STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
9.1.2015

SERIKALI ya
Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuhakikisha huduma za afya
zinaimarika licha ya ongezeko la idadi ya watu hapa Zanzibar ikilinganishwa na idadi iliyopo
kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo
mara baada ya kulifungua jengo jipya la upasuaji wa maradhi ya ubongo na uti wa mgongo lililopo hapo katika hospitali Kuu
ya Mnazimmoja mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za maadhimisho
ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Shein alisema
kuwa kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 idadi ya watu wa Zanzibar
ilikuwa ni laki tatu na ishirini ambapo
idadi hiyo imeongezeka mara nne ya wananchi wanaoishi Zanzibar ambao wanafika
milioni 1.4 hivi sasa jambo ambalo limepelekea utoaji wa huduma uwe tofauti na mara
baada ya Mapinduzi.
Alisema kuwa azma
ya Hospitali ya Manazimmoja kuwa ya rufaa ni ya muda mrefu wazo ambalo limeanza
yeye akiwa Naibu Waziri wa Afya na ndipo mchakato ukaanzia hapo na kupita
katika vipindi mbali mbali vigumu na hata hivyo mafanikio yameanza kuonekana.
Dk. Shein alisema
kuwa kuandaa mpango madhubuti katika kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa ya
rufaa ni jambo ambalo hupelekea mabadiliko makubwa ya mfumo wote wa hospitali
ili uende sambamba na utoaji wa huduma za afya.
Katika hotuba
yake hiyo Dk. Shein pia, alisikitishwa na baadhi ya viongozi ndani ya Mawizara
ya Serikali kuwazuia watendaji wao kujiendeleza na masomo kwa lengo la kupata
utaalamu zaidi ili kuiedeleza nchi yao.
Alisema kuwa
kufanya hivyo kunaviza maendeleo ya nchi kwani lengo la serikali ni kupata
wataalamu zaidi na iwapo wao wameshinda kazi hizo waiachie Serikali kwani
Serikali inathamini na inatambua umuhimu wa kuwapa elimu watendaji wake na iko
tayari kuwasaidia kwa hilo.
Alisema kuwa
jitihada zinahitajika hasa kwa kuhakikisha uongozi bora unapatikana katika
kuendesha huduma hizo katika hospitali hiyo kwani matarajio ni kuja kwa
wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali zilizokuwepo jirani na Zanzibar kwa kutambua
kuwa kitengo hicho ni pekee katika ukanda huu wa bara la Afrika.
Dk. Shein alisema
kuwa sambamba na kuanza kwa tiba ya maradhi hayo pia, Serikali imeamua kwa
makusudi kuimarisha huduma za kinga na tiba ikiwa na malengo la kuanzisha
kitengo cha kushughulikia maradhi yanayotokana na matatizo ya figo, maradhi ya
moyo, saratani pamoja na huduma nyengine.
Alisema kuwa
kitengo hicho kitakuwa chuo cha kutoa mafunzo kwa vijana wa ndani na nje ya
nchi na kuwasisitiza madaktari kutambua kuwa hivi sasa kuna mabadiliko
makubwa katika kuleta maendeleo hasa
katika huduma za afya.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa ukitaka kuwahudumia wagonjwa vizuri ni lazima huduma za uchunguzi
zifanywe vizuri huku akieleza matumaini ya kitengo cha uchunguzi wa maradhi cha
hospitali ya Mnazimmoja kupata cheti maalum cha ubora kutoka kwa taasisi
husika.
Dk. Shein
alieleza kufarajika kwake kwa ongezeko la madaktari hapa Zanzibar hivi sasa na
kusisitiza kuwa lengo kubwa hivi sasa ni kuongeza madaktari bingwa ili kuongeza
kutoa huduma za bora kwa wananchi sambamba na kuipa hadhi Hospitali hiyo ya
Mnazimmoja kuwa ya rufaa.
Alisisitiza kuwa
hospitali hiyo ni lazima ijiendeshe wenyewe
na kuitaka Wizara kuhakikisha kabla ya kikao cha tatu cha Baraza la
Wawakilishi Sheria itakayosimamia uendeshaji wa hospitali ya Mnazimmoja iwe tayari kwani uwezo wa kujiendesha wenyewe upo na
kutoa miezi miwili kuhakikisha Sheria hiyo inakuwa tayari.
Alisema kuwa
kuwepo kwa sheria na kanuni katika hospitali hiyo kutasaidia kuendesha
hospitali hiyo na kuondosha mchanganyiko wa mambo kwa.
Dk. Shein alisema
kuwa lengo la serikali kwa muda mfupi ujao ni kuhakikisha kuwepo kwa ‘E-
Health’ ‘E-Education’ na mchakato wake
umekuwa ukiendelea na kueleza kuwa mtandao wa mawasiliano utasaidia kwa kiasi
kikubwa kwani hizo zote ni kazi za pamoja kati ya wananchi na serikali kwani
lengo ni kupata wataalamu zaidi.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Profesa Mahmoud Kuresh akiwa
mwakilishi wa Taasisi ya elimu ya maradhi ya ubongo na uti wa mgongo ‘NED’ kwa
kuunga mkonno katika kuhakikisha kitengo hicho cha upasuaji kinajengwa hapa
Zanzibar na kuweza kutoa huduma
Nae Waziri wa
Afya Mhe. Rashid Seif alisema kuwa ndani ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuna mambo maendeleo mengi ya kujivunia na kutoa pongezi kwa washirika wa
maendeleo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Nae Profesa
Mahmoud alieleza juhudi zilizochukuliwa katika kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo
unafanikiwa pamoja na kupatikana kwa vifaa vyake huku akieleza kuwa kuwepo kwa
huduma hizo hapa Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa huduma za
afya na kuijengea sifa Zanzibar katika ukanda huu wa bara la Afrika.
Alisema kuwa
kituo hicho ni cha pekee katika ukanda huu na kusema kuwa huduma za mafunzo
nazo zitatolewa ili kuhakikisha Zanzibar inapata wataalamu wazalendo wa kufanya
pasuaji hizo.
Profesa Mahmoud
alisema kuwa uanzishwaji wa kituo hicho ilikuwa ni ndoto ya muda mrefu lakini
hivi sasa tayari kituo hicho kimeshaanza kufanya kazi na tayari kimeshaaza
kufanya upasuaji kwa wagonjwa wa maradhi hayo hapa nchini.
Profesa Mahmoud
ambaye alikuja hapa nchini akiwa na madaktari bingwa kutoka Spain na Marekani kwa
ajili ya kufanya upasuaji kwa watoto wenye maradhi ya vicha maji na baada ya
kuwafanyia watoto wengi ambao walikuwa zaidi ya 30 ndipo akaona haja ya kuwepo
huduma hizo hapa nchini na ndipo alipoanza mcahkato kwa kuashirikiana na
madaktari wenzake hao.
Nae Mkurugenzi
Mkuu wa Hospitali ya Mnazimmoja Dk. Jamala Taibu alitoa pongezi kwa Taasisi ya
NED pamoja na juhudi za Dk. Shein katika kuhakikisha kada ya afya inapata
wataalamu pamoja na madaktari bingwa ili kuimarisha sekta ya afya hapa nchini.
Mapema Dk. Mohamed Saleh Jidawi alisema kuwa zaidi ya
Tsh. Milioni 600 zimetumika katika ujenzi wa jengo hilo lenye vyumba viwili vya
operesheni, wodi nne, ukumbi wa mikutano pamoja na sehemu nyengine ambapo kwa
upande wa vifaa vyote vimetolewa kwa msaada na NED
Alisema kuwa
madaktari hao kutoka Spain ambao walikuja kutoa huduma hizo za watoto wenye
vicha maji mnamo mwaka 2004 na kuwafanyia upasuaji watoto 580 kati ya watoto
2623 waliofanyiwa uchunguzi na kusema kuwa hatua hiyo imesaidia kwa kiasi
kikubwa kuokoa fedha za Serikali kwani kama si upasuaji huo ingelibidi
wapelekwe nje ya nchi na kutumia fedha nyingi.
Aidha alisema
kuwa katika ujenzi huo Serikali imechangia asilimi 40 na asilimi 60 zimetolewa
na taasisi hiyo ya NED. Aidha, alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya RANS
ya hapa Zanzibar iliyoshinda tenda na hatimae kujenga jengo hilo jipya la
kisasa.
Katika ufunguzi
huo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad,
Mawaziri, Manaibu Waziri, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wawakilishi
wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Wafanyakazi wa Wizara ya Afya na viongozi
wengine wa Serikali na wananchi.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment