiti na madrassa peke yake bali skuli pia!

    ReplyDelete
    Replies
    1. @Adhubany Nakubaliana nawe kwa upande mmoja, mila nashauri tusiwazilaumu hizi Taasisi za Kiislam kwa sasa kwani lawama hazitasaidia. La msingi tukae nazo tuzielimishe na tuzishauri kwamba kuna ulazima sasa kuwa name skuli, hospital bora za kiislam, kwani hata kwenye sekta ya afya nako kuna matatizo hasa kwa mama zetu wakati wa kujifungua maadili ya kiislam yanakiukwa sana

      Delete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.