Na Zuhura Juma, PEMBA
WANAUSHIRIKA wa kikundi cha ufugaji wa nyuki cha ‘Tuungane
Cooperative’, kiliopo katika Shehia ya Tumbe Magharibi Wilaya ya Micheweni
Pemba, wameiomba Serikali kuwapatia mashine ya kukamulia Asali, ili iweze
kufikia kiwango.
Walisema kuwa
kuendelea kukamua kwa mikono ni jambo ambalo linawapa ugumu wa kuendeleza
ufugaji huo, kwani haifikii kiwango kinachotakiwa.
Wakizungumza na Mwandishi
wa habari hizi kijijini kwao walisema ili kuweza kutoa Asali yenye kiwango, ni vyema
Serikali kuwatafutia mashine ya kukamulia na kuacha kutumia mikono yao.
Katibu wa kikundi
hicho, Mbarouk Juma Mbarouk, alisema kuwa Asali inapokamuliwa kwa kutumia mikono,
inakuwa ni rahisi kuharibika, jambo ambalo si katika malengo yao.
“Malengo yetu ni
kukamua Asali yenye kiwango, ili idumu kwa muda mrefu, kwani kitu chochote unachotumia
mikono ni rahisi kuharibika”, alisema Katibu huyo.
Nae, Mwenyekiti wa
Kikundi hicho, Massoud Salim Said, alieleza kuwa lengo la Ufugaji huo ni kupunguza Umasikini
katiaka jamii, ingawa wanakwama kutokana na kutokuwepo kwa msukumo katika
vikundi vyao.
“Ili kuweza
kujikwamua na Umasikini, Serikeli hainabudi kutupa msukumo kwa vikundi vya Ushirika,
ambavyo vijana wengi tumejikita huko”, alieleza Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wa Mshika
fedha, Moza Mwazanije Hamad, alisema changamoto nyengine ambayo hurejesha nyuma ufugaji huo ni ukosefu
wa Soko, jambo ambalo hutumia Soko la ndani zaidi kuuza bidhaa hiyo.
“Tunatumia Soko la
ndani kuuzia bidhaa hii, kazi ngumu kipato kidogo kwani vifaa vinavyotumika
kufanyia Asali, vyote tunanunua”, alieleza Mshika fedha.
Aliiomba Serikali
kuwapatia kipima Asali, ili kuweza kujua kiwango kilichofikia kila baada ya
muda kabla ya kuvunwa kwa Asali hiyo.
“Huwa hatujui kama
ishapea au la, hivyo tukipata kipima Asali itakuwa kila baada ya muda tunaipima
na itakuwa tunaivuna kwa kupea kabisa”, alisema.
Mjumbe wa kikundi
hicho, Siwajibu Massoud Faki, alieleza kuwa kuna maadui ambao huingia katika Masanduku
ya Ufugaji huo, jambo ambalo hupelekea kuharibika kwa Asali yao.
“Tuna maadui kama Sisimizi,
Koyokoyo pamoja na Panya ambao huingia
kwenye Masanduku na kutuharibia, hivyo tunaiomba Serikali itupatie dawa”,
alieleza mjumbe huyo.
Alisema ili ufugaji huu uweze kukamilika, wanahitaji
kuwa na Masanduku ambayo hugharimu Tshilingi 4,000/= kwa moja, Nta pamoja na
masufuria ambayo yote yanahitaji fedha, jambo ambalo ni kikwazo kikubwa kwao.
Kikundi cha
Tuungane Cooperative, kina wanachama 20 Wanawake
nane na Wanaume 12, ambapo kimeanzishwa mwaka 2011, kwa lengo la kujikwamua na Umasikini.
No comments:
Post a Comment