Na Othman
Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, amesema mfungamano wa kibiashara uliopo
baina ya Zanzibar na Mataifa ya Ghuba na Mashariki ya mbali, utaimarika
kufuatia kuongezeka mawasiliano ya anga kati ya pande hizo.
Alisema hayo wakati akizindua
safari za anga kati ya Dubai na Zanzibar zilizoanzishwa na kampuni ya kimataifa
ya usafiri wa ndege ya Flydubai, hafla iliyofanyika uwanja wa ndege wa
Zanzibar.
Alisema wafanyabiashara wa
Zanzibar pamoja na mwambao wa Afrika Mashariki, wamekuwa wakilitegemea soko la
Dubai ambalo ndilo wanalolitumia kupata biadhaa zao.
Alisema uanzishwaji wa safari
hizo za moja kwa moja utakuwa kiungo kizuri kwa wafanyabiashara kuendeleza
biashara zao kwa kiwango kikubwa zaidi.
Alisema uimarishaji wa uwanja
wa ndege wa Zanzibar unaoendelea, umelenga kutoa huduma zinazokubalika kimataifa.
Alisema mkakati zaidi umewekwa kuhakikisha
uwanja huo unakuwa na mazingira rafiki ya kuyashawishi mashirika mbali mbali ya ndege ya kimataifa kufanya safari zake
Zanzibar.
“Uwanja wetu tulilenga utoe
huduma za moja kwa moja kati ya Zanzibar na mataifa mengine ya Ghuba, Mashariki
ya Kati na Ulaya. Hivi sasa tumeanza kupata faraja kwa kuona mashirika ya ndege
ya Ethiopia, Qatar na Oman,” alisema.
Aliipongeza Flydubai kwa uamuzi
wake wa kuanzisha safari hizo kati ya Dubai na Zanzibar.
Akitoa taarifa ya kampuni hiyo,
Makamu wa Rais wa kampuni hiyo, Sudhir Screedhara, alisema kampuni yake tayari
inaendelea kutoa huduma kwa karibu miji 12 ya mataifa ya Afrika.
Alisema mradi wao unaotumia
ndege mpya za kisasa aina ya Boeing
zipatazo 100 umewekeza kiwango cha fedha karibu dola za Marekani 60,000,000.
Aliipongeza Zanzibar kwa
kukubali kwake kuunga mkono uamuzi wa kampuni hiyo wa kutoa huduma za ndege
kati ya Dubai na Zanzibar.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya
Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, Dk. Juma Malik Akil, alisema serikali
itakuwa makini kuhakikisha miradi yote inayohusu sekta hiyo inasimamiwa vyema.
Alisema Flydubai itasaidia kuongeza
idadi ya watalii wanaongia Zanzibar kufikia milioni 2 kati ya mwaka 2015 hadi
2025.
No comments:
Post a Comment