Habari za Punde

ZEC yaandaa Semina maalum juu ya matayarisho ya uchaguzi mkuu

Na Mwajuma Juma, Zanzibar
 
TUME ya Uchaguzi Zanzibar  imesema kuwa tayari imeshakamilisha kutunga sera ya jinsia na ushirikishwaji wa makundi maalumu ili kutoa fursa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki katika mchakato wa uchaguzi.
  
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Divisheni ya uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Bw. Idrisa Haji Jecha, katika semina ya siku moja kwa waandishi wa habari, wakati akitoa mada juu ya matayarisho ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ilioyofanyika huko Hoteli ya Zanzibar Beach Resort  visiwani Zanzibar.
  
Alisema kuwa mchakato wa sera hiyo umefanywa kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UNMWOMEN).
 
 Alisema kuwa sera hiyo ina lengo la kuhakikisha wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu wanashirikishwa kikamilifu katika masuala yote katika mchakato wa uchaguzi.
  
Alifahamisha kwamba tayari maelekezo washapata na itakuwa na dira nzuri hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu.
  
Sambamba na hilo alisema kuwa katika matayarisho hayo tume hiyo inatarajia kutoa matokeo ya mapitio ya majimbo  ya Uchaguzi ya  Zanzibar mwishoni mwa mwezi huu .


Alisema ZEC inatakiwa kufanya mapitio ya majimbo ya uchaguzi katika kipindi cha kila baada ya miaka minane hadi miaka 10 na kuchunguza idadi ya mipaka na majina ya majimbo hayo ambapo kazi hiyo imeanza mwezi Juni 2014.


Alisema kazi hiyo tayari imeshafanyika vizuri kwa ushirikiano mkubwa wa wadau wa uchaguzi kwa Unguja na Pemba namna ya mipaka ya majimbo.

Kuhusu uteuzi wa wagombea wa kiti cha urais wa Zanzibar, alisema wagombea wa baraza la wawakilishi na ugombea udiwani katika Serikali za mitaa utafanyika septembar 7 mwaha huu.

Mapema  Mkuu wa Divisheni ya Utawala ya Uendeshaji  ya tume ya uchaguzi Zanzibar Bw.  Saadun Khamis alisema tume  imejipanga vizuri kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu ili kuweza kuepusha malalamiko kutoka kwa wadau wa uchaguzi kuwa tume hiyo kutokuwa huru na haki.
Alisema kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika muundo wa tume ya uchaguzi ikiwemo wadau kutoridhika na muundo wa tume ya uchaguzi kwani imekuwa ikitiliwa mashaka na wadau wa uchaguzi, kutokana na kuwa muundo wa tume hiyo hautowi nafasi kwa asasi za kiraia ushauri juu ya uteuzi na badala yake unatoa nafasi hiyo kwa vyama vya siasa pekee.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.