Habari za Punde

Wananchi Wamekuwa Wagumu Kufahamu Sheria.

Na Miza Kona. Maelezo. 
Wananchi wametakiwa kuwa na mwamko wa kuisoma sheria ili waweze kuijua na kupata haki zao pamoja na kuepukana na vitendo mbali mbali vinavyokwenda kinyume na sheria.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Huduma za Sheria Bi Harusi Miraji Mpatani wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Migombani Zanzibar.

Amesema wananchi wamekuwa ni wagumu wa  kufuata sheria kutokana na uelewa mdogo waliokuwa nao wa kutojua haki zao za msingi jambo linalopelekea kwenda kinyume na sheria hizo pamoja na kuwepo kwa kesi nyingi zikiwemo za udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Amesema kituo cha Huduma za Sheria kipo kwa ajili ya kuwasaidia Wazanzibar kuweza kuelewa na kujua haki zao pamoja na masuala ya sheria na haki za binadamu kwa kuwapatia elimu sahihi na ufafanuzi wa sheria hizo.

Amefahamisha kuwa kituo pia kinatoa msaada wa sheria na huduma kwa wananchi wasiojiweza wakiwemo Walemavu, Masikini ,Wanawake na Watoto pamoja na kuwaelimisha wananchi na kutatua migogoro.

“Elimu ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto inaendelea kutolewa lakini bado vitendo hivyo vinazidi kuongezeka vijijini hivyo jamii iwe na mwamko wa kuwafichua na kuwachukulia hatua wale wote wanaofanya vitendo hivyo”, ameeleza Mkurugenzi huyo.


Akizungumzia kuhusu ucheleweshaji wa kesi mahakani Mkurugenzi huyo amesema kuwa kuna kesi nyingi mahakamani ambazo bado hazijatolewa hukumu kutokana na kukwama  kwa kesi hizo mahakamni hapo na nyengine kukosa ushahidi hivyo kituo kinafuatilia tatizo hilo kwa wahusika na kulitafutia ufumbuzi.

Ameeleza kituo kina miradi miwili inayosimamia haki za watoto katika Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya Maghariri Unguja chini ya ufadhili ya Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Save The Children ambayo inapinga unyanyasaji wa watoto na kusimamia haki za binadamu.

Bi Harusi amefahamisha kuongezeka kwa watumiaji wa kituo hicho ni faraja kubwa ambayo inapelekea kupata matumaini mazuri ya maendeleo ya utoaji wa huduma za kituo kwani katika mwaka 2013 wateja waliofika kituoni hapo ni 3000 lakini kwa mwaka jana zaidi ya wateja 4000 walifika kupata huduma katika kituo hicho.

Aidha Bi Harusi amewataka wananchi kufuatilia Katiba iliyopendekezwa ili waweze kuielewa na kufanya maamuzi sahihi wakati ukifika pamoja na kutumia kituo hicho cha sheria kwani kinatoa huduma zake bure ili kuwasaidia wananchi kupata haki zao.


Kituo cha Huduma za Sheria kinatarajia kuazimisha miaka 23 tangu kuanzishwa kwake na kauli mbiu ni “Kutojua Sheria Sio Kukaa kimya”.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.