Habari za Punde

Dk Shein : Sekta ya Utalii ni eneo linalopewa kipaumbele katika ushirikiano kati ya Comoro na Zanzibar

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                          17 Septemba, 2014
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Moroni, Comoro
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema sekta ya utalii ni moja ya sekta ambazo Zanzibar na Muungano wa Comoro zinajiandaa kushirikiana kwa karibu ili kukuza sekta hiyo kwa manufaa ya serikali na wananchi wa pande mbili hizo.
 
Akijibu maswali kutoka kwa mwandishi wa Kituo cha Taifa cha Televisheni na Redio Comoro jana huko katika fukwe ya Mitsamihouli (tamka Misamihuli) katika siku yake ya pili ya ziara yake ya siku nne nchini humu, Dk. Shein alisema Comoro ina nafasi nzuri ya kuendeleza sekta ya utalii kama ilivyofanya Zanzibar.
 
Alikieleza kituo hicho kuwa eneo hilo la Mitsamihouli linafafana na maeneo mengi ya Zanzibar kama vile Nungwi, Kiwenga, Kizimkazi na mengineyo ambayo yanatumika kwa shughuli za kitalii ambapo Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuvutia wawekezaji na kuchukua hatua nyingine kuimarisha sekta hiyo.
 
Alifafanua kuwa sekta hiyo ni moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati Zanzibar na Comoro yanayoendelea hivi sasa wakati wa ziara yake.
 
Dk. Shein alibanisha kuwa mbali ya ushirikiano baina ya pande mbili hizo, Mpango wa Magharibi wa Bahari ya Hindi wa Chagamoto za Ukanda wa Pwani ambao ulizinduliwa hivi karibuni nchini Samoa ambapo Zanzibar na Comoro ni washiriki utatoa fursa zaidi kwao kushirikiana kwani moja ya malengo yake ni kuimarisha sekta ya utalii miongoni mwa washiriki wa mpango huo.
 
Kabla ya kutembelea eneo hilo la fukwe ya Mitsamihouli, Dk. Shein ambaye alikuwa amefuatana na Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Ali Mohamed Soilihi, alishiriki sala ya Adhuhuri katika msikiti mkuu wa mji huo ambao una historia kubwa ya ushirikiano wa kidini na kijamii kati ya visiwa vya Comoro na Zanzibar.
 
Katika salamu zake kwa wakazi wa mji huo mara baada ya sala hiyo ambayo iliongozwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Dk. Shein aliwahimiza watu wa Mitsamihouli kuienzi na kuiendeleza historia ya udugu na ushirikiano kati watu wa Zanzibar na Comoro.
Aliwaeleleza wananchi hao kuwa mlahaka mzuri na wa kihistoria walionao watu wa mji huo na Zanzibar hauko katika masuala ya dini pekee lakini hata katika mila, desturi na utamaduni.
 
Aliwaeleza kuwa ziara yake nchini Comoro imelenga kuimarisha uhusiano huo ambapo yeye na Rais wa Muungano wa Comoro mara zote walipokutana wamekuwa wakizungumzia dhamira ya kweli ya kudumisha na kukuza uhusiano kati ya watu wa Zanzibar na Comoro.
 
Naye Imamu wa msikiti huo sheikh Mouendhu (tamka Muendhu) Msaidie alimshukuru Dk. Shein kwa kuupa heshma mji wao kwa kuutembelea na kueleza kitendo hicho kuwa ni ishara ya mapenzi yake kwa udugu na urafiki wa watu wa Comoro na Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
 
Sheikh Msaidie alieleza kuwa upendo wa watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa watu wa Comoro unawafanya wananchi wa Comoro wanapofika nchini Tanzania kujisikia wako nyumbani na kuwashukuru kwa upendo wao.
 
Alisema watu wa Comoro wanajisikia huru zaidi kwenda Tanzania kwa shughuli zao mbali iwe za kibiashara au shida za kimatibabu kwani huko hupata faraja na hawajioni wapweke hata pale wanapopata shida kama misiba machungu yao huwa tofauti wakiwa na ndugu zao wa Tanzania.   
 
Mapema kabla ya kwenda Mitsamihouli, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitembelea kiwanda cha uvuvi na kuona sehemu mbali mbali za kiwanda hicho zikiwemo za uundaji wa boti za uvuvi za ukubwa mbalimbali, sehemu za kuhifadhi samaki na Ofisi.
 
Jana jioni, Dk. Shein alitarajiwa kutembelea Ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini humo ambako angezindua tovuti ya ubalozi huo na baadae kuzungumza na watanzania wanaioshi nchini Comoro.
 
Leo anatarajiwa kuendelea na ziara yake ambapo mapema asubuhi akiwa ameambatana na Mufti Mkuu wa Comoro atatembelea Chuo Kikuu cha Comoro kitivo cha (dini) Imam Shafi na makaburi ya viongozi mashuhuri wa dini ya kiislamu nchini Comoro.
 
Wakati wa mchana atatembelea kiwanda cha kusindika maua ya mlangilangi na karafuu na jioni atashiriki chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshma yake na Gavana wa Ngazija Mheshimiwa Moingibaraka (tamka Mwinyibaraka) Said Soilihi. 
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kumaliza ziara yake ya siku nne nchini humu kesho ambapo kabla ya kuondoka atazungumza na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Rais wa Muungano wa Comoro Dk. Dhoinine Ikililou.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.