Habari za Punde

Bajeti Izingatie Makundi yote


Na Himid Choko, BLW

Mratibu wa Programu ya Jinsia , Wizara ya Uwezeshaji , Ustawi wa Jamii, Vijana Maendeleo ya Wanawake na Watoto   ndugu Halima Abdulrahman  amewahimiza  Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi   kutumia  ushawishi wao kwa nguvu zote, ili kuhakikikisha kwamba bajeti ya serikali na zile za kisekta  zinazingatia   mahitaji ya makundi  mbali mbali katika jamii .

Ndugu Halima ametowa wito huo leo wakati akiwasilisha mada inayohusu  Bajeti na Mtazamo wa Kijinsia katika semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi huko Z- Ocean Hotel Chuwini.

Amesema  kwa kuwa  Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi    ndio waidhinishaji wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya serikali, hivyo  wana  wajibu wa kuhakikisha kwamba  serikali  inapanga bajeti kwa mtazamo wa kuzingatia makundi mbali mbali ikiwemo  kijinsia ni zana inayotusaidia kutekeleza misingi ya utawala bora ambayo ni usawa , uwajibikaji na ufanisi.

Aidha ndugu Halima  amesema  Wawakilishi wanapaswa  kuhakikisha kwamba  bajeti za serikali pia zinazingatia uwepo wa vifungu vitakavyochangia kukuza uwiano na usawa wa kijinsia katika kupata huduma mbali mbali ikiwemo  kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya nchi.

Halima amevitaja Baadhi ya Vifungu ambavyo vinafaa kuzingatiwa katika bajeti kuwa ni pamoja  Vifungu vinavyolenga kukuza ajira kwa wanawake, kukuza upatikanaji wa mikopo na taaluma ya ujasiriamali kwa wanawake na  Vifungu vinavyolenga kutekeleza programu za elimu na Afya kwa wanawake.


Aidha ndugu Halima ametaja vifungu vyengine vinavyofaa kuzingatiwa katika bajeti kuwa ni  Vifungu kwa ajili  ya huduma za hifadhi ya jamii katika kustaafu, kukosa ajira, ugonjwa, uzee na kukosa uwezo wa kufanya kazi  pamoja na vile vinavyolenga  kusaidia kukuza ufanisi katika shughuli za kilimo na kuboresha huduma ya maji mijini na vijijini 

Nae Mkuu wa kitengo cha idadi ya watu Tume ya Mipango Salama Ramadhan Makame  akiwasilisha mada inayohusu  Idadi ya Watu na Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii amesema  hivi sasa kunachangamoto kubwa ya ongezeko la ukuwaji wa  idadi ya watu  linalochangiwa na uzazi, vifo na uhamiaji  hivyo uchambuzi wa kina na mahitaji ya kisera yanahitajika ili kuoanisha  masuala ya idadi ya watu na maendeleo.

Amesema hatua hiyo itasaidia ongezeko la idadi ya watu isiwe kikwazo  bali iwe fursa katika uzalishaji  mali na maendeleo.

Amesema  kutokana na athari nyingi zinazotokana na kasi ya ongezeko la idadi ya watu  katika ardhi na kimazingira ipo haja ya kuaandaa mipango madhubuti ya maendeleo ya utekelezaji halisi wa mipango miji, ujenzi wa nyumba za ghorofa, matumizi ya nishati mbadala na uzazi wa mpango.

Semina hiyo ya siku nne ilikua ni maalum kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  ambao wanatarajiwa kuaza kuijadili Bajeti ya serikali kuazia  kesho (leo Jumatatu) kuwajengea uwezo ili waweze kuijadili vyema bajeti.

Akifunga  semina hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi seif Ali Idd amesema kutokana na taaluma iliyopatikana  katika semina hiyo anatarajia kupata michango mizuri  na  yakujenga  kutoka kwa wajumbe wajumbe  wakati wa mjadala wa bajeti hapo kesho.

Amesema ukuaji na uimarikaji wa uchumi wa taifa unategemea matokeo ya uchaguzi Mkuu ujao ambao anategemea utakuwa wa amani na utulivu.
Amesema  serikali  itahakikisha kwamba tume ya uchaguzi inaendesha uchaguzi wa haki , uhuru na uwazi.

Amesema uchaguzi uliosalama utapelekea kwa wageni, watalii na wawekezaji kuvutika kuja kwa wingi   hatimae kukuza pato la taifa litakalosaidia kuiimarisha uchumi wa taifa.


Aidha amesisitiza suala la umuhimu wa kutunza mazingira na uwazi katika bajeti .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.