Na Fatma Kassim
Imebainika wazazi wengi
wanaofika hospitali ya Kivunge kujifungua wanapata watoto wafu kutokana na matumizi
ya kupindukia ya dawa za miti shamba.
Matumizi ya dawa hizo pia
wakati mwengine husababisha kuzaliwa watoto wakiwa na afya dhaifu na kupata
magonjwa ya kudumu.
Matatizo mengine ni kuongezeka
kasi ya uchungu kwa mjamzito na kusababisha mtoto kufia tumboni, kuzaliwa akiwa
amechunika ngozi, wakati mwengine husababisha kuchanika fuko la uzazi na baadae
mama hushuka kizazi.
Asha Haidar mwenye umri wa miaka 32 mkaazi wa Pitanazako wilaya ya kaskazini ‘A’ mkoa wa
kaskazini Unguja, alifikishwa hospitali ya Kivunge Disemba 6 na anasema
lipotoka nyumbani tayari alikuwa amepewa
dawa na mama yake kwa lengo la kukazisha uchungu ili akifika hospitali
ajifungue mara moja.
“Na dawa za miti shamba
nimeanza kutumia tangu ujauzito wangu una miezi minne na nimetumia dawa hizi
kwa lengo la kuondoa maumivu nnayoyapata tumboni pamoja na mtoto wangu awe na
afya njema na wakati nimeanza uchungu nikiwa nyumbani nimepewa dawa na uchungu
ulikuwa na kasi,” alisema.
Aidha alisema aliugua kwa siku
nzima bila kujifungua na siku ya pili kwa jitihada za madaktari alijifungua
mtoto akiwa tayari ameshafariki tumboni.
Mama wa Asha, Mwatima Ali,
alisema ni utamaduni wao kutumia dawa za asili kwa sababu zinaimarisha afya ya
mjamzito na wakati wa kujifungua hujifungua mara moja.
Dk. Khamis Hamad Ali, alisema jamii
katika mkoa huo imekuwa na hamasa ya matumizi ya dawa za miti shamba kwa
wajawazito tangu mimba ikiwa changa, tatizo linalosababisha kujifungua watoto
wakiwa wameshafariki.
“Jamii imekuwa na utamaduni wa
matumizi ya dawa za miti shamba ambapo matumizi yake kwa kiasi kikubwa
yanakiathiri kiumbe kikiwa tumboni na hatimaye kujifungua wakiwa wameshakufa,”
alisema.
Katika kubabiliana na tatizo
hilo, alibainisha kuwa wamekuwa wakiwaelimisha wajawazito athari za matumizi ya
dawa hizo kwa afya za watoto tangu wanapohudhuria kliniki athari za matumizi ya
dawa hizo.
Alisema wamekuwa wakiwaelimisha
wakunga wa jadi hasa kwenye mikutano ya afya za vijijini ambapo hutumia fursa
hiyo kuwaeleza athari za matumizi ya
dawa hizo pamoja na umuhimu wa mjazito kuzalia hospitalini na
wasiwazalishwe na wakunga wa jadi.
Alisema tangu Disemba 1 hadi 10
jumla ya watoto watatu wamezaliwa wakiwa wafu kutokana na matumizi ya dawa za
miti shamba.
No comments:
Post a Comment