HOTUBA YA UFUNGUZI WA WARSHA JUU YA UDHIBITI WA
UTAKASISHAJI WA FEDHA HARAMU KWA MAAFISA UPELELEZI KUTOKA JESHI LA POLISI NA
WAENDESHA MASHTAKA KUTOKA AFISI YA MKURUGENZI WA MASHTAKA ZANZIBAR TAREHE 12 –
13 NOVEMBA, 2014
Imetolewa na Mhe. Said Hassan Said
Mwanasheria Mkuu Zanzibar.
1.
Kaimu
Kamisha, kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu,
2.
Ndugu
Washiriki kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Jeshi la Polisi Zanzibar,
3.
Washiriki
wa Warsha,
Mabibi na Mabwana,
Assalamu Alaykum.
Kwanza,
sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa kila kitu, Mola wa utukufu wote
na mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya
leo kuhudhuria warsha hii muhimu tukiwa na amani, usalama na utulivu.
Natoa
shukrani zangu za dhati kwa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu kwa kuandaa
Warsha hii muhimu inayohusu Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu na
kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi.
Aidha, ninatoa shukrani kwa washiriki wote kwa jumla kwa kuitikia
mwaliko na kuhudhuria warsha hii muhimu na kuwa tayari kutoa michango yenu
ambayo ninaamini itaifanya nchi yetu iimarishe mfumo wa udhibiti wa
utakasishaji wa fedha haramu.
Ndugu
Washiriki, mabibi na mabwana,
Utakasishaji
wa fedha haramu (money laundering) ni mchakato (process) wa makusudi unaofanywa
na wahalifu katika jitihada za kuficha chanzo halisi cha pato linalotokana na
uhalifu (proceed of crime). Vitendo vya
uhalifu kama biashara haramu ya dawa za kulevya, rushwa, ujangili, ujambazi,
biashara haramu ya kuuza watu na viungo vya watu, uuzaji haramu wa silaha,
uharamia, ukwepaji wa kodi na kadhalika hufanywa na wahalifu kwa lengo la
kupata fedha.
Fedha
zinazopatikana kutokana na uhalifu mbalimbali ni fedha haramu ambazo watu
hutafuta namna ya kuzifanya zionekane kuwa ni halali. Mchakato wa kuzihalalisha fedha hizi
zionekane kuwa zinatokana na shughuli halali, ndio huitwa “Money Laundering”
yaani Utakasishaji wa Fedha Haramu.
Tatizo
la kuzitakasa fedha haramu lipo, kwa kuwa vitendo vya kihalifu vinavyowapatia
pato haramu wahalifu kama biashara
haramu ya dawa za kulevya, rushwa, ujangili, ujambazi, biashara ya watu
na viungo vya watu, uuzaji haramu wa silaha, kukwepa kulipa kodi na uharamia
bado vipo pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na Serikali ya kupambana na
wahalifu.
Ndugu
Washiriki, mabibi na mabwana,
Utakasishaji
wa Fedha Haramu ni tatizo kubwa ulimwenguni kote na katika jamii. Madhara yake kiuchumi, kijamii, kisiasa na
kiusalama ni makubwa sana ikiwa ni pamoja na yafuatayo:-
·
Kushusha hadhi ya nchi kimataifa (erosion of
country’s integrity) na kusababisha nchi kutonufaika na mfumo wa fedha wa
kimataifa,
·
Kushusha imani ya wawekezaji na kusababisha
uwekezaji kupungua na wawekezaji wapya kutotaka kuwekeza nchini. Kushamiri kwa uhalifu, wawekezaji huwa na
hofu kuwa mitaji na mali zao havitakuwa salama,
·
Kusababisha uhalifu kuendelea kushamiri kwani
wahalifu wataendelea kufanya uhalifu; na kuendelea kunufaika na pato litokanalo
na uhalifu.
·
Kushusha hadhi ya mfumo wa fedha wa nchi (erosion
of the integrity of the financial system).
·
Kuharibu ushindani (ruin competitiveness) wa
kibiashara kutokana na wahalifu kuwa na mitaji inayotokana na fedha haramu; na wafanya
biashara halali kushindwa kuhimili ushindani.
·
Kuhatarisha utawala wa Sheria na usalama (threaten
peace, stability and rule of law) pale uhalifu unaposhamiri. Makundi ya uhalifu yanapojiimarisha hupata
nguvu na kujaribu kudhibiti au kushindana na vyombo vya dola.
·
Imani ya washirika wa maendeleo na jumuiya ya
kimataifa hupungua na nchi huathirika kiuchumi.
Ndugu
washiriki, Mabibi na Mabwana,
Ni
dhahiri kuwa madhara niliyoainisha ni makubwa na yana athiri moja kwa moja
jitihada za nchi yetu kufikia malengo yake ya maendeleo.
