Na Zuhura Juma, PEMBA
WACHIMBAJI wa Matofali katika Kware
ya Uwandani, Wilaya ya Chakechake, wamesema kuwa wako hatarini kupoteza maisha yao
kutokana na Vumbi linalowaingia Vifuani na Machoni mwao, na
kuiomba Serikali kupitia Wizara husika kuwatafutia ajira mbadala, ili kuendeleza Maisha yao.
Kilio
hicho kilitolewa na wachimbaji hao, wakati walipokuwa wakizungumza na mwandishi
wa habari, machimboni kwao Uwandani-Pemba.
Walisema
kuwa kutokana na Vumbi hilo linalowaingia
vifuani mwao pamoja na machoni, imekuwa ni kikwazo kikubwa kwao kilichokuwa
hakina mtetezi.
Walifahamisha
kuwa kutokana na kukosa ajira mbadala
ambayo itawaepusha na madhara hayo, imewabidi kuendelea kufanya kazi hiyo, ili
kujikimu kimaisha na Watoto wao.
Mmoja
wa Wachimbaji hao, Juma Khamis Othman, mkaazi wa Vitongoji kibokoni, alisema
kuwa kazi hiyo wameianza kwa muda mrefu, ambayo huifanya kila siku, hivyo vumbi
hilo huwaingia sana na kuwaathiri kidogo kidogo.
“Tunakaa
hapa kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni, na wengine tupo kwa muda mrefu,
na vifua vinatuuma lakini hatuna la kufanya, kwa sababu tunataka kula na
watoto”, alifahamisha.
Alisema
kuwa, kutokana na ugumu wa maisha wanalazimika kuendelea kuchimba Matofali hayo,
ingawa wanaathirika Kiafya, hivyo wanaiomba Serikali kuwapatia ajira mbadala ili kuepukana
na athari hizo.
Nae,
Mbarouk Suleiman Omar, mkaazi wa Vitongoji Kisiwani Pemba, alisema kuwa Macho
yao pia huwauma pamoja na kutoka Machozi kila wakati, kutokana na kukosa Miwani
ambayo huvaliwa wakati wa uchimbaji.
“
Yaani ni dhiki tupu ya kuchimba Matofali, lakini hatuna la kufanya, kwani ikiwa
hatukufanya hivi basi hatuli wala watoto hawasomi”, alieleza Mbaruok.
Kwa
upande wake, Suleiman Omar Khalfan, mkaazi wa Vitongoji Kibokoni ,alisema ili Taifa liweze kuwa na Vijana wenye nguvu na
kuweza kulipeleka mbele, Serikali hainabudi kuwatafutia ajira, kwani kazi hiyo
hupoteza nguvu nyingi kwa Vijana hao.
“Kazi
tunayoifanya ni ya nguvu sana, itafikia kipindi tutakuwa hatuwezi na sisi tuna
watoto hali hii itapelekea Watoto
wasisome kwani itakuwa hatuna pesa za kuwahudumia na wao watafuata kuchimba
kama sisi”, alisema Mchimbaji huyo.
Wachimbaji
hao ambao huchimba matofali zaidi ya 5000 kwa mwezi, hiyo ni kutokana na ugumu
wa Ardhi katika sehemu ya uchimbaji, ambapo Tofali moja huuzwa kwa Tshilingi
400/=.
No comments:
Post a Comment