STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 28 Septemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekitki wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema, katika miaka michache ijayo, Zanzibar itakuwa na madaktari wa kutosha kufikia uwiano uliopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) wa angalau daktari mmoja kuhudumia watu elfu kumi (10,000) kwa nchi zinazoendelea.
Dk. Shein ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akizungumza katika mahafali ya kwanza ya Skuli ya Udaktari ya Zanzibar inayoendeshwa kwa ushirikiano na Chuo kikuu cha Matanzas cha Cuba yaliyofanyika katika Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni mjini Unguja.
Katika mahafali hayo wanafunzi wa udaktari 38 ambao walichukua mafunzo yao hapa Zanzibar na nchini Cuba walikabidhiwa shahada zao za udaktari kutoka kwa Mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Matanzas Dk. Luis Ulpiano Perez Marques.
Dk. Shein aliwaeleza wahitimu na wageni waliohudhuria Mahafali hayo kuwa kuhitimu madakatari hao 38 kwa mpigo hapa Zanzibar ni ushahidi wa kutosha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikitekeleza kwa vitendo azma yake ya kuwapatia wananchi waker huduma bora za afya.
Alifafanua kuwa mwanzoni mwa mwaka huu uwiano wa daktari kwa idadi watu kwa Zanzibar ulikuwa ni daktari mmoja kwa wananchi 18,982 lakini kuhitimu kwa madaktari hao kumeleta mabadiliko katika uwiano huo.
Hata hivyo alisema katika kipindi kifupi kijacho vijana wengi waliopelekwa kusomea udaktari nchi za nje pamoja na Tanzania Bara watamaliza masomo yao hivyo kuongeza idadi ya madaktari na hivyo kupunguza pengo la uwiano huo.
Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliweka lengo la daktari mmoja kuhudumia wananchi 6,000 na kubainisha kuwa hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kutekeleza lengo hilo na kuwahakikishia wananchi kuwa kwa hali inavyokwenda kuna kila dalili kuwa lengo hilo litafikiwa.
Katika kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na wataalamu bingwa katika fani mbalimbali za udaktari, Dk. Shein alisema serikali itaandaa programu maalum itakayowapa fursa madaktari wanaomaliza masomo kujiunga na mafunzo ili kuwa kupata madaktari hao bingwa.
Aliongeza kuwa azma ya serikali hivi sasa ni kupata madaktari bingwa vijana watakaoweza kutoa huduma kwa miaka mingi kabla ya kustaafu hivyo Serikali itachukua hatua za makusudi kuwashawishi madaktari vijana kuendelea na mafunzo ili kuwa mabingwa katika fani wanazipenda na zile ambazo baadhi yao hawazipendi lakini ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya nchini.
Kwa hivyo alisisitiza suala la kuweka uwiano kati ya matakwa ya aina ya fani zinazopendelewa na madaktari na hali halisi ya mahitaji ya mabingwa wa afya katika fani nyingine ambazo wengi hawazipendelei lakini mi muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na Serikali tangu Mapinduzi ya mwaka 1964 ambapo moja ya ajenda yake ni kuwema hali za wananchi sawa katika utoaji wa huduma zote kwa wananchi ikiwemo afya.
Katika kufanya hivyo alisema utaratibu wa mafunzo yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Matanzas yaliwahi kutolewa pia miaka ya 1970 ambapo wadaktari wanafunzi 14 walipatiwa mafunzo ya miaka 4 Zanzibar na kuedelea na masomo yao kwa miaka miwili katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Nanjing nchini China na kuhitimu shahada ya udaktari katika chuo hicho.
Katika hotuba yake hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitoa shukrani za pekee kwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume ambaye ziara yake aliyoifanya nchini Cuba mwaka 2006 ndio iliyozaa skuli hiyo ya udaktari.
Alisema wazanzibari wanajivunia mafanikio hayo na kumshukuru Dk. Karume kwa busara zake na jitihada alizochukua hadi kupekelea kuanzishwa kwa mafunzo hayo na hatimae Zanzibar kwa mara kwanza imeweza kupata wahitimu wa udaktari katika ardhi yake wenyewe.
Akizungumza katika mahafali hayo Balozi wa Cuba nchini Tanzania Mheshimiwa Jorge Luis Lopez Tormo alipongeza jitihada za pamoja kati ya wahadhiri na madaktari wa Cuba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya kwa mafanuikio hayo.
Alitoa pia pongezi kwa wahitimu wa mafunzo hayo kwa kuwaamini wataalamu wa afya wa Cuba na wakati wote kuonesha dhamira na utayari wao kujifunza hadi kumaliza mafunzo hayo kwa kupata alama za juu.
Balozi huyo alisema nchi yake imeweza kuchangia mafunzo kwa madaktari na wataalamu wa afya katika nchi 121 katika bara la Asia, Afrika na Amerka wakati hivi sasa nchi yake inaratibu mafunzo ya udaktari yanayoshirikisha wanafunzi 29,580 katika nchi kumi ulimwenguni ikiwemo Tanzania.
Awali akitoa maelezo katika mahafali hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Saleh Mohamed Jidawi alisema mafunzo hayo yamegharimiwa kwa kiwango kikubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kuwa Serikali ina mpango wa kuwapatia madaktari hao mafunzo zaidi ili kupta mabingwa katika fani mbalimbali za afya.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment