STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
27.11.2014
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa katika Mpango wa Kukuza Uchumi na
Kuondoa Umasikini Zanzibar (MKUZA), sekta ya utalii ndio sekta mama na nyegine
zimekuwa zikiongeza nguvu hivyo inahitaji kuendelea kuungwa mkono ndani na nje
ya nchi.
Dk. Shein
aliyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Balozi mpya wa Tanzania nchini Canada Mhe.
Jack Mugendi Zoka, Ikulu mjini Zanzibar
aliyefika kwa ajili ya kuaga kwenda katika kituo chake kipya cha kazi nchini
humo kufuatia uteuzi wa Rais wa Jamhuri
ya Muuungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete hivi karibuni.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alimueleza Balozi huyo mpya wa Tanzania nchini Cadana kuwa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikifanyaa juhudi za makusudi katika
kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika na inaendelea kuwa sekta mama na muhimu
hapa nchini.
Dk. Shein
alisisitiza kuwa katika hatua ya uekezaji kwenye sekta ya utalii, serikali
imejikita zaidi na uekezaji kwenye ujenzi wa mahoteli ya kitalii kwa kuzingatia
kuwa ni miongoni mwa vivutio vikuu katika sekta hiyo ambayo imekuwa aikichangia
asilimia 80 ya fedha za kigeni hapa Zanzibar.
Alisema kuwa
kutokana na umuhimu huo hivi sasa hapa Zanzibar tayari kuna hoteli kadhaa za
daraja la kwanza huku bado serikali ikiendelea kuwakaribisha na kuwahamasisha wawekezaji
kutoka katika nchi mbali mbali duniani kuja kuekeza katika ujenzi wa hoteli za
kitalii hapa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein alitumiaa
fursa hiyo kumpongeza Balozi Zoka kwa kuteuliwa kuwa Balozi nchini humo na
kueleza kuwa Zanzibar na Canada zimekuwa
na mashirikiano makubwa hivyo, ipo haja ya kuyakuza na kuyaimarisha zaidi ili
kukuza uhusiano uliopo.
Akieleza juu ya
sekta ya uwekezaji Dk. Shein alimueleza Balozi Zoka kuwa mbali ya kutilia mkazo
uwekezaji katika ujenzi wa mahoteli pia, Serikali imekuwa ikitilia mkazo
uwekezaji katika Hospitali za kisasa za binafsi ambazo zinatibu maradhi maalum.
Akiyataja maradi
hayo, Dk. Shein alisema kuwa ni pamoja na maradi ya moyo, sukari, figo na
mengineyo ambayo bado huduma zake za tiba zinahitajika kwa kiasi kikubwa hapa
nchini, hivyo ipo haja kwa wawekezaji kutoka nchini Canada kuangalia fursa
hiyo.
Dk. Shein alisema
kuwa kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa la Canada (CIDA) , nchi
hiyo imeweza kuiunga mkono Zanzibar kwa kiasi kikubwa.
Akizungumzia
kuhusu nchi ya Cuba ambapo Balozi Zoka pia, ataiwakilisha Tanzania, Dk. Shein
alimueleza Balozi huyo kuwa nchi hiyo imekuwa na mahusiano ya kihistoria kati
yake na Zanzibar na kueleza kuwa ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuyatambua
Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12,
1964.
Dk. Shein
alimueleza Balozi Zoka haja ya kukuza uhusiano na ushirikiano na Cuba ambayo
Balozi Zoka pia, ataifanyia kazi kwani
ni nchi rafiki wa Zanzibar ambayo imeweza kuunga mkono juhudi za Serikali
katika kuimarisha sekta ya afya kwa kusaidia kuleta madaktari wakufunzi pamoja
na uanzishwaji wa Chuo cha Udaktari cha Zanzibar kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Matanzas
cha Cuba.
Nae Balozi mpya
wa Tanzania nchini Canada Mhe. Jack Mugendi Zoka alitoa pongezi kwa mafanikio
yaiopatikana hapa Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein katika kuimarisha
sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii.
Balozi Zoka
aliahidi kuwa atatumia fursa aliyoipata ya kuwawakilisha Watanzania wakiwemo
Wazanzibari nchini Canada sambamba na kuitangaza Zanzibar kiutalii kutokana na
vivutio vyake vilivyopo.
Aidha, Balozi
huyo alimueleza Dk. Shein kuwa ameweza kukutana na wadau wa sekta ya utalii
paamoja na uwekezaji wa hapa Zanzibar na kuweza kufanya nao mazungumzo pamoja
na kubadilishaja nae mawazo juu ya kuzifanyia kazi sekta hizo atakapokuwa
nchini humo ambao wameahidi kushirikiana nae kwa maslahi ya nchi.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment