Habari za Punde

Dk.Shein Aishukuru Halmashauri ya Sherehe za Maadhimisho ya Kitaifa kwa Kufanikisha Sherehe za Miaka 51 ya Mapinduzi.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                       12 Aprili, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameiongeza Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kwa kusimamia vyema maandalizi na kufanikisha maadhimisho ya sherehe za miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hafla fupi ya chakula cha jioni iliyofanyika Ikulu jana kwa ajili ya kuipongeza na kutoa shukrani kwa Halmashauri, Dk. Shein alisema Halmashauri hiyo ilifanya kazi vizuri kwa kushirikiana na kamati zake ndogondogo hadi sherehe hizo kufanyika kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame alizishukuru Kamati Tendaji za Halmashauri hiyo pamoja na vyombo vya habari na vikundi vya sanaa kwa ushirikiano wao hadi kufanikisha sherehe hizo.
Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa inaongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Makamu Mwenyekiti wake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mheshimiwa Haji Omar Kheir ambao wote walihudhuria hafla hiyo.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Mohamed Aboud alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuandaa hafla hiyo ambayo aliielezea kuwa ni uthibitisho sio tu kuwa Halmashauri hiyo na Kamati Tendaji zake zilifanya wajibu wake ipasavyo na zilistahili pongezi lakini pia ni kielelzo cha imani aliyonayo Mheshimiwa Rais kwa wajumbe wa Halmashauri hiyo na Kamati zake.
Aidha Mheshimiwa Waziri alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kushiriki kikamilifu katika ratiba za shughuli mbalimbali za maadhimisho hayo iliyotolewa na Halmashauri hiyo hadi siku ya kilele chake.
Katika mnasaba huo waziri huyo alimhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa Halmashauri hiyo itaendelea kutekeleza wajibu wake kikamilifu katika kufanikisha maadhimisho yajayo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wajumbe wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa, Kamati Tendaji kumi za Halmashauri hiyo, sekretarieti yake pamoja na vikundi mbalimbali vya Sanaa vilivvoshiriki maadhimisho hayo na waandishi wa habari.     


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.