Na Mwantanga
Ame,Dodoma
Kambi ya Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKAWA), inazidi kubomoka, baada ya wajumbe wengine kutoka vyama
vya CHADEMA na CUF kuonekana katika viwanja vya bunge.
Tayari wajumbe
kutoka kundi la UKAWA walioonekana katika viunga vya bunge wamefikia sita.
Hata hivyo, viongozi
wakuu wanaounda umoja huo wanaendelea na msimamo wa kutorudi bungeni.
UKAWA, waliamua utoka
bungeni Aprili mwaka huu, wakilalamikia kubaguliwa na kudhalilishwa.
Hali hiyo, ilisababisha
viongozi mbali wakiwemo wa kisiasa na dini kuwaomba kurejea bungeni kuendelea
kujadili rasimu.
Jana asubuhi mwandishi
wa habari hizi, aliwashuhudia wajumbe wengine kutoka chama cha CUF wakifanya
usajili.
Waliojitokeza jana
ni Mbunge wa Mtanda mjini, Said Arif (CHADEMA), huku pia kukiwa na wajumbe
wengine watano kutoka UKAWA waliojisajili na kupokea posho wakiwemo kutoka CUF.
Katibu wa bunge
hilo, Yahya Khamis Hamad, alithibitisha kuwepo kwa wajumbe hao na kusema hadi
jana asubuhi walishafikia sita huku kukiwa na taarifa za Mbunge mwengine
kujisajili.
Alisema hadi mchana wabunge
wote waliosajiliwa walikuwa 425 wakiwemo sita kutoka UKAWA.
Aliiwataja wajumbe
hao kuwa ni Clara Mwaitupa Mbunge wa Viti Maalum (CUF),Mbunge wa Viti Maalum,
Leticia Nyerere (CHADEMA), Mbunge wa Maswa, John Shibuda, Ali Omar, Jamila
Abeid na Fatma Mohammed Hassan.
Alisema baadhi ya wajumbe
hao wameanza kupokea posho ya shilingi 230,000 na shilingi 70,000 huku wengine
wakiwa bado jawajalipwa kutokana na kubanwa na kanuni.
Alisema utaratibu
uliotolewa ni kwamba mjumbe anatakiwa kupewa posho ya siku saba kwa ajili ya
kujiweka vizuri.
Wajumbe wa bungehilo
tayari wameanza mjadala kwenye kamati 12, ambazo zinajadili sura 15 za rasimu
hiyo, kazi ambayo itakamilika Oktoba.
Taarifa za ndani
ambazo Zanzibar Leo imezipata nje ya bunge, huenda idadi ya wajumbe hao
ikaongezeka wiki ijayo baada ya UKAWA, kumaliza mjadala wao unaotarajiwa
kufanyika mjini Dar es Salaam.
Wakati huo huo,
Mwenyekiti wa Kamati namba mbili ya bunge, Shamsi Vuai Nahodha, amesema baadhi
ya sura ya rasimu ya katiba zimekumbwa na msukosuko na kutopata theluthi mbili
na sasa watasubiri kura kuu ya bunge.
Nahodha, aliyasema
hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa jengo la
hazina mjini hapa.
Alisema katika
mjadala wao ibara ya 19 na 22 za rasimu hiyo, zilikosa kupata maamuzi baada ya
kutopigiwa kura kutokana na kutotimia kwa akidi ya wajumbe kutoka Tanzania Bara
na Zanzibar.
Alisema kwa mujibu
wa sheria,ibara hizo zlitakiwa kupata theluthi mbili ya kura kati ya Tanzania
Bara na Zanzibar.
Alisema wajumbe
waliotarajiwa kupiga kura hiyo kwenye kipengele hicho kwa upande wa Zanzibar
walitakiwa kuwa 12, lakini alikosekana mtu mmoja, huku sura ya 11 ilikosa mtu
mmoja kwa upande wa Tanzania Bara baada ya waliokuwepo kufikia 22 badala ya 23.
Alisema sura hizo
zinahusu maadili ya uongozi na utumishi wa umma, ambayo imebeba vipengele
vinavyohusu dhamana ya uongozi wa umma na kanuni za uongozi wa umma pamoja na
zawadi katika utumishi wa umma.
Alisema kuanzia sasa
kiongozi wa umma wakati anapotekeleza shughuli za kiserikali, akipewa zawadi,
zawadi hiyo itakuwa ni mali ya Jamhuri ya Muungano na ataiwasilisha kwa Katibu
Mkuu Kiongozi kupitia Katibu Mkuu wa Wizara au kiongozi wa taasisi ya serikali
inayohusika.
Alisema bunge hilo
litatunga sheria itakayosimamia pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina
na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.
Aidha alisema hadi
jana hakukuwa na mvutano wowote uliojitokeza.
No comments:
Post a Comment