Habari za Punde

Wanachama wa CUF 333 Waomba Ubunge na Uwakilishi katika Jimbo mbalimbali Zanzibar.

Na Haji Nassor, Pemba
JUMLA ya wanachama 333 wa chama cha wananchi CUF, kati yao wanawake wakiwa 22 sawa na asilimia 6.60 na wanaume 311 sawa na asilimia  93.39, wamejitokeza kuomba nafasi za ubunge na uwakilishi kwenye majimbo 18 ya kisiwani Pemba, huku nafasi ya ubunge ikiombwa na wanachama 196.
Taarifa kutoka wilaya nne za Pemba zinaeleza kuwa, kwa nafasi ya uwakilishi wanachama walioomba ni 137, wakiwa wanaume 129 sawa na asilimia 94.16, ambapo wanawake ni nane (8), sawa na asilimia 5.83.
Wawakilishi na wabunge wa sasa, wameripotiwa kuingia tena kwenye kinyang’anyiro hicho, isipokuwa mbunge jimbo la Mtambwe wilaya ya Wete, pekee dk Said na Mwakilishi wa jimbo la Ziwani wilaya ya Chake Chake Mhe. Rashid Seif hawakuchukua tena fomu za kutetea nafasi zao.
Imefahamika kuwa nafasi ya ubunge ndio yenye idadi kubwa ya wanachama hao, ambapo wamejitokeza 196, wakati jimbo Kojani wakijitokeza wanachama 17, kukiwa hakuna mwanamke, yakifuatiwa na majimbo ya Chake chake wakiwa 16, wanawake wawili (2), huku jimbo la Wawi idadi ya wanaume ikiwa sawa, ingawa kumejitokeza mwanamke mmoja.

Aidha majimbo mengine kwa nafasi hiyo yaliojitokeza idadi kubwa ya wanachama, ni jimbo la Mtambile waliojitokeza 15, akiwa mwanamke mmoja idadi hiyo ikiwa sawa na Jimbo la Mtambwe 15 ingawa hakukuna mwanamke aliejitokeza kwa nafasi hiyo.
Majimbo mengine yalioripotiwa kuwepo kwa msuguano mkali kwa nafasi hiyo ya kuelekea bungeni Dodoma, ni Jimbo la Chonga wilaya ya Chake chake kulikojitokeza wanachama 14, akiwemo mwanamke mmoja, ambapo jimbo lililotia fora kwa wanawake kujitokeza kwa wingi ni Jimbo la Ziwani 13, wakiwemo wanawake watano (5).
Majimbo mengine idadi ya wanaume na wanawake kwenye mabano Mgogoni 13 (1), Ole 13 hakuna mwanamke, Mkoani 12, hakuna mwanamke, Tumbe tisa mwanamke mmoja, Kiwani tisa hakuna mwanamke, Wete saba hakuna mwanamke, Konde watano mwanammke mmoja, Chambani watano hakuna mwanamke, Mkanyageni na Micheweni wanne hakuna mwanamke.
Katika hatua nyengine wapo wanachama 137 waliomba nafasi mbali mbali za uwakilishi kwenye majimbo hayo 18 na ikibainika kwamba ni mwakilishi wa Jimbo la Ziwani pekee Rashid Seif, ambae hakurudi, huku majimbo ya Chonga na Wete yakiwa na idadi sawa ya wanachama 12 wote, wanawake wakiwa wawili waili kwa kila jimbo.
Majimbo mengine ambayo kwenye mabano wanawake na nje idadi ya wanachama wote ni Kojani na Gando sita, Mtambwe nane, Ole wanne, Mkoani, Mtambile, Kiwani, Tumbe, pamoja na Konde kuna idadi sawa na wanachama nane kukiwa hakuna mwanamke.
Jimbo la Chambani tisa (mwanamke mmoja), Mkanyageni sita, Micheweni nane (mwanamke mmoja), Mgogoni saba, Chake Chake wanne, Wawi nane (mwanamke mmoja).
Baadhi ya wenyeviti wa CUF wilayani humo, walisema tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 na uchaguzi wa mwanzo mwaka 1995, idadi ya wanachama hasa wanawake kujitokeza kwa wingi hii ni mara ya kwanza.
Aidha Katibu wa CUF Mkoani Tahir Awesu alisema baada ya kazi hiyo, kilichobakia ni hatua za kamati ya uteuzi kufanya majukumu yake na kisha kufuatiwa na ngazi za juu za Chama.
Hivi karibuni waakati akizungumza na wanachama waliomba nafasi mbali mbali ikiwemo ubunge, uwakilishi na udiwani, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Mhe: Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wagombea wa nafasi hizo, kujenga imani na kamati za uteuzi za kuwapata wagombea kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Alisema kamati zote zilizoteuliwa kufanya kazi hiyo zitafanya kazi zake kwa umakini na uadilifu mkubwa, bila ya kujali wadhifa au umaarufu wa mgombea.

Alieleza kuwa kamati zilizochaguliwa zimewekewa vigezo maalum na zitafanya kazi ya kuwateuwa wanachama wenye moyo wa kujituma na kukitumikia chama ili kiweze kupata ushindi.

Akisoma taarifa ya maendeleo ya uteuzi wa wagombea, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF Omar Ali Shehe amesema jumla ya wanachama 310 wamejitokeza kugombea Uwakilishi na Ubunge kwa majimbo 32 ya Unguja.

Amesema hatua inayofuata sasa ni kwa wagombea hao kufanyiwa usaili, kazi inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii ambapo kwa upande wa Pemba tayari kazi hiyo imeshafanyika.

Mkurugenzi huyo ambae pia ni mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake  alisema kwa mara ya kwanza, tangu kuanza kwa chaguzi za vyama vingi mwaka 1995, chama hicho kinatarajia kusimamisha wagombea wa Udiwani katika wadi zote za Zanzibar, hatua inayoonesha kupevuka kwa chama hicho kisiasa.


Harakati za kupata wagombea ndani ya chama cha CUF ndio zimeanza kupambamoto, ili kupata mgombea mmoja kwa kila jimbo la uchaguzi na kwa kila mafasi, ili kujitayarisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini kote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.