Na Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, ameelezea huzuni na masikitiko yake
kuomboleza kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mabunge ya Nchi za
Jumuia ya Madola (CPA), Dk. William Shija.
Dk. Shija aliyefariki dunia
Jumamosi asubuhi mjini London, Uingereza, ambacho ndicho kilikuwa kituo chake
cha kazi, alisomea na kuwa mhadhiri wa uandishi wa habari kabla ya kuwa Mbunge
wa Sengerema kwa miaka 15 mfululizo na Waziri Mwandamizi wa serikali katika
Wizara mbali mbali.
Katika salamu zake kwa
Sekretarieti ya CPA, Kanda ya Afrika, Rais Kikwete, alisema amestushwa na kifo
cha Dk. Shija ambacho kimeinyang’anya Afrika na dunia, na hasa Tanzania na
Jumuia ya Madola, mtumishi mwadilifu na mwaminifu, ambaye alitoa maisha yake
kwa utumishi wa umma.
“Alikuwa kiongozi mfano katika
nafasi zote za umma alizozishikilia. Aliifanya kazi yake ya uhadhiri wa
uandishi wa habari kwa ufanisi mkubwa na aliwapa utumishi uliotukuka wananchi
wake wa Sengerema katika nafasi yake ya Ubunge. Dk. Shija alitumainiwa katika
nafasi zote nyingi na za uandamizi za uwaziri wa serikali,” alisema.
“Nawatumieni salamu za dhati ya
moyo wangu kuomboleza kifo cha Dk. Shija na naungana nanyi katika kumlilia.
Kupitia kwenu, nawatumia wajumbe wote wa CPA na Sekretarieti ya Chama hicho
pole nyingi kwa kuondokewa na kiongozi na mtendaji wao mkuu. Aidha, naomba pia
mniwasilishie pole zangu kwa wana-Sengerema ambao Dk. Shija aliwatumikia kwa
uaminifu na kwa miaka mingi,”alisema.
No comments:
Post a Comment