Na Madina Issa
Watu watatu wamefariki dunia
katika matukio tofauti katika mkoa wa mjini magharibi, akiwemo mtoto mchanga
kutupwa katika ziwa la Mwantenga.
Kamanda wa Polisi mkoa wa mjini
magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, aliwataja marehemu hao kuwa ni Khamis Ali Ame
na Rajab Suleiman Salum (19).
Alisema marehemu Khamis Ali Ame
alikufa Oktoba 9 mwaka huu saa 2:00 asubuhi Shaurimoyo ambapo kifo chake
kilitokea baada ya kuanguka chini wakati akitembea kuelekea katika shughuli
zake za kawaida.
Alisema marehemu alifikishwa
hospital kuu ya Mnazimmoja kwa uchunguzi na baadae kukabidhiwa jamaa zake kwa
ajili ya mazishi.
Alisema tukio jengine limetokea
Oktoba 8 mwaka huu saa 2:00 asubuhi katika bahari ya Kizingo ambapo iliokotwa
maiti ya kijana aliyetambulika kwa jina la Rajab Suleiman Salum (19) mkaazi wa
Taveta.
Alisema kifo cha marehemu
kilisababishwa na kuzidiwa na maji alipokuwa akiogolea katika bahari hiyo.
Alisema mwili wa marehemu
ulifikishwa hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa uchunguzi na kupewa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.
Tukio jengine lilitokea Oktoba 6 mwaka huu saa 12:30
usiku Nyerere ambapo mtoto mchanga wa kike wa siku moja, alikutwa ameshafariki
dunia baada ya kutupwa katika ziwa la Mwantenga.
Alisema chanzo cha mtoto huyo
kutupwa bado hakijajulikana na jeshi la polisi linaendelea na upelelezi.
No comments:
Post a Comment