Habari za Punde

Balozi Seif Afungua Mkutano wa 31 Jumuiya ya Serekali za Mitaa Tanzania.

 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiingia ndani ya Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere Jijini Dar es salaam kuufungua Mkutano wa 31 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania kwa niaba ya Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda.Kulia yake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Hawa Abdulrahman Ghasia na aliyeko nyuma ya Balozi ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa ambae pia ni Meya wa Jiji la Dar es salaam Dr. Didas Massaburi.
Balozi Seif akipatiwa maelezo ya jinsi Idara ya Bohari Kuu ya Taifa Tanzania inavyotekeleza majukumu yake kutoka kwa Meneja wa Taasisi hiyo Daudi Msasi wakati alipotembelea maonyesho kabla ya kuufungua Mkutano wa 31 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa.
Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki wa Benki ya NMB Bibi Domina Ferouz wa pili kutoka Kulia akimuelezea Balozi Seif mafanikio makubwa iliyoipata Benki hiyo katika kusaidia huduma za Kijamii Nchini Tanzania.
Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa ALAT ambae pia ni Meya wa Jiji la Dar es salaam Dr. Didas Massaburi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Hawa Abdulrahman Ghasia.
Balozi Seif akiufungua Mkutano wa 31 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania { ALAT } kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Jumiya ya Serikali za Mitaa Dr. Didas Mssaburi akilizindua rasmi Jarida la Jumuiya hiyo pamoja na Kitabu cha Utafiti.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa kutoka Halmashauri mbali mbali Nchini Tanzania wakiwa katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa Niaba ya Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa kutoka Halmashauri mbali mbali Nchini Tanzania wakiwa katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa Niaba ya Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda.(Picha na Hassan Issa OMPR)
Na Othman Khamis OMPR
Serikali za  Mitaa Nchini hazina budi kuhakikisha kwamba Wananchi wake wanatumia mbinu zitakazoongeza uzalishaji kwa kutumia zana bora za kilimo zitakazoambatana na mbegu na mbolea za asili ili kuisaidia Serikali kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2015.

Ni aibu kwa Serikali hizo kuwaacha wananchi wao kuendelea kuomba misaada ya chakula inapokuwa dhahiri kwamba maombi ya wananchi hao hayatokani na maafa.

Akiufungua Mkutano Mkuu wa 31 wa  Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania   { ALAT } hapo Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kwa niaba ya Waziri Mkuu Makamu wa Pili wa Rais nwa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali hizo lazima zihamasishe katika kuongeza bidi katika uzalishaji wa chakula na biashara.

Balozi Seif alisema ili kufikia na kuliwezesha Taifa kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kiashiria cha Pato la Taifa lazima kikue kwa asilimia Nane hadi Kumi na kukua huko iwe mfululizo kwa miaka isiyopunguwa 10 kuanzia sasa.

Alisema kitakacholiwezesha Taifa kufikia hatua hiyo ni uwepo wa uhakika wa chakula,kuweka wazi fursa za kiuchumi pamoja na afya bora, Serikali za Mitaa zikitambua wazi kwamba Kilimo, ufugaji, uvuvi, ufugaji nyuki na biashara ndogo ndogo ndio shughuli zinazogusa wananchi wengi walio katika Serikali hizo.

Balozi Seif ameipongeza Jumuiya ya Tawala za Mitaa kwa mafanikio makubwa iliyopata tokea kurejeshwa upya kwa Serikali za Mitaa Nchini Tanzania mwaka 1984

Alieleza kuwa Mkutano huo umefanyika wakati mzuri na muwafaka wa kujipima kiasi gani Jumuiya ya Serikali za Mitaa imeweza kusaidia Serikali za Mitaa kutimiza malengo na matarajio ya wananchi katika kujiletea maendeleo katika maeneo mbali mbali ya nchi.

Alisema Chama cha Mapinduzi muda wote kinaendelea kutoa sera na maelekezo kwa Serikali zote mbili katika kipindi chote cha Uongozi wake kupitia Ilani zake kwa lengo la kuendeleza, kusimamia na kuimarisha vyombo vya Wananchi ambavyo ni Serikali za Mitaa.

“ Tunaporudi kwa Wananchi ni muhimu tuendelee kuwapa matumaini kuhusu nia na shabaha ya Serikali ya kushirikiana katika kuboresha maisha yao na kuchochea kasi ya maendeleo “. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba yapo mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Mipango ya Sekta tofauti katika Halmashauri za Wilaya kutokana na jitihada kubwa za utoaji na usimamizi wa huduma pamoja na uchocheaji wa maendeleo katika ngazi mbali mbali  ndani ya Serikali za Mitaa.

Akizungumzia migogoro Balozi Seif alieleza kwamba zipo baadhi ya Halmashauri Nchini kutokana na kushindwa kuzingatia misingi ya Utawala Bora zimeingia katika dimbwi la migogoro isiyokwisha.

Alisema kwamba Halmashauri zenye migogoro ya kiutendaji na kisiasa kamwe haziwezi kuwa na maendeleo na hivyo kusababisha kushuka kwa kiwango cha huduma zinazotolewa kwa Wananchi.

Balozi Seif alitanabahishwa wazi kwamba migogoro ya Kidini, Kikabiloa na hata ile ya kijamii ikiachwa iendelee inaweza kuipelekea nchi kuwa katika kipindi kigumu cha kukosa umoja, utulivu na amani miongoni mwa Wananchi wake.

Akigusia maendeleo  yaliyopatikana katika Serikali za Mitaa Balozi Seif alifahamisha kuwa viashiria vingi vya uchumi Mkuu vinaendelea kuimarika ikiwemo ukuaji wa Pato halisi la Taifa, Ukusanyaji wa Mapato, kupunguwa kwa mfumko wa Bei na ongezeko la Mauzo ya Nje.

Alisema wastani wa Pato la Mtanzania limneongezeka kutoka shilingi milioni 1,025,038/- kwa mwaka 2012 hadi shilingi Milioni 1,186,424/- mwaka 2013 sawa na ongezeko la asilimia 15.7%, wakati uchumi wa Taifa umekuwa kwa asilimia 7.0% kwamba 2013 ikilinganishwa na na asilimia 6.9% mwaka 2012.
Alisema kuwa makusanyo ya kodi yameongezeka kutoka wastani wa shilingi Bilioni Mia 117 kwa mwezi mwaka 2005/2006 hadi wastani wa shilingi Bilioni Mia 800 kwa mwezi mwaka 2013.

Aidha alieleza kwamba mfumko wa Bei umepungua hadi kufikia asilimia 6.1% mwezi machi mwaka 2014 ikilinganishwa na asilimia 9.8% mwezi machi mwaka 2013.

Akitoa Taarifa fupi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa ambae pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es salaam Dr. Didasi Massaburi alisema mfumo wa Mikutano wa Jumuiya hiyo ulioanzishwa mwaka 2011 umeleta mafanikio makubwa ndani ya Serikali za Mitaa.

Dr. Massaburi alisema miradi mbali mbali ya kiuchumi na Kijamii imeanzishwa kutokana na vugu vugu la Mikutano hiyo na kutoa fursa pana zaidi kwa wajumbe wake kuwa wazi katika kuwasilisha changamoto zinazozikabili Halmashauri zao.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa  ameipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na washirika wa maendeleo ndani na nje ya Nchi kwa jitihada zao zilizosaidia kufanikisha majukumu ya Jumuiya hiyo ikiwemo Mikutano yake ya kila mwaka.

Akimkaribisha mgeni rasmi kuufungua Mkutano huo wa 31 wa ALAT Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Hawa Abdulrahman Ghasia ameipongeza Manispaa ya Kinondoni kwa kushika ushindi wa mwanzo kwenye mashindano ya kupata Meya Bora kila mwaka.

Waziri Ghasia alisema Manispaa ya Kiondoni imepata ushindi huo kutokana na mipango yake madhubuti ya kukusanya Mapato kwa kutumia mfumo waTeknolojia ya Kisasa wa Kompyuta.

Alisema Manispaa hiyo imefanikiwa kukusanya  mara mbili Mapato yake kutoka Shilingi Bilioni 18 hadi Bilioni 36 kwa Mwaka kazi ambayo haijawahi kufanywa na Manispaa yoyote ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

“ Kutokana na umahiri wa Majaji walioutumia kwenye zoezi la kumtafuta mshindi kwenye Kinyang’anyiro hicho ushindi wa Kinondoni haukuwa na mashaka wala upendeleo, na kama ipo manispaa iliyopindukia kiwango hicho naruhusu itajwe ili tuipokonye ushindi Manispaa ya Kiondoni “. Alisisitiza Waziri Ghasia.

Kupitia Mkutano huo wa 31 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Mhe. Hawa Ghasia alizitaka Manispaa na Halmashauri za Wilaya nyengine Nchini Tanzania kuongeza juhudi ili zikaribie au kupindukia mafanikio yaliyoipata Manispaa ya Kiondoni.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda kuufungua Mkutano huo alipata fursa ya kutembelea maonyesho ya bidhaa na vitu mbli mbali vinavyozalishwa katika Halmashauri mbali mbali hapa  Nchini.

Balozi Seif akiambatana na Mwenyeji wake Waziri anayesimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Hawa Abdulrahman Ghasia pamoja na Viongozi wa Wizara yake na Jumuiya ya Serikali za Mitaa alionyesha kuridhika kwake na ubora wa bidhaa hizo zilizo katika kiwango cha Kimataifa.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.