Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika Yafanyika Jijini Dar-es-Salaam.Serikali Yasisitiza Uwazi katika Takwimu

Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa itaendelea kuwapatia wananchi takwimu sahihi zinazohusu sekta mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kushiriki katika ngazi za maamuzi na masuala mbalimbali nchini. 

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  Omar Yussuf  Mzee wakati akifungua rasmi maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yanaoongozwa na kauli mbiu isemayo Takwimu Huria kwa uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau wote.

Amesema upatikanaji wa taarifa na  takwimu sahihi kwa wananchi unaongeza ushiriki wao katika maamuzi na kuwajengea uwezo wa kutathmini utendaji wa Serikali katika masuala mbalimbali yakiwemo mapato na matumizi.

Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu itaendelea kuhakikisha kuwa takwimu mbalimbali zinapatikana kwa urahisi kupitia mtandao, machapisho na mifumo rahisi ili kuwawezesha wananchi na wadau mbalimbali kuzipata pindi wanapozihitaji.

“ Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika mwaka huu yanaongozwa na kauli Mbiu isemayo Takwimu Huria kwa uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau wote ambayo inalenga kurahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi kwa urahisi na kumwezesha mtumiaji kuzipata bila kizuizi chochote” Amesema.

Amefafanua  kuwa upatikanaji wa takwimu huria unawawezesha wananchi kujua sababu zinazoifanya serikali kutekeleza maamuzi mbalimbali, kuongeza uwajibikaji na kuwawezesha kupima matokeo ya sera za Serikali, kutathimini matumizi ya Serikali na kushiriki katika midahalo mbalimbali ya kitaifa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Aldegunda Kombo akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi hiyo amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika mwaka huu yameweka msisitizo katika kuweka miundombinu ya kuwarahisishia wadau kupata takwimu sahihi kwa wakati.

Amesema maadhimisho hayo licha ya kujadili masuala mbalimbali yanajikita katika kuweka msukumo wa kuhakikisha kuwa takwimu sahihi zinawafikia wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo bila vikwazo vyovyote ili kuongeza uwazi wa utendaji wa shughuli za serikali serikali.

Naye mwakilishi kutoka nchi washirika wa maendeleo Bw.Jacques Morisset akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ameeleza kuwa takwimu sahihi ni ufunguo wa maendeleo kwa nchi yoyote duniani.

Amesema kuwa upatikanaji wa taarifa mbalimbali unawawezesha wananchi kutambua na kupima kiwango cha maendeleo ya nchi yao katika masuala mbalimbali yanayogusa maisha yao ya kila siku yakiwemo ya matumizi ya rasilimali, Elimu, ukuaji wa uchumi, shughuli za kilimo na sekta ya viwanda na Biashara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.