Na Laylat Khalfan
Shilingi milioni 41
zimepatikana baada ya Kitengo cha Usarifu na Masoko, kusafirisha tani 11 za
mwani kuanzia Julai 2013 hadi Juni 2014.
Mkurugenzi wa Idara ya mazao ya
baharini, Mohammed Sudi Mohamed, alisema fedha hizo zinaingia kwenye mfuko wa
hazina wa serikali.
Aidha alisema asilimia 80 ya
uzalishaji wa mwani unafanywa kisiwani Pemba kwa sababu watu wengi
wanajishughulisha zaidi na kilimo hicho wakiwemo wanaume.
Asilimia kubwa ya mwani
uliouzwa nje ni mwembamba ambao ingawa hauna
maslahi mazuri kwa wakulima lakini uzalishaji wake ni mkubwa duniani
kote.
Ofisa wa mwani kutoka kitengo
cha ukulima wa mwani Maruhubi, Hamisuu Maruzuk Yussuf, alisema kumekuwepo na
athari mbalimbali za uharibifu wa misitu kunaokosababishwa na ukataji wa miti
kwa ajili ya matumizi ya kilimo hicho.
Pia alisema kuna tatizo la
mmong’onyoko wa fukwe za baharini unaosababishwa na idadi kubwa ya watu
wanaopita kila siku katika eneo moja kwa ajili ya shughuli za upandaji mwani.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili
wakulima wa zao hilo, alisema kuwepo kwa bei ndogo ya mwani kunawafunja moyo
wakulima ikilinganishwa na kazi kubwa ya uoteshaji wa zao hilo.
No comments:
Post a Comment