Na Ramadhani Ali na Maelezo
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohdraza Hassan Daramsi ameahidi kushirikiana na Ushirika wa Akiba na Mikopo wa Elimu Zanzibar (Elimu SACCOS) kufanya Biashara pamoja ili kuinua hali za maisha ya wananchama wake.
Raza ametoa ahadi hiyo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa 15 Elimu Saccos katika Ukumbi wa wa Judo Amani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Katika kuimarisha mashirikiano hayo Mwakilishi huyo ambae ni mfanyabiashara maarufu Zanzibar amewaeleza wanachama hao kuwa yuko tayari kutoa mikopo na vifaa vya ujenzi wa nyumba bila riba.
Amewataka wanachama hao, ambao wengi ni walimu kutoka Skuli za Mikoa yote mitano ya Zanzibar, kuitumia fursa hiyo ili waweze kujenga nyumba bora za kuishi.
‘’Jiandaeni mimi niko tayari kutoa kila msaada unaohitajika kwa Saccos hii ili kuhakikisha hali za maisha ya walimu zinaimarika,‘’ alisisitiza Mwakilishi huyo.
Aliwakumbusha wanachama hao kuwa unapoingiza siasa, dini ama ukabila katika vikundi vya kiuchumi huwezi kupiga hatua ya kimaendeleo na hatimae ni kufilisika.
Amewapongeza viongozi Elimu Saccos kwa kusimamia mabadiliko makubwa ya uendeshaji wake kwa kuondosha mfumo wa riba na kuelekeza nguvu kujiendesha kwa kufanya biashara.
Katibu Mkuu wa Elimu Saccos Bi. Salma Simai Rajab alisema tayari Ushirika huo umetoa mikopo ya kawaida, dharura na vifaa kwa wanachama 1,640 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja na ina akiba isiyopungua milioni 67.
Bi. Salma alisema Ushirika wa Elimu Saccos ulianzishwa mwaka 1997 ukiwa na wanachama 61 na hivi sasau inawanachama 2534. Idadi ya wanachama imekuwa ikiongeza kila mwaka kutokana na juhudi za viongozi kuwahamasisha walimu kujiunga na mahitaji ya walimu kwa jumla.
No comments:
Post a Comment