Na Salum
Vuai
Pamoja na
kuwepo sheria nzuri na kanuni za usimamizi wa sekta ya usafiri nchini, bado
ajali za barabarani zimeendelea kuongzeka na kupoteza maisha ya wananchi wengi.
Aidha ajali
hizo zimekuwa zikisababisha ulemavu wa kudumu kwa watu wengi na kuharibu
miundombinu, hali inayoitia hasara kubwa serikali.
Katika kikao
cha nne cha kawaida cha Bodi ya Usafiri Barabarani kilichofanyika katika ofisi
ya Mfuko wa Barabara Maisara mjini Zanzibar, wajumbe walieleza kusikitishwa
kwao na hali hiyo, licha ya kuwepo mikakati mbalimbali kuidhibiti.
Takwimu za
kitengo cha usalama barabarani cha Jeshi la Polisi zilizowasilishwa kwenye
kikao hicho, zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka minne, 2010/2013 jumla ya
ajali 3,217 zilitokea Unguja na Pemba, zikihusisha vyombo mbalimbali vya moto,
baiskeli, waendao kwa miguu na wanyama.
Vifo 480
vilitokea kutokana na ajali hizo, ambapo wanaume waliopoteza walikuwa 404 na
wanawake 76.
Aidha, watu
4,361 walijeruhiwa, kati yao, wanaume 3346 na wanawake 1015.
Katika kikao
hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Mussa Msheba Suleiman, ilielezwa
kuwa, idadi hiyo ya ajali ni ya kutisha kwani inaendelea kupukutisha ya nguvu
kazi inayotegemewa na nchi katika kuleta maendeleo.
Mchanganuo
wa takwimu hizo unaonesha kuwa, mwaka 2013, ndio ulioongoza kwa kuwa na ajali
nyingi zilizofikia 836, zikisababisha
vifo 126, (wanaume 109 na wanawake 17), na mejeruhi 1,139, (wanaume 824 na
wanawake 315).
Kwa mujibu
wa takwimu hizo, idadi ya ajali imekuwa ni ya kupanda na kushuka kati ya mwaka
2010, 2011 na 2012.
Mwaka 2010, jumla
ya ajali zote ilikuwa 747, vifo 112 (wanaume 92, wanawake 20), na majeruhi
1264, wakiwemo wanaume 920 na wanawake 344.
Mnamo mwaka
2011, jumla ya ajali 809 ziliripotiwa Unguja na Pemba, ambazo zilisababisha
roho za watu 106 kupotea, wanaume 90 na wanawake 16.
Ajali hizo
za mwaka 2011 ziliacha majeruhi 1,056 wakiwemo wanaume 887 na wanawake 169.
Mwaka 2012
watu 136 walifariki dunia kutokana na ajali 825 zilizotokea, na kati ya hao,
wanaume walikuwa 113 na wanawake 23, huku watu 902 wakijeruhiwa (wanaume 715 na
wanawake 187).
Wajumbe hao
wa Bodi, katika kuelezea ongezeko la ajali nchini, walisema hali hiyo
inasababishwa na mambo mengi ikiwemo madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri
kuzifumbia macho sheria na kanuni zilizopo.
Kwa upande
mwengine, walisema pamoja na jeshi la polisi kujitahidi kuwashika wanaokiuka
sheria na kuwafikisha mahakamani, lakini ni hukumu chache sana zinazotolewa kwa
wahusika, au kupewa adhabu ndogo kulinganisha na ukubwa wa makosa hao.
Walishauri
hatua mbalimbali za kuchukua ili kupunguza idadi ya ajali, ikiwemo Idara ya
Usafiri na Leseni kuweka wakaguzi wake barabarani ili kukabiliana na madereva
na matingo wakorofi.
No comments:
Post a Comment