
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
15.12.2014

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amelipongeza Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya ambazo zimeweza
kupata mafanikio makubwa na kuzidi kuijengea sifa ndani na nje ya nchi.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ukiongozwa
na Mwakilishi wa Shirika hilo nchini Rofaro Chatora aliyefika Ikulu mjini
Zanzibar kwa lengo la kumtambulisha Mwakilishi mpya wa Shirika hilo kwa upande
wa Zanzibar Dk. Andemichael Ghirmay Redae.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kumkaribisha Mwakilishi huyo mpya wa (WHO) nchini na kumueleza kuwa Shirika
hilo limekuwa na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na Zanzibar ambalo limeweza kutoa misaada mbali mbali
katika huduma za afya na elimu hapa nchini.
Dk. Shein alisema
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake imekuwa ikichukua juhudi
za makusudi katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika licha ya kuendelea
kuungwa mkono na Washirika wa maendeleo likiwemo shirika la (WHO).
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa Zanzibar inathamini sana misaada ya Shirika la (WHO) ambayo
imekuwa ikiitoa hapa Zanzibar kwa muda mrefu hatua ambayo imewezesha kupiga vita maradhi
mbali mbali yakiwemo Malaria, maambukizi ya virusi vya UKIMWI, vifo vya akina
mama na watoto na mengineyo.
Alisema kuwa
mbali ya juhudi hizo ongezeko la idadi ya watu hapa nchini pamoja na suala la
bajeti ni miongoni mwa changamoto ambazo serikali imekuwa ikikabiliana nalo ambapo
hata hivyo juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuimarisha
huduma za afya hapa nchini.
Kwa upande wa
kinga pamoja na matayarisho kwa maradhi ya kuambukiza kama vile Ebola, Dk.
Shein alisema kuwa Serikali itaendelea kuweka mikakati katika kutekeleza hatua hizo
ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuchukua hadhari juu ya ugonjwa
huo.
Nae Mwakilishi wa
Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Bwana Rofaro Chatora kwa upande wake, alimueleza
Dk. Shein kuwa Shirika hilo limejikita katika maeneo sita ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
malengo ya Milenia yanafikiwa katika sekta ya afya pamoja na kusukuma ama
kuchangia huduma za afya ili sekta hiyo izidi kuimarika.
Kwa maelezo ya
Mwakilishi huyo wa (WHO) nchini, eneo jengine ni kuendeleza huduma muhimu zikiwemo
bajeti kwenye sekta hiyo, kujihusisha zaidi katika kupiga vita maradhi
yasioambukiza ambayo hivi sasa yameshika kasi kwa kama vile maradhi ya moyo,
kisukari na mengineyo.
Aidha,
kuimarisha huduma za kijamii kama vile
maji safi na salama, makaazi mazuri sambamba na kujiweka tayari kwa kinga katika
kuyakabili maradhi mbali mbali ya kuambukiza kama vile ugonjwa wa Ebola ambao
umekuwa tishio hivi sasa.
Katika suala zima
la kujikinga na kujitayarisha na maradhi ya kuambukiza, Chatora alisema kuwa
umefika wakati kwa Zanzibar kuweka mikakati maalum katika kujikinga na maradhi
hayo.
Alieleza kuwa
licha ya kuwa ukanda huu wa Tanzania ikiwemo Zanzibar dalili za ugonjwa huo
ikifananishwa na maeneo ya Magharibi mwa
Afrika suala la kinga na matayarisho ya kuyakabili maradhi hayo ni jambo
lisiloepukika.
Mwakilishi huyo
alisisitiza kuwa katika hatua hiyo ya kujikinga na ugonjwa huo thakili si Wizara
ya Afya peke yake yenye jukumu la kupambana na ugonjwa huo bali ni jukumu
la Wizara zote zilizomo ndani ya Serikali zikashirikiana pamoja katika vita
hivyo.
Nae Mwakilishi mpya
wa Shirika hilo anaefanyia kazi zake Zanzibar Dk. Andemichael Ghirmay Redae amekiri
juhudi zinazochukuliwa na Zanzibar katika kuiamrisha huduma za afya na kueleza
haja ya kuimarisha mikakati huku akiahidi kutoa ushirikiano wake kwa upande
wake kwa kupitia Shirika la WHO analolifanyia kazi hapa Zanzibar.
Mwakilishi huyo
wa Zanzibar alieleza kuwa kuimarika kwa huduma za afya hapa Zanzibar ni suala
muhimu sana hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ni visiwa vya kitalii.
Mapema Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Saleh Mohammed Jidawi alieleza mashirikiano sambamba
na juhudi zinazochukuliwa na Shrikala (WHO) hapa Zanzibar katika kuunga mkono
juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma za afya na za kijamii.
Kwa maelezo ya
Dk. Jidawi, miongozi mwa juhudi ambazo (WHO) imekuwa ikiendelea kuiunga mkono
Zanzibar ni pamoja na kusaida maabara ya afya ya umma kisiwani Pemba ambayo ni
kituo cha utafiti wa maradhi ya kuambukiza
pamoja na kuisaidia maabara ilioko katika Hospitali ya Mnazimmoja mjini
Unguja ili kuendelea kupata hadhi.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment