Habari za Punde

Balozi Seif Afanya ziara Jimboni Kwake

Mbunge wa Jimbo la Kitope akiwahimiza wanafunzi wa Madrasat Swalihina ya Kijiji cha Mkadini ndani ya Jimbo la Kitope kusoma kwa bidii ili baadaye waje kusaidia kikazi chao maadili mema.kushoto la Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi na Katibu wa CCM Jimbo la Kitope Nd. Khamis Khamis.
Fundi  wa uchimbaji Kisima Bwana Moh’d Mussa akitoa maelezo kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif mara baada ya kukizindua rasmi  Kisima cha Kijiji cha Muembe Majogoo kitakachotoa huduma za maji safi kwa wananchi wa Kijiji hicho.
Balozi Seif akimkabidhi zawadi Kiongozi wa Kikundi cha Karati cha Kijiji cha Mkadini mara baada ya kufanya onyesho lao wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji hicho.
Mmoja wa Wananchi wa Kijiji cha Muembe Majogoo aliyezunguukwa na wanawe akiwa na katiba inayopendekezwa akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif hayupo pichani wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho.(Picha na – OMPR – ZNZ.)


Na Othman Khamis OMPR.                                                                                                      
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Wana jamii wana wajibu na haki za  kuzitumia vizuri fursa zote zinazotolewa na washirika wa maendeleo katika kusogezewa mahitaji yao ya lazima zikiwemo huduma za Msingi.

Alisema wajibu wa wananchi utawapa hamasa washirika hao wa maendeleo katika kuongeza nguvu za misaada na hata mikopo nafuu kulingana na mazingira ya maeneo yanayolengwa.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzbar alisema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mkadini mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo jipya la Madrasatul Swalihina ya kijiji hicho iliyopata ufadhili wa washirika wa maendeleo ya Kijamii.

Alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye miradi mbali mbali ya iliyoanzishwa na jamii ambayo imepata ufadhili au mikopo kutoka kwa Taasisi na mashirika ya maendeleo ndani na nje ya Nchi.

Balozi Seif aliwahimiza wanafunzi wa madrasat Swalihin kujitahidi kusoma kwa bidii ili baadaye waje kutumia elimu hiyo kusaidia vizazi vyao na hata vile vijavyo katika kudumisha maadili mema.

Alifahamisha kwamba mafunzo ya dini yanayoongozwa katika misingi ya maadili wakati wote yamekuwa yakileta faida kubwa ndani ya jamii na kupelekea kuwa na kizazi kinachozingatia heshima na utii.

Balozi Seif aliwakumbusha walimu kuendelea kuhubiri mafundisho ya dini kama yanavyoagizwa katika misingi ya amani na upendo kwa lengo la kuwajengea maadili mema watoto wanaowafundisha.


Alisema tabia inayofanywa na baadhi ya walimu kupotosha watoto na hata jamii kwa visingizio visivyoeleweka imekuwa ikileta athari zinazoendelea kushuhudiwa na kila mtu hapa Nchini.

Akizungumza na wana CCM baada ya kukagua Majengo ya Matawi ya CCM ya Mkadini,Kitope B, Kitope A, Mbaleni na Muembe Majogoo na kukabidhi fedha pamoja na vifaa mbali mbali vya ujenzi  kwa ajili ya Matawi hayo Balozi Seif alisema Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba ina nguvu ya muda mrefu wa kuendesha mahitaji ya Watanzania endapo itapigiwa kura ya ndio.

Alisema wabunge wa Bunge Maalum waliotengeneza Katiba iliyopendekezwa wana haki ya kutembea kifua mbele kwa vile wamefanya kazi ya ziada kwa kuwapatia Wananchi  katiba ilioyobeba maslahi yote wanayohitaji kupatiwa Watanzania walio wengi.

Aliwakumbusha Wana CCM na Watanzania wote kwamba sura ya tatu katika Katiba iliyopendekezwa imeainisha jinsi matumizi ya Ardhi  yalivyotoa fursa ya kina kwa kila Mtanzania awe anatoka Bara au Zanzibar atakavyokuwa na uwezo wa kutumia ardhi popote alipo kwa mujibu wa taratibu zilivyowekwa.
Alisema sura hiyo imewekwa wazi ili kuwapa nafasi pana  Wazanzibari wanaokusudia kutumia ardhi iliyopo upande wa Tanzania Bara kwa shughuli za uchumi na kijamii kwa vile ardhi iliyopo Zanzibar haiwezi kukidhi mahitaji ya idadi ya wananchi waliopo hivi sasa.

Naye Mke wa Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi alisema zaidi ya shilingi Milioni Mia Mbili ya Hamsini { 250,000,000/- }  zilizotolewa na Mbunge wa Kitope tayari zimeshatumika katika ujenzi wa Matawi 20 yaliyomo ndani ya Jimbo hilo.

Mama Asha alisema gharama ya fedha zilizobakia katika kukamilishia kazi ndogo ndogo za ujenzi kwa baadhi ya majengo ya Matawi yaliyobakia inakadiriwa kufikia shilingi Milioni Nane.

Alisema ujenzi wa Ofisi hizo za Matawi ya Chama cha Mapinduzi ni miongoni mwa ahadi iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope wakati alipokuwa akiomba nafasi ya ubunge  katika kipindi cha pili cha Uongozi wake kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Alifahamisha kwamba lengo la ujenzi huo wa Matawi ya CCM ni kuhakikisha kwamba wakati wa kura ya maoni kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2015 wanachama wa Matawi yote ya Jimbo hilo wanafanya vikao vyao ndani ya ofisi zao mpya zenye hadhi kamili ya Chama chenyewe.

Katika ziara hiyo  Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope ambae pia ni  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alizindua kisima cha maji safi na salama kitakachohudumia Wananchi wa Kijiji cha Muembe Majogoo.

Balozi Seif aliwahakikishia wananchi wa Kijiji cha Muembe Majogoo kwamba Serikali kwa kushirikiana na Uongozi wa Jimbo hilo utajitahidi kutafuta mbinu za kupatikana kwa huduma za kudumu za maji safi ya Bomba.

Ujenzi wa Kisima hicho kilichogharamiwa na Balozi Seif kwa zaidi ya shilingi Milioni 3.6 chenye urefu wa Pima 10 umekuja kufuatia matatizo makubwa ya muda mrefu yaliyokuwa yakiwasumbuwa  wananchi hao ya kupata huduma za maji safi na salama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.