Na Joseph
Ngilisho,Arusha
UGAIDI wa aina yake
umegubika jiji Arusha, ambapo watu wasiofahamika wanaotumia usafiri wa
pikipiki, wanawashambulia kwa risasi wanawake hasa wenye usafiri wa magari bila
kupora chochote.
Tayari wanawake
watatu wamepigwa risasi katika maeneo tofauti jijini hapa huku mmoja kati yao
aliyetajwa kwa jina la Shamim Rashird Yulu (30) mkazi wa Mbauda akipoteza maisha.
Marehemu alipigwa risasi
ya shingo na anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Mbauda.
Kamanda wa Polisi
mkoani hapa, Liberatus Sabas, alisema mashambulizi hayo ni ya kigaidi kwani
wahusika baada ya kushambulia hawachukui chochote na wamekuwa wakiwalenga
wanawake wenye magari pekee.
Akizungumzia
shambulizi lililosababisha kifo, alisema limetokea juzi majira ya saa 3:00
usiku katika eneo la Sakina kwa Iddi wakati marehemu akijaribu kuingia nyumbani
kwake.
Alisema marehemu
alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Saloon yenye namba za usajili T506 BYA
na kwamba alipofika eneo hilo watu wasiofahamika wakiwa na pikipiki walimpiga
risasi shingoni na alifariki muda mfupi katika hospitali ya Selian.
Aidha katika tukio
jingine mwanamke mwingine ambaye ni mke wa Mkurugenzi wa Shirika linalotetea
haki za wafugaji la Pingos, Flora Porokwa, amelazwa hospitali ya Seliani baada
ya kupigwa risasi kwapani iliyotokezea mgongoni na kuacha jeraha kubwa.
Mwanamke huyo
alisema baada ya kufika eneo la kwa Iddi akiwa na gari lake aliona watu wawili
wakiwa na pikipiki wakimzuia kwa mbele wakati akijaribu kukata kona ya kuingia
bara bara ya vumbi ili aelekee nyumbani kwake.
Alisema mmoja wao alimfuata na kumpiga risasi bila kuchukua
chochote.
Tukio kama hilo limetokea
eneo la Olasiti ambapo mwanamke mmoja asiefahamika jina alijeruhiwa kwa risasi
na amelazwa hospitali ya mkoa ya Mount Meru akiendelea na matibabu.
Kamanda Sabas alisema
tayari jeshi la polisi limeanza mazungumzo na wadau mbali mbali wakiwemo
wafanyabishara kuangalia uwezekano wa kufunga kamera za CCTV kwenye mitaa mbali
mbali jijjini hapa, zitakazosaidia kupunguza matukio ya kihalifu.
Wakati huo huo watu
watatu wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za ugaidi huku mmoja aliyetajwa kwa
jina la Adamu Musa Pakasi (34) mkazi wa Siwandeti wilayani Arumeru,akikutwa na
bunduki ya kienyeji inayotumia risasi za short gun.
Alisema mbali na
silaha hiyo pia alikutwa na risasi 38 za short gun,mafuta ya kusafishia bunduki
na ganda moja la risasi.
Alisema watuhumiwa
hao wanahusishwa na mtandao wa kigaidi wa kuripua mabomu na kwamba silaha hizo
ni sehemu ya silaha zilizokuwa zikitumika kwenye uhalifu na uripuaji wa mabomu.
Mtuhumiwa huyo
alikutwa na silaha hiyo pamoja na risasi zikiwa kwenye mfuko wa nailon nyumbani
kwake na kwamba polisi itawafikisha mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
No comments:
Post a Comment