Kwa
kuzingatia madhara makubwa ya utakasishaji wa fedha haramu, kiuchumi, kijamii,
kiusalama na kisiasa, nchi mbalimbali duniani zikiongozwa na dhamira ya
kukabiliana na uhalifu, makubaliano na mikataba ya Umoja wa Mataifa na itifaki
za kikanda (UN Conventions and regional protocols), zimekubaliana kuchukua
hatua mbalimbali za kupambana na utakasishaji wa fedha haramu. Kila nchi inatakiwa kuwa na mfumo wa kisheria
na wa kitaasisi (legal and institutional frame work) na kupambana na
utakasishaji wa fedha haramu.
Mfumo wa
kisheria ni pamoja na kutunga sheria zinazokidhi viwango vya kimataifa na
kuridhia mikataba ya kimataifa. Mfumo wa
kitaasisi ni pamoja na kuwa vyombo vya ushauri (advisory bodies) na vitengo vya
udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu (financial intelligence units) kwa
ajili ya kutekeleza sheria za kupambana na utakasishaji fedha haramu. Vitengo vya udhibiti wa utakasishaji wa fedha
haramu ni mihimili muhimu katika mfumo wowote imara wa kudhibiti utakasishaji
wa fedha haramu.
Ndugu
Washiriki,
Nchi
yetu kwa maana ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutambua kuwa tatizo la
utakasishaji wa fedha haramu linahitaji udhibiti ili kupunguza madhara yake
makubwa kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiusalama, ilitunga Sheria ya Udhibiti wa
Utakasishaji wa Fedha Haramu mnamo mwaka 2006 (The Anti- Money Laundering Act);
na kwa upande wa Zanzibar ilitunga Sheria ya Kudhibiti na Usafishaji wa Fedha
Haramu na Mapato ya Uhalifu Nam. 10 ya mwaka 2009 (The Anti- Money Laundering and
Proceeds of Crime Act) na hivyo kufanya utakasishaji wa fedha haramu kuwa ni
kosa la jinai pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndugu
Washiriki,
Nimeelezwa
kuwa katika warsha hii mtapata fursa ya kupitia masuala mbalimbali kuhusu utakasishaji
wa fedha haramu, mbinu wanazotumia wahalifu, hatua na jitihada mbalimbali
zinazochukuliwa na serikali mbalimbali na jumuiya ya kimataifa katika udhibiti
wa utakasishaji wa fedha haramu na mambo yanayohusiana nayo. Ni dhahiri kuwa mmepata fursa adhimu ya
kujadiliana na kueleweshana masuala haya muhimu ambayo kwa kiasi fulani ni
mapya. Ninaomba itumieni fursa hii kwa
umakini ili ilete tija kwenu binafsi na taifa kwa ujumla.
Ninaomba nisieleze kwa undani zaidi kuhusu
masuala haya, niwaachie wataalamu matakaokuwa nao siku mbili hizi. Labda, nisisitize kidogo umuhimu wa
ushirikiano katika kukabiliana na suala hili.
Ukweli kuwa tupo washiriki kutoka taasisi mbalimbali ni ishara na ujumbe
wa kutosha kuwa tunahitaji kushirikiana kwa karibu kiutendaji ili mapambano
haya yafanikiwe na kuinusuru nchi yetu dhidi ya uhalifu na hivyo kuiletea
maendeleo inayostahiki.
Ndugu
Washiriki, Mabibi na Mabwana,
Ninaomba
nikamilishe hotuba yangu kwa kueleza kuwa jitihada za Serikali za kupambana na
utakasishaji wa fedha haramu zinaonesha mafanikio makubwa sana, kwani uhalifu
unapungua nchini, wawekezaji wameendelea kuwa na imani na usalama wa mitaji na
mali zao, mfumo wetu wa fedha unaaminika na unazidi kukua, kuimarika na hakuna
makundi ya wahalifu yanayotishia utawala wa kisheria nchini. Hata hivyo tusibweteke na mafanikio hayo.
Serikali
itaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya utakasishaji wa
fedha haramu yanaendelea ili kuinusuru nchi yetu na madhara yake ambayo ni ya
kiuchumi, kisiasa, kiusalama na kijamii; na hata athari za kimataifa.
Ndugu
Washiriki, Mabibi na Mabwana,
Kwa mara nyingine tena ninawashukuru wote
walioandaa na kushiriki warsha hii muhimu na ninakutakieni uendeshaji na
usikivu mzuri. Matumaini yangu ni kuwa
mtashiriki vizuri; na taaluma mtakayoipata katika warsha hii mtaifanyia kazi na kuifikisha kwa wenzetu ambao tunafanya nao
kazi lakini hawakubahatika kuhudhuria warsha hii ili kuongeza mwangaza katika
jitihada za nchi yetu za kupambana na uhalifu.
Baada ya kusema hayo, sasa ninatamka kuwa Warsha
hii imefunguliwa rasmi.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment