STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 04 Septemba , 2014
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza mazishi ya marehemu Mhe. Ali
Khamis Abdalla aliyekuwa Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Mazishi ya
Marehemu Ali Khamis Abdalla yalifanyika Fuoni, Wilaya ya Magharibi Unguja Mkoa
wa Mjini Magharibi, ambapo miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni pamoja na
Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe.
Pandu Ameir Kificho.
Wengine ni
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji,
viongozi wengine wa dini, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wakuu wa vikosi vya
Ulinzi na Usalama pmoja na viongozi wengine vyama vya siasa na Serikali.
Mapema Dk. Shein
alishiriki na kuungana na wananchi pamoja na wanafamilia na viongozi mbali
mbali wa dini vyama na Serikali katika sala ya kumsalia Marehemu Ali Khamis Abdalla
iliyofanyika huko katika Mskiti wa Masjid Mahfoudh-Mazizini nje kidogo ya mji
wa Zanzibar.
Mazishi hayo
yalifanyika kwa heshima zote za Kidini na Serikali ikiwa ni pamoja na kupigwa
risasi baridi pamoja na Paredi la Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Ali
Kahmis Abdalla alizaliwa mwaka 1914 Nganani, Makunduchi na alikulia katika
kijiji cha Ndijani na kupata elimu yake ya awali mwaka 1925 katika skuli ya
Ndijani hadi mwaka 1928.
Baada ya kurejea
masomoni aliajiriwa kama Msaidizi Afisa Kilimo (Assistance Agricultural Oficer)
mnamo mwaka 1942 ambapo mnamo mwaka 1952 aliteuliwa kuwa Meneja wa shamba la
Serikali Kizimbani, pamoja na majukumu hayo aliendelea na kazi hizo za
kilimo katika maeneo ya Chukwani na
Selemu Pemba hadi mwaka 1963.
Mwisho wa mwaka
wa 1963 alichaguliwa kuwa Katibu katika Ubalozi wa Zanzibar nchini Misri na
alitumikia kwa miezi minne hadi April 1964, baadae aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu
wa Wizara ya Kilimo hadi 1967 na mwaka 1968-1975 alifanya kazi katika mashamba
ya Mikonge huko Tanga.
Mnamo tarehe 21
Oktoba mwaka 1985 alichaguliwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi akiwa Spika
wa Pili toka kuanzishwa kwa Baraza hilo mwaka 1980 na alidumu na wadhifa huo
hadi mwaka 1995.
Wakati wa uongozi
wake akiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi alikuwa na busara, hekima na ujasiri
katika kusimamia maamuzi ya chombo hicho muhimu cha kutunga Sheria.
Miongoni mwa
baadhi ya mambo aliyoyasimamia katika kazi yake hiyo ni pamoja na kuliingiza
Baraza hilo katika Mabaraza ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CPA) ambapo
pia chini ya uongozi wake alifanikiwa kuendesha kikao ambacho kilichopitisha
Sheria namba 15 ya mwaka 1992 iliyohusiana na mfumo wa siasa ya vyama vingi
nchini Tanzania jambo ambalo limetengeneza historia kubwa hapa nchini.
Marehemu Ali
Khamis hadi kufa kwake amejaaliwa kupata watoto 13 na wajukuu 39 na ameacha
kizuka mmoja.
Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar pamoja na Baraza la Wawakilishi ilitoa mkono wa pole kwa
wafiwa wote na kuwataka wawe na subra katika msiba huo.
Nao wanafamilia
walitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na viongozi
wote na wananchi pamoja na Jeshi la Polisi kwa kutoa ushirikiano wao mkubwa katika
mazishi ya mzee wao huyo.
Rajab
Mkasaba
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment