Habari za Punde

Hotuba ya Balozi Seif ufungaji wa mkutano wa 18 Baraza la wawakilishi

HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR,
MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO
WA 18 WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR,
TAREHE 30 JANUARI, 2015
--------------------------------
                              

1.0            Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uhai, uzima na afya njema na kutuwezesha kukutana leo hii kukamilisha Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi ambao umejadili masuala mbali mbali kwa mustakbali wa nchi yetu na watu wake.  Aidha, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijaalia nchi yetu kubaki katika hali ya amani na utulivu. Pia, naomba kuchukua fursa hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa kuendelea kuliendesha Baraza letu kwa umahiri na mafaniko makubwa.  Uwezo wako, busara zako pamoja na hekima uliyonayo ndivyo vilivyouletea mkutano huu mafanikio hayo.
 
2.0            Mheshimiwa Spika, natoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa uongozi wake wa busara na hekima ambao umechangia sana katika maendeleo tunayoendelea kuyapata katika nchi yetu.  Mheshimiwa Dkt. Shein ameendelea kuwa mfano bora wa uongozi makini ambao sote tunatakiwa kuiga mfano huo katika nafasi zetu mbali mbali ili tuweze kuiletea maendeleo ya haraka nchi yetu.  Ndiyo maana amekuwa akisisitizia tuache kufanya kazi kwa mazoea (business as usual) ili tuweze kupiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo nchini mwetu.
 
3.0            Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuendelea kumsaidia na kumshauri kwa hekima Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na  kwa  mashirikiano yake mazuri kwa Ofisi yangu.
 
4.0            Mheshimiwa Spika, nawashukuru kwa dhati Waheshimiwa Mawaziri kwa kutoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali zilizotolewa na wajumbe na kujibu masuali kwa umakini, ufasaha na usahihi. Ni matumaini yangu kwamba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu na wananchi waliokuwa wakifuatilia kwa karibu zaidi mijadala ya mkutano huu wamefaidika na majibu na ufafanuzi uliotolewa na Waheshimiwa Mawaziri.
5.0            Mheshimiwa Spika, nawashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako Tukufu kwa umakini wao wa kuhoji na kuuliza maswali na kupata majibu na ufafanuzi juu ya utendaji wa shughuli za Serikali.  Vile vile, Waheshimiwa wamekuwa wakitoa maoni na maelekezo wakati wa kujadili Miswada inayowasilishwa hapa Barazani. Ni imani yangu kwamba, kufanya hivyo kutaimarisha utendaji wa Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi wetu.
 
6.0            Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa 18, jumla ya maswali ya msingi …… na maswali ya nyongeza ……. yaliulizwa na Waheshimiwa Wajumbe na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri.  Aidha, jumla ya Miswada Minne (4) ya Sheria imewasilishwa na kujadiliwa kwa kina hatimae kupitishwa na Baraza lako tukufu, ambayo ni:
 
i.   Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Sheria ya Kupunguza na Kukabiliana na Maafa Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
ii.   Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Taasisi ya Ulinzi ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar na Mambo Yanayohusiana na Hayo.
iii. Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu Nambari 2 ya mwaka 1996 na kuweka badala yake Masharti bora ya Kuhifadhi, Kulinda na Kusimamia Mazingira, Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
 
iv. Mswada wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Kuanzisha Tume ya Maadili ya Viongozi na Mambo Yanayohusiana na Hayo
 

7.0            Mheshimiwa Spika, Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Sheria ya Kupunguza na Kukabiliana na Maafa Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo, uliwasilishwa, kujadiliwa na hatimae kupitishwa katika Mkutano wa 18.  Mswada huu ulikusudiwa kuweka sheria mpya inayoweka mfumo wa kisheria katika shughuli za kukabiliana na maafa na mambo ambayo yataondosha mapungufu yanayoonekana katika sheria ya sasa. Aidha, Sheria hii mpya itawiana na Sera ya Kukabiliana na Maafa ya 2011 pamoja na Makubaliano na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa inayohusiana na masuala ya kukabiliana na maafa iliyoridhiwa na nchi yetu.
 
8.0            Mheshimiwa Spika, Serikali inawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wote kwa michango na maoni yao na inawahakikishia kuwa michango na maoni yao yamepokelewa na kuzingatiwa ipasavyo ili kuwa na sheria bora itakayoweza kukidhi mahitaji ya wakati huu katika kukabiliana na maafa.
 
9.0        Mheshimiwa Spika, Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Taasisi ya Ulinzi ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar na Mambo Yanayohusiana na Hayo. Mswada huu unapendekeza kuanzisha Shirika la Ulinzi ambalo litakuwa chini ya JKU.  Shirika hilo linalopendekezwa litakuwa Wakala wa Serikali na litafanya kazi za ulinzi.    Kwa ujumla michango, maoni pamoja na maelekezo ya Waheshimiwa Wajumbe yamepokelewa na kufanyiwa kazi katika kuboresha mswada huu.
 
10.0           Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu pia kuliwasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza Mswada wa Sheria ya Kuhifadhi, Kulinda na Kusimamia Mazingira, Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Mswada huu una lengo la kuondoa mapungufu yaliyopo katika utekelezaji wa Sheria ya sasa.  Aidha, Sheria hii itazingatia Sera ya Mazingira ya Mwaka 2013, Mazingatio maalum ya Kimataifa juu ya Usimamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi na uchimbaji wa mafuta na gesi  pamoja na Haja ya kutenganisha shughuli za kiutekelezaji na uzingatiaji wa Sheria (enforcement and compliance) na zile za usimamizi (governance).
 
11.0           Mheshimiwa Spika, Mswada mwengine uliowasilishwa na kujadiliwa ni Mswada wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Kuanzisha Tume ya Maadili ya Viongozi na Mambo Yanayohusiana na Hayo.  Madhumuni na sababu ya Mswada huu ni kupendekeza kutungwa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kuanzisha Tume ya Maadili ya Viongozi.  Baada ya kutungwa kwa Sheria ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Serikali imeamua kuwasilisha Mswada huu ambao utasimamia maadili ya viongozi wote hapa Zanzibar kama walivyotajwa katika Sheria hii.
 
12.0           Mheshimiwa Spika, sote tunaelewa kwamba kuwa na maadili kwa viongozi ni jambo la msingi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali popote ulimwenguni. Kuwepo kwa Sheria hii kutaiongezea heshima nchi yetu kwa kuimarisha misingi ya utawala bora na uwajibikaji kwa viongozi wa Serikali yetu. Ninaamini utekelezaji wa sheria hii utaleta matumaini mapya kwa wananchi katika upatikanaji wa huduma zilizo bora kupitia taasisi mbali mbali za Serikali.
 
13.0           Mheshimiwa Spika, Wajumbe wengi wa Baraza lako tukufu walikuwa na hofu na Mswada huu.  Niwahakikishie Wajumbe wako kuwa hakuna haja ya kuwa na hofu na Mswada huu kwani hauna madhara yoyote kwao, mradi wamekuwa waadilifu, waaminifu na wanatunza heshima zao kama viongozi.  Washike njia kuu, wasichepuke.  Wakichepuka, sheria hii ndipo itakapo wabana.
 
14.0           Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kutoa wito kwa viongozi wote kuisoma, kuifahamu na kuitekeleza ipasavyo Sheria hii ili iweze kuleta tija kwa jamii kama ilivyokusudiwa. Aidha, niwanasihi watendaji watakaopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa Sheria hii wawajibike ipasavyo katika kuhakikisha kuwa lengo na madhumuni ya kuanzishwa Sheria hii yanafikiwa.     
 
15.0         Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Januari, 2015 nchi yetu ilitimiza miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, jambo ambalo ni la kujivunia kwa Wazanzibari wote.  Kama ilivyo kawaida, sherehe hizo zilitanguliwa na shamra shamra mbali mbali ikiwemo uzinduzi wa miradi 35 ya maendeleo. Wakati wa kilele cha maadhimisho ya sherehe hizo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein aliwahutubia wananchi na kuainisha maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Saba.
 
16.0           Mheshimiwa Spika, katika hotuba hiyo, Mheshimiwa Rais alizungumzia maendeleo yaliyopatikana katika sekta zote zikiwemo Sekta ya Huduma za Jamii, Sekta ya Kiuchumi na Sekta za Uzalishaji.  Katika Sekta ya Huduma za Jamii hasa elimu, Mheshimiwa Rais alitangaza kufutwa kwa michango ya aina zote katika elimu ya msingi na ada za mitihani kwa elimu ya sekondari.  Tamko hilo lina umuhimu mkubwa kwa jamii kwani litawawezesha wananchi wetu kuwa na uhakika wa kupata elimu kama ilivyoasisiwa na Jemedari wa Mapinduzi yetu Matukufu, Mzee Abeid Amani Karume, ya kutaka kila Mzanzibari awe na fursa ya kupata elimu.
 
17.0         Mheshimiwa Spika, Sote Wazanzibari tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi huu wa kizalendo unaoijengea sifa nchi yetu na kuongeza imani kwa wananchi wetu na kutoa fursa kwa watoto wetu hasa wanaotokana na familia zenye kipato kidogo kupata haki yao ya msingi ya elimu.
 
18.0           Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Afya, Serikali inaendelea kusimamia na kuimarisha huduma za kinga na tiba katika hospitali na vituo mbali mbali vya afya Unguja na Pemba. Katika kuimarisha huduma za kinga Serikali imeendelea kuchukua juhudi za kukuza uelewa wa jamii juu ya kujikinga na maradhi mbali mbali.  Aidha, Serikali imeyafanyia matengenezo makubwa na kujenga majengo mengine mapya  ya hospitali zake pamoja na kuweka vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba.    Vile vile, katika kuimarisha hospitali ya Mnazimmoja Serikali imejenga Wodi ya Wagonjwa Mahatuti (ICU) ya kisasa, na Kitengo cha Huduma za Upasuaji wa Vichwa na Uti wa Mgongo (Neurosurgical Unit) na kuwekewa vifaa vyote muhimu na tayari vinafanya kazi ya kutoa huduma zilizokusudiwa.  Napenda kuwashukuru sana wahisani wetu katika maendeleo kwa msaada wao mkubwa waliotupatia katika kuimarisha huduma hii muhimu ya afya.
 
19.0         Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Serikali imechukua jitihada maalum za kuongeza madaktari na wahudumu wengine wa afya ili kukidhi mahitaji ya kitabibu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.  Hivi sasa jumla ya Madaktari Bingwa kumi na mbili (12) wa fani mbali mbali wako masomoni na miezi michache iliyopita tumeshuhudia madaktari 37 wa Chuo cha Udaktari Zanzibar (Zanzibar Medical School) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Matanzas cha Cuba wakihitimu masomo yao ya Shahada ya kwanza na tayari wameshaanza kufanya kazi. Pia tutaendelea kushirikiana na nchi marafiki katika kutupatia madaktari bingwa wa maradhi mbali mbali pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa madaktari wetu.  Hivi sasa tunao madaktari wapatao 40 kutoka Jamhuri ya Watu wa China na Cuba ambao wanaendelea kutoa huduma katika Hospitali zetu.  Napenda kuzishukuru nchi za China na Cuba kwa misaada yao hiyo.
 
20.0         Mheshimiwa Spika, suala la udhalilishaji wa kijinsia bado ni changamoto katika nchi yetu, kwani pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa za kudhibiti vitendo hivyo viovu bado wapo watu miongoni mwetu wanaoendeleza vitendo hivyo.  Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzidisha mapambano dhidi ya waovu hao. Watu hawa wamo miongoni mwetu na tunaishi nao.  Viongozi na wananchi kwa pamoja tuwafichue na kuwafikisha katika vyombo vya sheria bila ya kuoneana muhali kwani watu hao wanavunja utu na heshima ya wenzao na kuwasababishia madhara makubwa kimwili na kisaikolojia.  Aidha, natoa wito kwa wale wote wenye taarifa kutosita kufika Mahakamani kutoa ushahidi pale wanapohitajika na kuacha kabisa suala la kumaliza kesi hizi majumbani.
 
21.0         Mheshimiwa Spika, sekta ya kilimo bado ni tegemeo la wananchi wengi katika kujipatia ajira, kipato, chakula na kuimarisha lishe na afya zao. Kwa kuelewa hali hii, Serikali inaendelea kutoa msukumo mkubwa kuisaidia sekta hii na kuwasaidia wakulima ili waweze kuongeza tija na uzalishaji na hivyo kuimarisha vipato vyao.
 
22.0       Mheshimiwa Spika, kilimo cha mpunga katika msimu huu wa 2014/2015 kimeanza na kinaendelea vyema.  Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Maliasili imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kwamba huduma za kilimo cha matrekta na pembejeo nyengine zinapatikana kwa uhakika na kwa bei nafuu ambazo wakulima watazimudu.  Aidha, Serikali imeongeza kiwango cha upatikanaji wa mbegu bora ya mpunga, dawa ya magugu na mbolea kupitia Program ya Ruzuku Katika Kilimo cha Mpunga.
 
23.0       Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa wakulima wote wa zao la mpunga nchini kuungana na juhudi hizi za Serikali kutumia fursa ziliopo kuhakikisha wanalima kwa wakati na kufuata kanuni zote za kilimo bora, ikiwemo matumizi ya mbegu bora, matumizi sahihi ya mbolea na kuhudumia mashamba yao kwa kufanya palizi za mapema ili azma ya Serikali ya kuongeza uzalishaji wa zao hili iweze kufikiwa.  Sambamba na hili, Serikali inawahimiza wakulima wote wa mazao mengine kuchukua juhudi stahiki kwa kufuata ushauri wa Mabibi na Mabwana Shamba ili nao waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao.
 
24.0       Mheshimiwa Spika, Sekta ya utalii imeendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Takwimu zinaonyesha kwamba  mchango wa  sekta hii katika Pato la Taifa umefikia zaidi ya asilimia 27.  Sekta hii vile vile imechangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa ajira ambapo hadi mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2014 ilichangia kutoa ajira zisizokuwa za moja kwa moja zipatazo 60,000 na za moja kwa moja 22,884. Kutokana na mchango wa sekta hii katika maendeleo yetu, Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kitaasisi na kiuendeshaji ili kukidhi viwango vya kimataifa katika utoaji wa huduma za kitalii. Hii ikiwa ni pamoja na kuimarisha mashirikiano baina ya Serikali na Sekta binafsi zinazohudumia watalii.
 
25.0       Mheshimiwa Spika, ili Sekta hii izidi kukuwa na kuleta tija katika nchi yetu hatuna budi sote kwa pamoja Taasisi za Serikali, Sekta binafsi na wananchi kuzidi kushirikiana katika kuimarisha vivutio pamoja na miundombinu itakayowavutia watalii ikiwemo usafi na utunzaji wa mazingira, uwekezaji katika ujenzi wa hoteli zenye viwango bora na kudumisha amani na utulivu katika nchi yetu na kuhakikisha kwamba mapato yanayotokana na sekta hii yanakusanywa kikamilifu na kuingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
 
26.0       Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza dhana ya Utalii kwa wote, Serikali itazidi kuhamasisha wananchi kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango zitakazoweza kuingia katika soko la utalii na hivyo kuifanya sekta hii kuzidi kuwanufaisha wananchi. Hivi sasa wananchi wengi wamepata fursa ya kuuza bidhaa zao kwenye hoteli kadha, hali ambayo imeongeza upatikanaji wa soko la bidhaa wanazozalisha wananchi. Kwa azma hiyo hiyo ya kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta ya utalii, Serikali imefanya utafiti wa kuibua vivutio vipya vya utalii vilivyopo katika maeneo ya vijijini. Matokeo ya utafiti huo yatasambazwa kwa wananchi ili kuongeza uelewa wa fursa za sekta ya utalii zilizopo katika maeneo yao. Utekelezaji wa mpango huu unakadiriwa kutoa ajira za moja kwa moja zaidi kwa wananchi hasa wa vijijini. Aidha, sekta zinazohusika zinaagizwa kuandaa na kutekeleza mipango itakayoamsha ari ya wananchi kupenda kutembelea maeneo yenye vivutio vya utalii ili kukuza utalii wa ndani.
 
Hata hivyo, kuiimarisha sekta hii  hatuna budi sote kuwa wadau wa kudumisha amani na utulivu nchini.  Bila ya amani na utulivu hakuna mtalii atakayekuja nchini mwetu kwani atahofia usalama wake.
 
27.0     Mheshimiwa Spika, Sekta ya Miundombinu ya Usafirishaji ni muhimu sana katika ustawi wa nchi yetu. Kwa hapa kwetu miundombinu hiyo inajumuisha barabara, bandari na viwanja vya ndege. Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta hii ili kuhakikisha wananchi na hata wageni wanapata huduma bora za usafiri na usafirishaji wa bidhaa zao kutoka eneo moja hadi jengine.  Kama sote tulivyoshuhudia katika kuadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu miradi mbali mbali ya miundombuni ilizinduliwa ikiwemo barabara za mjini na vijijini, uimarishaji wa viwanja vya ndege na kuimarisha huduma za usafiri wa baharini. Haya yote yanafanyika katika kuendeleza azma ya Serikali ya kuimarisha uchumi na kupunguza umasikini.  Serikali itaendelea na hatua za kuimarisha miundombinu ya usafiri Unguja na Pemba kadri hali yetu ya uchumi itakavyoruhusu.
 
28.0     Mheshimiwa Spika, suala la utoaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi  limekuwa na     mjadala mkubwa ndani ya Baraza lako tukufu, kwani kuna baadhi ya Waheshimiwa Wawakilishi wamekuwa wakilalamika juu ya baadhi ya wananchi wao kutokupatiwa vitambulisho hivyo kwa sababu mbali mbali. Naomba ieleweke kuwa, Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi vinatolewa kwa mujibu wa  sheria Na. 7 ya mwaka 2005.   Hivyo,  mlengwa ni lazima atimize matakwa ya sheria hiyo kabla ya kupatiwa vitambulisho.   Matakwa hayo ni pamoja na kuwa Mzanzibari wa kuzaliwa au, mwananchi kukaa katika eneo lake si chini ya miezi 36 mfululizo na ambae ametimiza umri wa miaka 18.
 
29.0     Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 13 (1) (2) cha Sheria hiyo kimetoa haki kwa mtu yeyote kukata rufaa kwa Mkurugenzi wa Vitambulisho dhidi ya Afisi ya Usajili na pindipo hakuridhika na uamuzi wa Mkurugenzi anaweza akakata rufaa kwa Mheshimiwa Waziri. Bado kama hajaridhika anaweza kukata rufaa Mahakama Kuu.
 
30.0     Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kuwa Waheshimiwa Wawakilishi na Wanasiasa na wananchi hatuna sababu ya kulalamikia jambo ambalo lina utaratibu mzuri wa kisheria. Suala zima la upatikanaji wa vitambulisho tusilihusishe na siasa kwani suala hili lina utaratibu wake wa kisheria.  Ni wajibu wetu kutumia sheria hiyo katika kutafuta haki zetu.
 
31.0     Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu hivi karibuni nchi yetu imekamilisha zoezi la kupata Katiba Inayopendekezwa.  Kwa mara nyengine tena napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa pongezi zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha na kusimamia kwa umakini mkubwa mchakato mzima wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi kufikia kupata Katiba Inayopendekezwa. Aidha, nawapongeza kwa dhati kabisa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti  pamoja na Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa ushiriki wao na kazi kubwa waliyofanya iliyopelekea kumalizika kwa zoezi hilo kwa mafanikio makubwa. Ni wajibu wa Viongozi na wananchi sote kuisoma na kuielewa Katiba hiyo ili hatimae tuweze kushiriki kikamilifu katika hatua ya kuipigia kura ya maoni Katiba hiyo inayopendekezwa wakati utakapofika.
 
32.0      Mheshimiwa Spika, Kama ilivyokwisha tangazwa  kuwa ifikapo mwezi Aprili 2015 nchi yetu itakuwa na zoezi la upigaji wa kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Nawasihi wananchi wote na kwa kila anaepaswa na mwenye haki ya kupiga kura hiyo ni wajibu wake kwenda kupiga kura.  Utaratibu maalum utapangwa ili kila mmoja atumie haki na fursa hiyo bila bughudha. Natoa wito kwenu tuitumie fursa hiyo bila ya mikwaruzano ili kulimaliza zoezi hilo la kihistoria kwa utulivu mkubwa na maelewano.
 
33.0      Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena naomba kukushukuru kwa dhati kabisa wewe binafsi kwa kazi kubwa unayoifanya ya kuliendesha Baraza letu kwa umakini mkubwa.  Vile vile, nawashukuru Naibu Spika, Wenyeviti wa Baraza na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu kwa kutekeleza majukumu yao vyema.  Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa ushiriki wao mzuri katika mkutano huu wa 18 ambao umemalizika salama na kwa mafanikio makubwa. Nawashukuru watendaji wote wa Serikali wakiongozwa na Makatibu Wakuu kwa juhudi zao za kuliwezesha Baraza kuendesha shughuli zake.  Namshukuru pia Katibu wa Baraza la Wawakilishi na wafanyakazi wote wa Baraza hili kama kawaida yao kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huu.  Nawashukuru Wanahabari wote na Wakalimani wa alama kwa kazi nzuri wanazozifanya za kuwaelewesha wananchi yanayotokea katika Baraza hili.  Nawatakia Wajumbe wote kurudi katika sehemu zetu za kazi kwa salama na amani na pia turejee Majimboni mwetu kwenda kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuwaletea maendeleo na kuiletea maendeleo nchi yetu.  Mwisho nawatakia heri na baraka za mwaka mpya wa 2015.
 
34.0               Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa heshima naomba kutoa hoja ya kuliahirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano tarehe 11 Machi, 2015 saa 3.00 barabara za asubuhi.
 

35.0               Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.