Habari za Punde

Shirika la UNFPA Yakabidhi magari ya Wagonjwa Zanzibar.

Na RAMADHANI ALI /MAELEZO ZANZIBAR                        
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) limekabidhi  msaada wa magari manne ya Ambulance  kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar ambayo yatatumika katika Hospitali nne.

Mwakilishi wa UNFPA Tanzania  Dkt. Natalia Kanem alimkabidhi Waziri wa Afya Rashid Seif Suleiman magari hayo katika sherehe zilizofanyika   Wizarani Mnazimmoja.

Dkt. Natalia alitaka  magari hayo yatumike kwa uangalifu ili  kufikia malengo ya millennia  ya kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto wanaozaliwa hasa katika maeneo ya vijijini.

Alisema moja ya sababu inayopelekea vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga ni tatizo la usafiri ambalo linachangiwa na uwezo mdogo wa baadhi ya familia hasa katika maeneo ya vijijini.

Aliongeza kuwa  msaada huo ni  sehemu ya Mpango maalum wa Shirika la Umoja wa  Mataifa  ulioanza  mwaka 2011 na kumalizika Juni 2015  ambao  huenda ukaendelea hadi mwaka 2016 kusadia  masuala ya Afya na Lishe.

Amesema  mpango huo wa miaka minne  ambao unahusisha maeneo  makuu saba unaendeshwa kwa pamoja na Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa  ambayo ni WHO, UNFPA, UNICEF na WFPA.


Mwakilishi huyo wa UNFPA amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Jakaya Mrisho Kkwete na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Muhamed Sheina kwa juhudi kubwa wanazochukua katika kuimarisha huduma za  mama wajawazito na watoto wachanga.

Aliesema UN inathamini juhudi hizo na  juhudi za kuimarisha uchumi hivyo aliahidi  kuwa wataendelea  kuunga mkono kuhakikisha mama wajawazito na watoto wanaozaliwa wanaendelea kuishi katika mazingira yaliyo  salama.

Waziri wa Afya  Rashid Seif Suleiman, alilishukuru Shirika la UNFPA kwa misaada mbali mbali inayotoa kwa Wizara hiyo  na ameahidi kuwa magari hayo yatatumika katika malengo yaliyokusudiwa.

Amekiri kuwa tatizo la usafiri kwa  mama wajawazito Zanzibar limekuwa likiwasumbua wananchi wengi na inafikia wakati akinamama hujifungua wakiwa kwenye gari  wakati wa kupelekwa Hospitali ambazo hazina stara wala hazifai kwa kazi hiyo.

Alieleza matarajio  yake kuwa tatizo hilo kwa sasa litapungua kwa kiasi kikubwa baada ya kupatiwa msaada huo ambao umekuja wakati muwafaka ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaelekeza juhudi zake kuimarisha  huduma za afya mijini na vijijini.

Gari hazo za ambulance ambazo zitapelekwa katika Hospitali ya Kivunge, Mwembeladu, Mkoani na Micheweni zimegharimu shilingi milioni 245,000,000 za kitanzania.
                                                  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.