Na
Zuhura Juma, PEMBA
WAJASIRIAMALI
wa kikundi cha uzalishaji chumvi cha masumbuko salt, kiliopo Masota Wilaya ya
Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wameiomba Serekali, kuwasaidia vitendea kazi
pamoja na soko la uhakika la kuuzia bidhaa zao.
Wajasiriamali waliyaeleza hayo, wakati
walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, katika mashamba yao ya
utengenezaji wa Chumvi, Masota.
Walisema kuwa ukosefu wa mashine ya kuvutia
maji chumvi kutoka baharini hadi kwenye mabwawa yao ni tatizo kubwa
linalorudisha nyuma maendeleo ya biashara yao.
Walisema kuwa, pindi serikali
ikiwasaidia mashine hiyo, wataweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo, hususan kwa
wanachama wao, ambao biashara ya Chumvi ndio moja ya njia ya kuwapatia
maendeleo.
“ Maji yanapotoka huku juwa likiwa kali,
imekuwa ni tatizo kwetu, tukiwa na mashine ambayo tutakayoweza kuyavuta maji
hayo kutoka sehemu moja na kuyaleta katika mabwawa yetu, tutaweza kupunguza
ugumu wa tatizo letu”walisema wanaushirika hao.
Mkuu wa kikundi hicho, Hamad Omar Faki
alisema wamekuwa wakichukuwa muda mrefu katika kuifanya kazi hiyo ya chumvi,
kwa kutumia nguvu za mikono kwa kuyavuta maji ili yajae katika mashimo yao,
jambo ambalo huchukuwa muda mrefu.
‘Tunapata shida sana katika kufanya
chumvi hii, kwa sababu tunavuta maji kwa kutumia mikono yetu kwa hiyo
tunapoteza muda mrefu mpaka kuimaliza ‘ alieleza Mkuu huyo.
Nae fundi wa uzalishaji chumvi kutoka
katika ushirika huo, Said Shamata alisema ushirika wao umekuwa ukikosa hydrometer
ambayo hutumika kupimia maji hayo, wakati yanapokuwa katika mashimo hayo jambo
ambalo ni kikwazo kikubwa katika kutekeleza shughuli hiyo.
‘’Hydrometer ni muhimu sana kwetu kwa
sababu tunapima maji, ili tujue kiwango gani tumefikia na kuweza kuyachanganya
maji haya kwa kiwango kinachohitajika’’alisema.
Alisema kuwa ili chumvi iweze kuangusha
inatakiwa ifikie nukta ishirini na nne (24) ambazo zinapimwa kwa hydrometer na
inaweza kuchukuwa muda wa siku sita mpaka kufikia siku kumi na mbili kukamilika.
Kwa upande wake mshika fedha wa kikundi
hicho, Said Abdalla Faki alisema tokea kuanzishwa kikundi hicho ni mafanikio
madogo ambayo wanayapata kwa kutokuwepo kwa soko la uhakika la kuuzia chumvi
hiyo.
‘’Hatuna soko kama siku hizi chumvi polo
shilingi elfu sita kwa sababu jua kali na inakuwa elfu nane mpaka tisa kwa
kipindi cha mvua’’.alieleza mshika fedha.
Hata hivyo waliwataka wananchi
kujishuhulisha katika kazi mbali mbali za ujasiria mali, kwa kuachana na tabia
ya kukaa mitaani, kikundi cha Masumbuko Salt kilianzishwa mwaka 2009 kikiwa na
wanachama tisa, wanaume sita na wanawake watatu.
No comments:
Post a Comment