Mwandishi wetu na mitandao
WAKATI Zanzibar ikichukua
juhudi kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauingii nchini kwa kuwapima abiria
wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege na bandarini, imebainika tiba ya
mgonjwa mmoja wa Ebola ni dola za Marekani 315,000 sawa na shilingi milioni
520.4.
Hata hivyo, hakuna dawa
mahasusi wala chanjo ya ugonjwa huo hatari ambao tayari umeanza kuingia nchini
Uganda baada ya mtu mmoja kufariki kwa kupatwa na virusi vya homa ya Marburg,
ambavyo vinashabihiana kwa sehemu kubwa na Ebola.
Badala yake madaktari katika
kliniki zinazowahudumia wagonjwa wa Ebola wanamsaidia mgonjwa kwa kumuongezea
maji, kupunguza shinikizo la damu, kumuwekea mashine ya oxygen, kumuongezea
damu na kutibu magonjwa mengine nyemelezi.
Uchunguzi uliofanywa na
mwandishi wa habari hizi kupitia vyombo vya habari vya kimataifa, umegundua
gharama kubwa za kuwatibu wagonjwa wa Ebola na upungufu wa wataalamu ni
miongoni mwa sababu zinazopelekea nchi za Afrika kushindwa kudhibiti ugonjwa
huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari
la Uingereza, Reuters, ugonjwa huo unaweza kudhoofisha uchumi wa Afrika kwa
sababu ya gharama kubwa za kuwatibu wagonjwa.
Shirika hilo limewanukuu
wanasayansi wakisema kuwa kuna hatari kubwa ya ugonjwa huo kusambaa katika
mataifa ya magharibi hasa Uingereza na Ufaransa kutokana na safari nyingi za
ndege zilizopo kati ya nchi hizo na mataifa yaliyoathiriwa na ugonjwa huo.
Shirika la Afya Duniani (WHO)
halijazuia safari za ndege katika mataifa yaliyoathiriwa na ugonjwa huo badala
yake imekuwa ikiyahamasisha mashirika ya ndege kuchukua tahadhari.
Mashirika ya Ndege ya Uingereza
na Emirates, yamesimamisha safari zake katika nchi za Afrika Magharibi zenye
visa vya Ebola.
No comments:
Post a Comment